Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Julai 18, 2019 katika ukumbi wa mikutano wa ndani kwa Watumishi wa Serikali. |
WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim
Majaliwa amewataka watumishi wa umma katika wilaya na mikoa nchini kufanya kazi
kulingana na falsafa ya kiongozi wa nchi ambaye kwa sasa ni Rais Dkt. John
Pombe Magufuli ili kuwaletea wananchi maendeleo.
1. KUFANYA KAZI KWA KUFUATA PHILOSOPHY YA JPM
Akizungumza katika mkutano wa ndani na watumishi wa
serikali kutoka wilaya za Moshi Mjini, Mwanga na Same katika ziara yake mkoani
Kilimanjaro iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura Julai 18 mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kumekuwa na
watumishi wa serikali ambao wamekuwa wakifanya kinyume na matakwa ya kiongozi wa
nchi hali inayosababisha mambo kwenda mrama katika taasisi za umma.
“Fanya kazi kwa maelekezo ya kiongozi wa nchi, iga
philosophy (falsafa) yake, itakurahisishia kufanya kazi bila wasiwasi wowote.
Wafanyakazi wengi wamekuwa wakishindwa kutekeleza majukumu yao kwa kushindwa
kufuata falsafa ya kiongozi wa nchi,” alisema Majaliwa.
2. KUACHA UBAGUZI WA KISIASA, UKABILA NA UWEZO WA MTU
Katika mkutano huo wa ndani wa kuwakumbusha watumishi wa
serikali wajibu wao Waziri Mkuu aliwataka watumishi hao kuondokana na ubaguzi
wa rangi, ukabila, vyama vya siasa na uwezo wao kwani kwa kufanya hivyo
maendeleo ya nchi yatafikiwa bila wasiwasi.
“Usiwe sehemu ya kuifanya serikali kuwa ya hovyo,
msimamo wa serikali hii haumlindi mtumishi yeyote wa serikali endapo
atathibitika kufanya hayo,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Aidha Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa serikali katika
halmashauri zao kuheshimiana na kutambuana ili kujenga mahusiano bora mahali pa
kazi.
3. KUHESHIMIANA ILI KUJENGA MAHUSIANO MAZURI
“Msipotambuana mtavurugana, mnapaswa kuheshimiana kila
mmoja kwa nafasi yake, kila mmoja akijiona yupo juu ya mwenzake hakutakuwa na
mahusiano mazuri,” alisema Majaliwa.
Majaliwa aliongeza kuwa kuna umuhimu wa kutambua mamlaka
na kufanya kazi kama timu ili kuijenga nchi ya Tanzania, kutokana na ukweli
kwamba kumekuwa na tabia ya baadhi ya wafanyakazi wa halmashauri fulani fulani
nchini kudharau madiwani na kuwaona sio kitu.
“Kuna majimbo na wilaya hapa nchini hazielewani.
Isipokuwa sijasikia kwa hapa
Kilimanjaro, naona pako shwari…ni jambo zuri na la
kupongeza,” alisema Waziri Mkuu.
Hata hivyo Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa idara katika
halmashauri husika wasiwe wachoyo katika kutoa nafasi kwa watumishi wengine
kupata uzoefu katika kazi ili kujenga serikali imara.
4. WAKUU WA IDARA NA KUJENGA TEAM WORK
“Gawanya majukumu, wapeni nafasi ndani ya idara, kila
siku semina ni wewe tu, mara Dar, mara Dodoma, wakiona umevaa suti nzuri
wanafikiri ni fedha za kwenye safari zako, maana hutulii ofisini…wape nafasi muwe
na lugha moja,” aliongeza.
5. MATUMIZI YA LUGHA RAHISI KUWASILISHA UJUMBE
Waziri mkuu aliwataka watumishi wa serikali kuachana na
kauli za kuwatisha wananchi, na kuwataka kutumia kauli nyepesi zenye kueleweka
ili kutengeneza jamii ambayo itakuwa na ushirikiano kwani serikali haina uwezo
wa kufanya kila kitu isipokuwa kwa ushirikiano na wananchi inaweza.
Ziara ya Waziri Mkuu katika Mkoa wa Kilimanjaro ni ya
pili baada ya ile ya kwanza aliyozuru wilaya za Siha, Hai na Rombo na sasa
akizuru Moshi Mjini, Mwanga na Same.
STORY BY: Jabir Johnson Moshi…Julai 18, 2019
STORY BY: Jabir Johnson Moshi…Julai 18, 2019
0 Comments:
Post a Comment