Monday, July 1, 2019

Utani ni nini?

Cartoon: CREDIT...Supa Deo
Utani ni utanzu mojawapo wa fasihi simulizi. Asili ya utani ni kitenzi kutania chenye maana ya kumfanyia mtu mzaha au stihizai. Fani hii ni ya kipekee katika fasihi simulizi.

Ina sehemu kubwa katika maisha ya kila siku. Kila wakati katika jamii za Kiafrika ulikuwa ni wakati wa vichekesho na furaha kupitia kwa utani. Utawasikia watu wakitaniana kazini, arusini, ngomani, vilabuni na hata matangani! Zamani, utani ulitekeleza jukumu la kuliwaza wafiwa nyakati za kilio au maombolezo kama njia ya kuondoa huzuni.

Aghalabu utani hufanywa kwa njia ya malumbano. Mtu mmoja humtania mwenzake, naye mwenzake humjibu papo hapo kwa utani. Hii ndio sababu ukaitwa malumbano ya utani. Fani hii ya utani japo imepotea katika jamii nyingi, ni fani iliyostawi sana katika jamii nyingi za Kiafrika.

KOMEDIA
Hata hivyo imeanza kujitokeza hapa na pale katika komedia na katika vyombo vya mawasiliano. Kumbuka utani wa Mwana- komedia Owago Nyiro: ’Ujaluo Utakuua!’Katika kiwango cha watoto, utani unajitokeza kupitia mchongoano ambao ni maarufu sana kwa watoto. 

Kwa ajili ya maelezo haya, utani unaweza kugawanywa katika mafungu yafuatayo: i. Utani kati ya ukoo(mbari) na ukoo ii. Utani kati ya jamaa au ndugu iii. Utani kati ya kabila moja na jingine. Mpaka sasa, kuna makabila ambayo ni 'watani’ wa jadi, yaani,wanaweza kutaniana bila yeyote kuudhika wala kulalamika.

Mathalan, Mzaramu na Mdigo; Mturkana na Mkikuyu,Msukuma na Mnyamwezi n.k. Almradi kila jamii ina watani wake. iv. Utani wa kirafiki/kati ya marafiki v. Utani kati ya watu wa jamii moja wanaoishi katika wilaya tofauti:k.m. 

Wakikuyu wa Kiambu/Kabete,Muranga/Metumi na Nyeri/Gaki ndigi maguru (kamba miguuni), wana namna yao ya kutaniana na hata kuimbiana nyimbo za utani.

JAMII MBALIMBALI
Miongoni mwa Waluyia, Wabukusu na Wamaragoli ni watani.Miongoni mwa Wakalenjin, Wanandi hutaniana na Wakipsigis, ilhali miongoni mwa Wamijikenda, Wadigo ni watani wa Wagiriama,kama sikosei. 

Utani hutokea katika jamii hizi kwa watu kufanyiana stihizai au masihara bila yeyote kuudhika. Ajabu ni kuwa jambo lile lile la utani likisemwa na mtu ambaye si mtani wa jadi wa jamii husika, utamsikia mwenye kutaniwa akilalamika:

Aisee! tuheshimiane,tafadhali usinitanie; mimi sio mtani wako yakhe!’ Utani huu unapotokea, huwa unatekeleza dhima fulani kama vile: kukejeli/kuumbua, kuburudisha/kuchekesha, kukosoana/kujengana, kuhifadhi mila na desturi, kuadilisha/kufunza maadili,kuadibu/kutia adabu n.k. 

Aidha,utani hujenga uhusiano na maelewano mazuri baina ya wale wanaotaniana.

ELIMU
Halika dhalika, utani baina ya wazee na wajukuu wao hulenga kutoa elimu ya mwanzo kwa watoto. Kwa mfano, katika utanzu huu, babu na bibi wamepewa jukumu la kutaniana na wajukuu wao ili kuwatolea elimu na kuwahamasisha kimaadili. 

Wazazi wanapotoa elimu hii, huwa ni kwa njia ya kukemea isiyo na upole. Lakini babu na bibi wanapotoa elimu hii, huwa sio kwa ukali bali kwa upole. Hawa huwatania wajukuu wao hata kwa mambo yanayoweza kuonekana kuwa ya aibu kwa wazazi ili kuwalainisha. 

Utani wa babu na bibi hufanyiwa wajukuu wakiwa bado wadogo. Wakishakwea ngazi ya utu uzima, huacha kutaniwa.

MJUKUU
Wakiwa wadogo si ajabu kumsikia babu akimtania mjukuu wake wa kike:’ Nimekwisha kukuoza kwa yule mwendawazimu anayezurura pale sokoni; hata mahari tayari nimekwisha yapokea!’ 

Haya yanaelezewa kumkosoa anayetaniwa kuwa haandami maadili yanayotukuzwa na jamii na angehitajika kujistahi kama anataka kuolewa na mume wa maana. 

Sifa mojawapo ya utani ni kuwa watani hujua ni lini na kwa kiasi gani na nani wa kumtania, kutegemea mila na ada za jamii husika. Hii ni kwa kuwa utani una mipaka.Katika utani, ni lazima watu waheshimiane. Utani hufanywa na watu wanaoelewa lugha ya jamii yao vizuri.

BIBI
Mathalan katika jamii nyingi, mjukuu wa kiume wa kwanza huchukuliwa na bibi kuwa 'mume wake’Hii ni kwa sababu yeye hupata jina kutoka kwa mumewe. Leo hii, watoto hawauelewi utani wa bibi na babu. 

Mtoto aliyelelewa mjini akipelekwa kumsalimu bibi au nyanyake na kutaniwa kwa salamu 'karibu nyumbani mume wangu’na bibi, atashangaa kwa nini nyanya jizee liseme kuwa yeye ni mume wake! Hata hivyo, ni kawaida kwa watu kutaniana hata siku hizi. 

Ingawa mabadiliko katika mfumo wa kijamii ni tisho kwa asasi hii, utani bado upo.

SOURCE: Alex Ngure

0 Comments:

Post a Comment