NA FELISTA HENRY
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) wanatarajia kutoa mafunzo ya majuma
mawili kwa mafundi na waendelezaji wa vyanzo vya umeme unaozalishwa kutokana na
rasimali za nishati jadidifu.
Serikali kupitia REA imeanza utekelezaji wa mradi kabambe wa awamu ya tatu
wa kusambaza nishati vijijini utakaojumuisha vijiji 7,873 katika wilaya na
mikoa yote ya Tanzania Bara ambao utatekelezwa kuanzia mwaka huu wa fedha hadi
2020/21.
Mkurugenzi Mkuu wa Nishati vijijini Mhandisi Boniface Gissima amesema malengo
ya mafunzo hayo ambayo yataanza mwishoni mwa Aprili hadi Juni mwaka huu ni kuwajengea uwezo
mafundi na waendelezaji wa teknolojia waliopo maeneo ya vijijini ili waweze
kutoa huduma bora na endelevu.
Mikoa itakayohusika na mafunzo hayo ni Mara, Geita, Tabora, Simiyu na
Arusha ambako mafunzo kuhusu nishati itokanayo na mionzi ya jua na utayarishaji
wa mpango biashara yatatolewa.
Hata hivyo Gissima
amewataka waombaji wa mafunzo hayo wawe na elimu ya kidato cha nne huku wenye
vyeti vya ufundi VETA daraja la kwanza
watapewa kipaumbele na watume kabla ya Machi 17 mwaka huu.
0 Comments:
Post a Comment