Wednesday, February 22, 2017

Raia 14 wa India wapandishwa kortini Kisutu

NA MWANDISHI WETU
Raia wa India wafanyakazi kwenye Kampuni la Quality Group Ltd wakiwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Februari 22, 2017.
Raia wa 14 wa India ambao wanafanya kazi Quality Group wamefikishwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu likiwemo la kufanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali.
Hati ya mashtaka, iliyosomwa na mwendesha Mashtaka Method Kagoma mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha imewataja washtakiwa hao kuwa ni Rojat Surkar na wenzake kumi na watatu.
Imedaiwa mahakamani hapo kuwa Februari 13, mwaka huu, katika ofisi ya Quality Group Ltd iliyopo katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikutwa wakiwa na viza zilizoghushiwa.
Katika shtaka la pili imedaiwa kuwa siku na mahali hapo washtakiwa hao wakiwa raia wa India walikutwa wakiishi nchini Tanzania bila ya kuwa na kibali.
Hata hivyo, washtakiwa hao ambao wanatetewa na mawakili watatu, Alex Mgongolwa na Hudson Ndusyepo wamekataa kujihusisha tuhuma hizo na wako nje kwa dhamana.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 7, mwaka huu.

0 Comments:

Post a Comment