Wednesday, February 22, 2017

Shahidi Namba 5 kesi ya Scorpion atinga mahakamani leo

NA MWANDISHI WETU
Salum Njwete (katikati) akitoka katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Oktoba 19, 2016
USHAHIDI wa kesi inayomkabili Salum Njwete maarufu Scorpion umeendelea kusikilizwa leo katika mahakama ya wilaya ya Ilala huku shahidi wa tano ambaye ni daktari akidai kuwa mlalamikaji angechelewesha kufikishwa hospitalini angepoteza maisha.

Imedaiwa mahakamani hapo kuwa Septemba 6 mwaka jana Scorpion mwenye miaka 34 akiwa Buguruni Shell alimchoma kwa kisu mlalamikaji Said Mrisho machoni, mabegani na tumboni kisha kumnyang’anya vitu vya thamani na fedha taslimu.

Mwendesha Mashtaka Gloria Mwenda akisaidiwa na Sylivia Mitanto, mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule wamedai kuwa kesi ya mshtakiwa huyo mwenye miaka 34 inaendelea kwa mashahidi kuisaidia mahakama kufikia mwafaka wa shauri hilo.

Shahidi huyo ambaye ni daktari wa kitengo cha upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ameiambia mahakama kuwa jeraha la mlalamikaji upande wa kushoto wa tumbo lilitokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali ikiwa ni sentimeta 30 kutoka kwenye utumbo mwembamba.

Pia ameongeza alimpeleka mgonjwa katika chumba cha upasuaji na kulifumua tumbo zima ili kujua kama damu ilisambaa na baadaye alimshona utumbo wa ndani uliokuwa umepasua kisha akamalizia kumshona nje na kumpeleka wodini kuendelea na matibabuu ya kawaida.
Kesi hiyo itatajwa tena Machi 8 na kuendelea kusikilizwa Machi 13 mwaka huu.


0 Comments:

Post a Comment