Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro imefanikiwa
kutekeleza miradi ya maji safi na salama kwa ajili ya wananchi wa wilaya hiyo,
ambapo zaidi ya Tsh. bilioni 3.1 zimetumika katika kutekeleza miradi hiyo.
Hayo yameelezwa na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya
ya Siha, Valerian Juwal, wakati alipotembelea na kukagua miradi ya maji
iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa wilayani humo, hivi karibuni.
“Serikali imeweka kipaumbele katika utekelezaji wa
miradi kadhaa ambayo inalenga kuboresha maisha ya watu moja kwa moja na miradi
ya maji ni moja wapo ya mpango huo na ndiyo maana na sisi wilayani hapa
tumeweka mikakati ya kuhakikisha azma hiyo inafanikiwa”, alisema.
Alisema kuwa miradi ya maji iliyotekelezwa na
inayoendelea kutekelezwa wilayani humo ni pamoja na ule mradi wa maji wa
Magadini-Makiwaru ambao alisema unatekelezwa kwa kufanyiwa upanuzi na
ukarabati.
“Mradi huu unagharimu jumla ya Tsh. 1,218,470,359.50,
ambapo utawanufaisha wananchi wa vijiji vya Wiri, Mawasiliano, Kandashi,
Olkolili na Mkombozi”, alisema.
Juwal aliendelea kusema
mrdai mwingine ni ule wa Lawate-Fuka, uliogharimu jumla ya Tsh.
1,499,918,959.43, ambao umehusisha upanuzi na ukarabati, ambao alisema
kukamilika kwake kutawanuifaisha wakazi wa vijiji vya Kishisha, Embukoi,
Ngaritati na Naibili.
Aliendelea kusema kuwa mradi mwingine ni ujenzi na
upanuzi kwa mradi wa Losaa-KIA, ambao utanufaisha wananchi wa eneo la Munge kwa
Lazaro Letiyo, Kiruswa-Sinai, Kwa Daniel Philipo na mtaa wa Kobil, ambao
alisema umegharimu Tsh. 25,593,000.000.
“Mwingine ni ujenzi wa mradi wa maji wa Magadini
Makiwaru kutoka Gararagua-Dutchcorner kwenda Kilingi, Kilali, Melari na Sanya
Hoyee, ambao unagharimu Tsh. 368,755,475.05”, alisema.
Aidha aliutaja mradi mwingine kuwa ni ule wa
Magadini-Makiwaru, unaotoka Dutchcorner kwenda tawi la Kilali, uliogharimu Tsh.
milioni 70, ambao alisema utahusisha ujenzi wa vituo nane vya kuchotea maji.