Monday, February 6, 2017

JPM ampaisha Makonda vita dawa za kulevya

NA MWANDISHI WETU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameitaka mahakama kuendesha kesi za Dawa za Kulevya haraka iwezekanavyo pindi ushahidi unapopatikana kutokana na kesi hizo kukaa muda mrefu bila kusikilizwa.
Hayo yanajiri siku chache baada ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuendesha vita dhidi ya wanaodaiwa kuwa kujihusisha na dawa za kulevya.
Akizungumza katika hafla ya kuapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ikulu jijini Dar es Salaam leo asubuhi amesema katika vita hiyo haipaswi kuwachekea wanaojiita watu maarufu endapo watapatikana wakijihusisha na biashara hiyo wanapaswa kufikishwa mahakama mara moja.
Aidha Rais Magufuli ameunga mkono jitihada za wadau wanaopinga biashara hiyo wakiwamo Makonda na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu kwa kusema kuwa watakutana na vipingamizi lakini watapaswa kuifanya hata kama ni ngumu.
Ongezeko la biashara ya dawa za kulevya barani Afrika, limeongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya hasa vijana wadogo na kuongeza  vitendo viovu vinavyofanywa na magenge ya kihalifu. 
Katika hafla hiyo Rais Magufuli amemwapisha Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo aliyechukua nafasi iliyoachwa na Jenerali Davis Mwamunyange, Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Luteni Jenerali James Mwakibolwa, Kamishina Jenerali wa Magereza Juma Malewa, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Nyakimura Muhoji, mabalozi Paulo Meela kuwa balozi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Samuel Shelukindo kuwa balozi wa Tanzania nchini Ufaransa.
Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo akiapa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. (Picha zote na Ikulu)




0 Comments:

Post a Comment