Mwaka 1960 Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika
kwa uzalishaji wa zao la katani ikizalisha tani 230,000; miaka 20 baadaye
ilianguka na kufikia tani 32,000 kwa mwaka. Mnamo mwaka 1997 Tanzania ilikuwa ikizalisha
tani 19,000. Sababu nyingi zinaelezwa ikiwamo kuingia kwa kamba za plastiki.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa ameshika katani iliyokua imeanikwa, wakati alipotembelea
shamba la katani la Hassan Sisal Estate Makanya, wilayani Same katika mkoa
Kilimanjaro Julai 19.2019. Anayetoa maelezo ni Meneja Mshauri wa shamba hilo,
Ndekirwa Nyari Julai 19,2019. (PICHA KWA HISANI YA OFISI YA WAZIRI MKUU)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa
Makanya wajipange na kutafuta maeneo ya ekari tatu hadi nne ili nao waanze
kulima mkonge.
Majaliwa aliyasema hayo wakati akizungumza na
wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata katani kilichopo kwenye shamba la mkonge
la Hasani, kata ya Makanya, wilayani Same, Kilimanjaro, mara baada ya kukagua
uzalishaji kwenye kiwanda hicho.
“Niwasihi wananchi wa hapa na vijiji jirani ingieni kwenye
kilimo cha mkonge kwa sababu kina soko ndani na nje ya nchi. Tafuteni maeneo ya
ekari tatu au nne anzisheni kilimo cha mkonge sasa. Zao hili lipo kwenye mazao
ya nyongeza ya mkakati ambayo ni chikichi na mkonge.”
“Na uzuri wake unalima mara moja tu, halafu kila mwaka
unakuwa unavuna tu. Viongozi wa Serikali ya Kijiji simamieni jambo hili,”
alisisitiza.
Mazao mengine ya mkakati ambayo Serikali ya awamu ya
tano ilianza kuyatilia mkazo ili kuimarisha uzalishaji wake, upatikanaji wa
pembejeo na masoko ni pamba, chai, tumbaku, kahawa na korosho.
Mapema, akitoa taarifa juu ya uzalishaji kwenye kiwanda
hicho, Nyari alisema shamba lote lina ukubwa wa ekari 2,453 na kwamba
uzalishaji umekuwa ukiongezeka kidogo kidogo ambapo mwaka 2014 walizalisha tani
za mkonge 713 na hadi kufikia mwaka 2018 walifikisha tani 890 za mkonge. “Mwaka
huu tunatarajia kufikisha tani 1,080 kwa sababu eneo lililopandwa mkonge
limeongezeka,” alisema.
Alisema moja ya changamoto inayowasumbua ni tabia ya
wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yenye mkonge mchanga hali ambayo
alisema inaua miche hiyo michanga.
Aliitaja changamoto nyigine kuwa ni ukosefu wa maji ya
uhakika, hali ambayo inawafanya washindwe kuzalisha singa za katani ambazo ni
safi.
0 Comments:
Post a Comment