|
Paul Makonda |
Hivi karibuni mkuu wa
Dar es Salaam Paul Makonda alikaririwa akisema kuhusu kuwakamata wabunge
waliokimbia vikao vya bunge ambao wengi wao ni wa upinzani lakini kuna maneno
mawili aliyasema vizuri bila kupepesa mdomo, maneno hayo ni uzururaji na
uchagudoa.
Pia RC Makonda aliwahi
kuendesha operesheni jijini hapo ya kuwaondoa ombaomba, kwa kauli kwamba
atakayepatikana akiwapa msaada ombaomba ambao husimama katika kando ya njia
atatozwa kiasi cha shilingi laki mbili.
Nafahamu hayo yote ni
makosa ya jinai kuyafanya katika mipaka ya nchi yetu kutokana na sheria zetu
zilivyo licha ya mkanganyiko wake lakini swali moja muhimu ni kwamba yanaweza
kuondoka kirahisi kama tunavyodhani, kabla sijasonga mbele niangazie hili.
Kosa la jinai ni tendo
lolote ambalo limekatazwa kwa sheria, ambapo mtu yeyote akilitenda anakuwa
ameikosea Jamhuri. Katika makosa ya jinai, mlalamikaji anakuwa ni Jamhuri,
ikiwakilishwa na mwendesha mashitaka wa Serikali.
Mtu binafsi
aliyedhurika kwa tendo la kijinai siye anayeshitaki mahakamani. Yeye anabakia
kuwa ni shahidi tu, na ni mara chache kwamba Mahakama inaweza kuagiza kulipwa
fdia kwa mtu aliyedhuriwa na tendo la kijinai.
Katika Makosa ya
Jinai, mtu anayepatikana na hatia huadhibiwa, na anayeonekana hana hatia
huachiwa huru. Adhabu za makosa ya Jinai ni pamoja na: kuachiwa kwa masharti,
kifungo cha nje, faini, kifungo gerezani kwa muda maalum, kifungo cha maisha na
kunyongwa hadi kufa.
Makosa yote ya Jinai
sharti yawe yameandikwa katika sheria mbalimbali. Hata hivyo, kwa nchi yetu ya
Tanzania, makosa mengi ya Jinai yametajwa katika Kanuni ya Adhabu (Sura ya 16
ya Sheria za Tanzania).
Hivyo Kifungu cha 176A
kinasema Mtu yeyote akiwa ni muuza kilabu ya pombe, hoteli, nyumba, duka,
chumba au mahali pengine panapofikiwa na watu mara kwa mara kwa ajili ya
kununua au kunywa viburudisho vya namna yoyote, anayeruhusu au kukubali kwa
makusudi makahaba wa kawaida kukusanyika na kubaki katika jengo lake kwa ajili
ya ukahaba, mtu huyo atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atawajibika.
Pia kifungu cha 177(a)
kinasema Yeyote miongoni mwa watu wafuatao- mtu aliyepatikana na makosa kwa
mujibu wa fungu la 176 baada ya kuwa alipata kuonekana na makosa zamani ya kuwa
mzembe na mzururaji; atahesabiwa kuwa ni muhuni na atawajibika kwa adhabu ya kifungo
cha miezi mitatu jela, na kwa kila kosa litakalofuata kifungo cha mwaka mmoja
jela.
Baada ya kuangazia
hapo, niseme mtu yeyote yule haidhuru awe mbali vipi na shughuli za kisayansi,
mapambano ya kisiasa, harakati za kimapinduzi na kadhalika, huwa anakuwa na
hamu ya kutaka kujua vile ulimwengu utakavyokuwa kwa wakati ujao. Mustakabali
wake ukoje? Maafa ya vita au furaha ya maisha ya amani.
Dunia na maumbile
yake, yakiwemo majani, miti, wanyama, ndege, pamoja na binadamu mwenyewe
atakuwaje? Atasalia milele au yote yenye uhai yataangamia kutokana na maendeleo
ya kisayansi na ufundi?
Je, unyonyaji na
ukandamizaji, unyonge pamoja na maovu mengine yaliyoiandamana jamii ya
binadamu, yatakomeshwa kabisa na milele au la maovu yote hayo yatadumu daima?
Malimwengu
yamzungukayo mwanadamu hayana kikomo wala mipaka yoyote ile na hatimaye hujaa
siri ambazo mwanadamu anaweza kuzigundua kwa taratibu tu, hatua kwa hatua
lakini hadi sasa binadamu huyu hajafaulu kamwe kuzijua zote kwa ukamilifu.
Mtaalamu wa Elimu ya
Jamii nchini Uingereza Herbert Spencer (1820-1903) alisema kuwa wanadamu wa
rangi nyeusi wamejaliwa kuwa akili na akili isiyoweza kujizamisha katika
uwazaji mtupu. Spencer aliongeza kusema akili yake Mwafrika ni akili
iliyojifungia katika mitokezo tu (yaani vinavyoonekana). Kitendo hicho humfanya
Mwafrika huyu kutegemea hisia zaidi kuliko mawazo. Hali ambayo itamfanya
ashindwe kupokea fikara za daraja la juu.
Sasa muono huo wa
Spencer ulienda sambamba na ule wa msomi wa Ujerumani Georg Wilhelm
Friedrich Hegel (1771-1831) ambaye alisema Afrika imezama katika dimbwi la giza
ambapo akili yake haijafikia kwenye kiwango cha fikara pembuzi (objective
thinking). Hivyo kwa mantiki hiyo Mwafrika hawezi kuibua muono wake wa daraja
la juu ambao utaweza kupita mfumo wa kufikiri kwa hisia.
