Tuesday, February 28, 2017

Google yakubali mchango wa ‘Malaika wa Rehema’ Abdul Sattar Edhi

CALIFORNIA, MAREKANI
Abdul Sattar Edhi enzi za uhai wake
KAMPUNI ya Google iliyo maarufu kwa utoaji wa huduma za intaneti na bidhaa zake imemkumbuka mwanzilishi wa Edhi Foundation aliyejitolea maisha yake kuwasaidia watoto maskini tangu akiwa na miaka 20 kwa kuchapisha picha za mfano kwenye nembo yake. 
Google walivyokubali mchango wake Februari 28, 2017 katika nembo yao.
Huyo ni Abdul Sattar Edhi ambaye alifariki mwaka uliopita akiwa na miaka 88, baada ya figo kushindwa kazi. Angekuwa hai leo ingekuwa siku ya kusheherekea kuzaliwa kwake miaka 89 iliyopita.Kinachostaajabisha kwa Edhi maarufu  ‘Malaika wa Rehema’ hakuwahi kupata Tuzo ya Amani ya Nobel kutokana na mchango wake mkubwa kwa watu maskini.
Hata alipokuwa anasumbuliwa na maradhi ya figo alikataa kwenda kutibiwa nje na huduma zote alizipata katika hospitali ya serikali nchini humo.Mwaka 2015 kupitia Edhi Foundation alifanya changizo la hiari la dola 100,000 za Marekani kwa ajili ya waathirika wa kimbunga cha Katrina.Edhi alizaliwa katika mji wa Bantva Gujarat nchini India kabla ya mgawanyiko wake na Pakistan Februari 28, 1928.
Google imetambua thamani ya mwanzilishi huyo kwa kusambaza nembo yake yenye mfano wa sura yake na magari ya wagonjwa ya Edhi Foundation. Akiwa amesambaza magari ya wagonjwa zaidi ya 1,800 kwenye maeneo mbalimbali nchini Pakistan, mwaka 1997 aliingia katika rekodi za dunia za Guiness kwa kuwa na shirika kubwa la kujitolea lenye magari ya wagonjwa.  
Edhi ataendelea kukumbukwa kwa kauli zake kuwa hakuna dini kubwa kama utu, hata kama mtu akisoma bado utu ni muhimu. 
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa nchini humo mwezi ujao Benki Kuu ya Pakistan inatarajia kutengeneza sarafu ya rupia 50 yenye picha ya Edhi ikiwa ni ukumbusho tosha na kutambua kazi yake nchini humo.

0 Comments:

Post a Comment