Wednesday, July 24, 2019

Bilioni 3.1 zatumika miradi majisafi Siha



Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro imefanikiwa kutekeleza miradi ya maji safi na salama kwa ajili ya wananchi wa wilaya hiyo, ambapo zaidi ya Tsh. bilioni 3.1 zimetumika katika kutekeleza miradi hiyo.

Hayo yameelezwa na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Siha, Valerian Juwal, wakati alipotembelea na kukagua miradi ya maji iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa wilayani humo, hivi karibuni.

“Serikali imeweka kipaumbele katika utekelezaji wa miradi kadhaa ambayo inalenga kuboresha maisha ya watu moja kwa moja na miradi ya maji ni moja wapo ya mpango huo na ndiyo maana na sisi wilayani hapa tumeweka mikakati ya kuhakikisha azma hiyo inafanikiwa”, alisema.

Alisema kuwa miradi ya maji iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa wilayani humo ni pamoja na ule mradi wa maji wa Magadini-Makiwaru ambao alisema unatekelezwa kwa kufanyiwa upanuzi na ukarabati.

“Mradi huu unagharimu jumla ya Tsh. 1,218,470,359.50, ambapo utawanufaisha wananchi wa vijiji vya Wiri, Mawasiliano, Kandashi, Olkolili na Mkombozi”, alisema.

Juwal aliendelea kusema  mrdai mwingine ni ule wa Lawate-Fuka, uliogharimu jumla ya Tsh. 1,499,918,959.43, ambao umehusisha upanuzi na ukarabati, ambao alisema kukamilika kwake kutawanuifaisha wakazi wa vijiji vya Kishisha, Embukoi, Ngaritati na Naibili.

Aliendelea kusema kuwa mradi mwingine ni ujenzi na upanuzi kwa mradi wa Losaa-KIA, ambao utanufaisha wananchi wa eneo la Munge kwa Lazaro Letiyo, Kiruswa-Sinai, Kwa Daniel Philipo na mtaa wa Kobil, ambao alisema umegharimu Tsh. 25,593,000.000.

“Mwingine ni ujenzi wa mradi wa maji wa Magadini Makiwaru kutoka Gararagua-Dutchcorner kwenda Kilingi, Kilali, Melari na Sanya Hoyee, ambao unagharimu Tsh. 368,755,475.05”, alisema.

Aidha aliutaja mradi mwingine kuwa ni ule wa Magadini-Makiwaru, unaotoka Dutchcorner kwenda tawi la Kilali, uliogharimu Tsh. milioni 70, ambao alisema utahusisha ujenzi wa vituo nane vya kuchotea maji.

0 Comments:

Post a Comment