Monday, July 29, 2019

Jukwaa la Walimu Wazalendo Kilimanjaro latoa saruji mifuko 547

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole.

Jukwaa la Walimu Wazalendo wa shule za msingi na sekondari Mkoa wa Kilimanjaro,  wameunga mkono juhudi za utendaji kazi ambazo zinafanywa na rais Dkt. John Pombe  Magufuli  kwa kutoa, mifuko ya saruji  547 kwa ajili ya kuunga mkono shughuli za maendeleo mkoani humo.

Akizungumza mara baadha ya  kukabidhi  mifuko hiyo ya saruji kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM) Taifa,  Mwenyekiti wa Jukwaa la Walimu Wazalendo mkoa wa Kilimanjaro George Madaraka, alisema mchango huo umetolewa kutoka kwa Walimu Wazalendo kutokana na kutambua mchango wa serikali ya awamu ya tano katika utoaji wa elimu pasipo malipo.

“Kutokana na jinsi serikali  inavyotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, nasi tumeona ni vema kuiunga mkono kwa kuchangia saruji  mifuko 232 ili kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa, vyoo vya wasichana na wavulana pamoja na kujenga kituo cha polisi Usangi wilaya ya Mwanga,”alisema Madaraka.

Madaraka alisema Jukwaa la Walimu Wazalendo waliweza kujichanga na kufanikisha kupata mifuko ya saruji 232 ambayo waliikabidhi kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole.

Kwa Upande wake mgeni rasmi ambaye alizindua Jukwaa la Walimu wazalendo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey Polepole,  pia aliwasaidi kuendesha harambee na kuwezesha kupatikana mifuko ya saruji 315, ambapo yeye mwenyewe alichangia mifuko ya saruji 30.

“Niwapongeze kwa kazi kubwa mliyoifanya Jukwaa la Walimu Wazalendo mkoa wa Kilimanjaro, katika kuunga mkono jitihada za serikali,”alisema Polepole.

“Naomba nielekeze mifuko hii iliyopatikana hapa, mifuko ya saruji 127 ipelekwe Wilaya ya Mwanga kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi Usangi,  pia mifuko ya saruji 30 ipelekwe katika Wilaya ya Rombo kwa lengo la kujenga  matundu ya vyoo katika shule, huku mifuko itakayobaki 370 Katibu wa CCM mkoa ataelekeza wapi ipelekwe kwa ajili ya kusaidia maendeleo,”alisema.

Nae Afisa Elimu Mkoa wa Kilimanjaro Paulina Nkwama, alisema kuhusiana na elimu msingi bila malipo mkoa huo, unapokea shilingi takriban bilioni 1.27 kila mwezi , ambazo zinawasaidia katika masuala ya uendeshaji wa shule pamoja na posho ya madaraka kwa viongozi.

Aidha alisema katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 mkoa umepokea takriban shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu, jambo ambalo wanaendelea kuipongeza serikali.

STORY BY: Kija Elias na Jabir Johnson, Moshi….Julai 29, 2019
Jukwaa la Walimu Wazalendo wa shule za msingi na sekondari Mkoa wa Kilimanjaro, katika picha ya pamoja na Humphrey Polepole.


0 Comments:

Post a Comment