Kwanza poleni kwa kazi
kubwa mlioifanya, hakika kuwa na degree ni ndoto ya vijana wengi. Kwa juhudi
zenu na kwa baraka za Mola mumeweza kumaliza salama. Ila kuna kitu kidogo
ningependa kuongea na nyinyi.
Huku mtaani mnapoingia ni
tofauti na chuo, maisha ya mtaa kamwe usifananishe na chuo. Huku mambo magumu
kidogo zaidi ya chuo, huku unatakiwa kuishi kwa busara na hekima zaidi ili
uweze kutimiza malengo yako.
Yule mjomba aliyekwambia
mtumie CV ukimaliza chuo tu anakuajiri usishangae akikuzimia simu. Yule danga
aliyekuchezea kipindi upo chuo huku akikwambia ukimaliza anakuajiri usishangae
akaanza kuwa busy kupitiliza.
Wale marafiki uliokuwa
unakula nao bata hutawaona tena, utakuwa nyumbani na bibi yako akiwa na
matumaini kesho unaingia kazini ili uweze kununua yule ng'ombe aliyemuuza ili
kukusomesha. Utakuwa wewe na familia yako huku wakitegemea makubwa kutoka
kwako.
Kwa bahati mbaya huku
mtaani ni gombania goli, kila mtu anatafuta nafasi ya kuajiriwa ili aweze
kusaidia familia yake. Acha kujishaua eti bila milioni sifanyi kazi. Labda
nikwambie tu, huku kuna watu wana fegree kama yako na wana miaka mitatu hawana
ajira.
Ogopa sana kukaa nyumbani
bila kufanya kazi au chochote kile, jaribu kuwa msaada kwa familia kwa kitu
chochote unachoweza kufanya kipindi hiki unasubiri ajira. Jitolee maofisini,
jiajiri, fanya biashara au kitu chochote kile ambacho kitakuwa msaada kwa wewe
na familia yako.
0 Comments:
Post a Comment