Friday, July 5, 2019

Geita mbioni kuanzisha kampeni kumuokoa mtoto wa kike dhidi ya vikwazo



Watoto wengi wa kike wanazongwa na vikwazo vingi vinavyowafanya washindwe kutimiza ndoto zao, vikiwamo umaskini, mila, desturi kandamizi. Vikwazo hivyo vimeufanya mkoa wa Geita kuwa mbioni kuanzisha kampeni yenye malengo ya kumwokoa mtoto wa kike dhidi ya changamoto zinazomkabili.

Mkuu wa mkoa wa Geita Mhandisi Robert Bagriel, aliyasema akiwa mkoani Kilimanjaro, wakati wa hafla fupi ya kuwapokea wapanda mlima 64  waliopanda mlima kwa lengo la kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa watoto wa kike wamekuwa waathirika wakubwa wa maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi, hivyo kuna haja kubwa ya kuongeza hamasa katika jambo hilo ili kuwakinga na maambukizi mapya watoto wa kike.

“Kuanzisha kwa kampeni ya upandaji Mlima Kilimanjaro, inayolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi (GGM Kilimanjaro HIV and AIDS Challenge, mimi imenisukuma kwenda kuanzisha kampeni maalum mkoani kwangu ya kumuokoa mtoto wa kike,”alisema Mhandisi Gabriel.

Alisema kuwa takwimu  zinaonyesha kuwa kiwango cha wasichana sita kati ya kila 10 wanakuwa kwenye maambukizi mapya, mimi kama Mkuu wa Mkoa wa Geita naondoka nayo, nikifika Geita nitaanzisha kampeni maalum itakayokuwa na lengo la kumuokoa mtoto wa kike”, alisema.

Akiongea wakati wa kuwapokea wapanda mlima hao, Makamu wa rais wa kampuni ya Anglo Gold Ashanti kupitia mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) Simon Shayo  alisema zaidi ya taasisi  50 zinazojihusisha na kampeni dhidi ya Ukimwi zimeshanufaika na kampeni hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2002.

“Tangua kuanzishwa kwa kampeni hii zaidi ya shilingi bilioni 13 zimesha kusanywa  katika kampeni hiyo tangu ianzishwe na kuungwa mkono na mashirika mbalimbali yasiyo kuwa ya kiserikali,”alisema.

Alifafanua kuwa mbali na taasisi hizo pia watoto yatima wengi wamenufaika na kampeni hiyo kwa kupata elimu, ambapo alisema tayari kuna ambao wako katika shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu mbalimbali pamoja na vyuo vingine vya elimu ya juu.

Nae Kaimu mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS) Jumanne Isango, alisema kuwa ipo haja ya kuongeza nguvu  katika kukabiliana na changamoto ya mapambano dhidi ya Ukimwi.

Awali akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt Anna Mghwira, aliwapongeza wadau wengine ambao wamejitokeza kuiunga mkono GGM katika kampeni hiyo zikiwemo taasisi za Serikali, ambapo alisema kujitokeza kwao kunazidi kuipa nguvu kubwa kampeni hiyo.

STORY BY: Kija Elias

0 Comments:

Post a Comment