Monday, February 27, 2017

Waziri Mkuu Majaliwa kufanya uzinduzi Feb 28

NA MWANDISHI WETU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Kassim Majaliwa kesho atafungua mkutano wa siku moja wa Watendaji Wakuu na Wenyeviti wa Bodi za Mashirika ya Umma utakaojadili nafasi za Mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Mpango wa II wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Mkutano huu ambao umeandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina utafanyika Ikulu jijini Dar es Salaam ukiwakutanisha zaidi ya washiriki 100.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph Semboja amesema kwamba malengo ya mkutano ni kukusanya maoni ya viongozi kuhusu nafasi ya Mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano; kuzungumzia changamoto tarajiwa katika utekelezaji wa majukumu haya na; kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
Profesa Semboja amesema Mashirika ya Umma yana nafasi na uwezo mkubwa wa kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano, 2016/17–2020/21 wenye kaulimbiu ‘Maendeleo ya Viwanda kwa Mabadiliko ya Kiuchumi na Maendeleo ya Watu’,” .

Pamoja na mambo mengine, mkutano utajadili namna ya kuboresha mifumo ya  kiundetaji ndani ya mashirika na mahusiano miongoni mwa mashirika na taasisi za Serikali; kufungamanisha mipango ya mashirika ya Umma na Mpango wa Pili wa Maendeleo; kutathmini kiwango na aina ya rasilimali zinazohitajika kuwezesha utekelezaji wa mipango na; kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mipango.

0 Comments:

Post a Comment