Kwa maana nyepesi ni
kwamba mfumo wa Mwafrika akiwamo Mtanzania umejengeka katika imani na mapokeo,
hakuna hali ya ujikosoaji (self-criticism) na mawazo pinganifu. Watu huwaza na
kuyapokea mambo kama yanavyoelezwa katika mfumo wa mapokeo hali ambayo
huwafanya waishi katika ulimwengu wa mitholojia.
Kwa upande mmoja
mtazamo huo unaweza kuwa na afya katika kuondokana na watu wanaozurura,
machagudoa na ombaomba lakini sio kazi nyepesi kama inavyochukuliwa, binafsi ni
mwamini wa binadamu mmoja kubadilika na sio kama kundi.
Hapa kuna pande zote
mbili utawala na wananchi husika wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Je, nini kifanyike katika kufikia kudhibiti kabisa hali hii ambayo tumeitungia
sheria miaka na miaka lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu? Tumuangalie mtu
huyu.
Mwanafalsafa ya
Ugiriki Socrates katika suala juu ya maadili alisema elimu na maadili ni vitu
vinavyokwenda sawa. Kama maadili yanaendana na kuifanya roho kuwa nzuri kadri
iwezekanavyo ni lazima kujua kitu gani kinachoifanya roho iwe nzuri.
Socrates aliona kuwa
matendo yetu ambayo ni mabaya au mazuri ni matokeo ya elimu tuliyonayo, basi
matendo yetu ni lazima yatendwe kulingana na ama elimu yetu au maumbile.
Pamoja na ukweli huo
Socrates alikuwa tayari kukubali ukweli kuwa binadamu anatenda vitendo vya
dhambi. Alisema Mtu kama kiumbe mwenye akili; shughuli yake maalum ni kuongoza
maisha yake kulingana na maumbile yake yaani kiumbe mwenye kufikiri.
Hata hivyo Socrates
aliona kuwa kila binadamu ana tamaa isiyoepukika ya kupenda kuwa na furaha au
kuwepo kwa hali nzuri ya roho yake hivyo huchagua vitendo fulani kwa matumaini
kuwa vitamletea furaha.
Anahoji Socrates ni
tendo gani au tabia gani itampa furaha huyu mtu? Socrates alifahamu kuwa baadhi
ya tabia huonyesha kama zinatoa furaha lakini katika ukweli halisi hazitoi
furaha. Hivyo basi kwa namna hivyo mtu huyu hupenda kuwa na madaraka, anasa za
mwili na kumiliki vitu ambavyo huviona ni alama ya mafaniko na furaha huku
akishindwa kufahamu kuwa anachanganya hivi vitu na msingi halisi wa furaha.
Unaweza kumuona mtu
anayemsaidia ombaomba anadhani kwa maoni yake kuwa anamsaidia maskini na kwamba
atapata thawabu peponi siku moja. Utamsikia mtu akisema “…mimi bila kusaidia
ombaomba sioni kama nabarikiwa (yaani kuwa na furaha)…” huku akisimamia imani
na mapokeo.
Pia unaweza kuona mtu
amekuwa na maisha mazuri ana gari, nyumba, fedha lakini kila siku ni kulala na
wanawake wa kila namna kwa imani kwamba anapata furaha bila kufahamu kuwa
anachanganya mafaili.
Machangudoa wanasimama
katika vichochoro mbalimbali kwasababu kuna watu ambao uwezo wao wa kufikiri
umekaa katika hisia tu na ndio sababu kila siku tunatukanwa na wazungu kuwa
watu tusiojiweza kila siku tunawategemea wao.
Hivyo ukibadilika na
kutambua ukweli kuhusu furaha ya kweli ni utulivu wa roho hautakwenda kuwafuata
machagudoa hali ambayo itawafanya wapungue kumsubiri mtu kama wewe.
Kwa upande wa utawala
mwarobaini mwa changamoto hizi ni kama alivyosema mwanafalsafa wa Ugiriki
mwanafunzi wa Socrates, Plato katika kitabu chake cha Republic (Jamhuri) kwa
kutumia uhusiano uliopo kati ya meli na nahodha, alisema kama ilivyo katika
meli ambapo uwezo wa uongozi wa nahodha unategemea elimu yake ya majini, ni
hali hiyo hiyo inatawala kwa meli ya nchi, kwamba meli ya nchi lazima iongozwe
na nahodha ambaye ana elimu thabiti au elimu ya kutosha.
Plato aliamini kuwa
elimu ya viongozi ilipaswa ihusiane na nidhamu ya hali ya juu ya kiakili ambapo
mkazo ulikuwa kwenye masomo ya sayansi ya uendeshaji na uendeshaji vitu
kisayansi.
Elimu kwa kadri
ya Plato ilikuwa siyo jambo la kusoma vitabu mbalimbali na kupata shahada bali
ni ile hali inayomfanya mtu awe na uwezo wa kujua ukweli kama ulivyo na kuishi
kadiri ya misingi ya elimu hiyo na kwamba elimu lazima imfanye mtu abadilike
kutoka kwenye ulimwengu wa kivuli na kwenda kwenye ulimwengu wa mwanga.
Hata wewe mtanzania
uliye mzururaji, changudoa, ombaomba unaweza kubadilika kutoka hivyo ulivyo na
ukawa mtu mwingine mzuri ambaye jamii itakukubali. Tuachane na dhana ya kutumia
njia ngumu kutatua tatizo hili bali itumike njia ya kisayansi kwa kuwapelekea
elimu kwa njia mbalimbali watu hao hatimaye hawa wazungu wataacha kuicheka
Tanzania na Afrika kwa ujumla.