Friday, February 3, 2017

Polisi Songwe lawamani

SONGWE, MBEYA
JESHI la polisi mkoa wa Songwe limetupiwa lawama kwa kitendo cha baadhi ya askari wa usalama barabarani wilaya ya Mbozi kuanzisha utaratibu wa kuwatoza shilingi 30,000 kila abiria anayekutwa amepanda magari ya mizigo yanayoelekea maeneo ya vijijini.
Inadaiwa wanaotozwa kiasi hicho cha fedha wanaposafiri kwenda vijiji vya Igamba, Harungu Utambalila, Chitete na Kamsamba wilayani Momba kutokea Vwawa na Mlowo ambako ni maeneo ya mjini.
Wakazi wa mkoa huo wamesema miundombinu mibovu ya barabara zinazounganisha wilaya moja na nyingine za Songwe ni miongoni mwa changamoto inayowakabili.
Wameongeza kuwa usafiri mkubwa unaotumiwa na wananchi kutoka maeneo ya vijijini  kuingia mjini kuuza mazao yao na kupata mahitaji mbalimbali ni usafiri wa magari ya mizigo kwani hakuna usafiri wa mabasi.
Diwani wa kata ya Itumpi Richard Mahaya akitoa masikitiko yake mbele ya Mkuu wa wilaya ya Mbozi juu ya utaratibu huo wa baadhi ya askari wa usalama barabarani kuwatoza faini katika suala la usafiri tena bila hata kutoa risiti amesema kitendo hicho ni unyanyasaji.
 Mkuu wa wilaya ya Mbozi John Palingo amekiri kuwepo kwa tuhuma hizo huku akiahidi kulifanyia kazi jambo hilo.

0 Comments:

Post a Comment