Saturday, February 25, 2017

Facebook yakiri kusaidia mkutano wa Republican

MARYLAND, MAREKANI
Mark Zuckerberg wa Facebook
WAKATI washauri wa juu wa Rais Donald Trump wakisisitiza kuwa wataendelea kumshawishi kiongozi huyo wa Marekani kutekeleza ahadi zake alizoahidi wakati wa kampeni, imeelezwa Facebook ilichanga dola 62,500 za Marekani kufanikisha Kongamano la Siasa lenye mrengo wa Kihafidhina (CPAC).
Kongamano hilo linafanyika National Harbor, Maryland nchini humo likiwaleta pamoja wanasiasa wa chama cha Republican na wanaharakati takribani 10,000 akiwamo makamu wa serikali ya Trump Mike Spence.
Mapema kabla ya kongamano hilo la siku nne Msemaji wa Facebook alithibitisha kujihusisha kwao kwa kutoa semina za kiufundi na maeneo ya kustarehe.
Hata hivyo Facebook imeendelea kusema kuwa mchango wake huo hauna maana ya kuwa ni kampuni lenye mrengo wa kisiasa na kwamba litabaki kujihusisha na masuala ya jamii bila kujali itikadi za kisiasa.
Kuthibitisha hilo Facebook imesema inatarajia kuunga mkono makongamano mengine mawili ya kisiasa ya Netroot Nation na PDF ikiwa ni sehemu ya utafiti wao namna ambavyo siasa na teknolojia inaweza kufanya kazi pamoja.
Mapema mwezi huu Facebook ilikuwa ikisheherekea miaka 13 tangu kuanzishwa kwake huku mapato yake kwa mwaka jana yakiwa dola za Kimarekani Bilioni 27.6
Donald Trump akiwasili katika Kongamano la CPAC 2017

0 Comments:

Post a Comment