Monday, February 13, 2017

Dangote kufungua viwanda 10 vya sukari Ethiopia

ADDIS ABABA, ETHIOPIA
Aliko Dangote
MFANYABIASHARA namba moja kwa utajiri barani Afrika Aliko Dangote yupo mbioni kufungua viwanda 10 vya sukari nchini Ethiopia.
Vyanzo vya nchini Ethiopia vinasema tajiri huo raia wa Nigeria ameshajenga viwanda viwili katika eneo la Omo Kuraz na Beles na kwamba vimeanza kufanya kazi tangu mwishoni mwa mwezi uliopita.
Waziri wa Masuala ya Ujasiriamali wa Ethiopia Girma Amente amesema mpaka mwaka 2020 wanataka kuwa na viwanda 13 vya uzalishaji wa sukari.
Shirika la Sukari la Ethiopia limesema wameshaingiza sukari tani 200,000 kutoka nje huku likiongeza kusema uzalishaji wa zao hilo umekuwa hauzidi tani 400,000.
Kuingia kwa Dangote nchini humo kutafikia malengo ya taifa hilo kuzalisha tani 700,000 kwa mwaka.
Kwa miaka mingi Dangote amekuwa akiingiza sukari katika nchi mbalimbali barani Afrika kutoka Brazil.
Tangu mwaka 2001 hadi sasa Dangote amekuwa na hekta 200,000 za mashamba ya miwa ambapo nchini Ethiopia alionyesha nia ya kuwekeza mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Forbes Dangote anakadiriwa kuwa na utajiri wenye thamani ya dola Bilioni 12.4 akishika nafasi ya kwanza Afrika kwa miaka sita mfululizo na nafasi ya 51 duniani mwaka uliopita

Maendeleo ya Sukari nchini humo yatapungua tatizo la ajira kwani zaidi ya Waethiopia 350,000 watajipatia ajira  na ifikapo mwaka 2020 itakuwa imetoa ajira 600,000.

0 Comments:

Post a Comment