Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, John Pombe Magufuli tarehe 26 Mei, 2019 amekutana na kufanya
mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Ikulu Jijini
Pretoria.
Katika mazungumzo hayo, Rais
Magufuli amempongeza Mhe. Rais Ramaphosa kwa kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya
Tano wa Afrika Kusini na amemhakikishia kuwa Tanzania itadumisha uhusiano na
ushirikiano wa kidugu na kihistoria na nchi hiyo ulioasisiwa na Baba wa Taifa
Hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere na Hayati Nelson Mandela kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na Chama cha ANC (African National Congress).
Rais Magufuli amemshukuru, Mhe
Rais Ramaphosa kwa kumkaribisha kufanya nae mazungumzo siku moja baada ya
kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Afrika Kusini na amebainisha kuwa
anatarajia uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini utaimarishwa zaidi katika
masuala ya uchumi na kukuza lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake, Rais Ramaphosa
amemshukuru Rais Magufuli kwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwake, na
amemhakikishia kuwa Afrika Kusini inatambua mchango mkubwa wa Tanzania katika
ukombozi wa Taifa hilo na kwamba katika kipindi chake cha uongozi wake
atauendeleza na kuuza zaidi uhusiano huo.
Rais Ramaphosa amesema kufuatia
uamuzi wa Afrika Kusini kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili, nchi yake
itachukua walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania ili watumike kufundisha somo hilo
katika shule za msingi na sekondari.
Aidha, Rais Ramaphosa ameahidi
kufanya Ziara Rasmi ya Kitaifa nchini Tanzania kabla ya Mkutano wa Jumuiya ya
Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliopangwa kufanyika mwezi Agosti
2019 nchini Tanzania Na pia atahudhuria mkutano huo.
Kabla ya mazungumzo hayo Rais Magufuli
ambaye ameongozana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Prof. Palamagamba Kabudi amemkabidhi Rais Ramaphosa zawadi ya vitabu vya
kusoma na kufundishia lugha ya Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM).
SOURCE: Ikulu ya Tanzania
PHOTO BY: CCM Blog
0 Comments:
Post a Comment