Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Fredrick Onael Shoo amepokea vitabu zaidi ya
100 vya historia ya kanisa hilo Afrika Mashariki kutoka kwa familia ya Mshumbue
Marealle II OBE aliyetafsiri kutoka lugha ya kiingereza hadi Kiswahili.
Familia hiyo imetoa kitabu hicho chenye kurasa 207
kinachojulikana, “HISTORI YA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI AFRIKA MASHARIKI 1902-1912
(Kilimanjaro, Arusha, Meru na Pare).”
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kumkabidhi iliyofanyika
ofisini kwa Askofu Mkuu Dkt. Shoo jana, Themi Marealle ambaye ni miongoni mwa wanafamilia ya Marealle II alisema
wameamua kufanya hivyo ili waumini watakaokisoma waweze kujua historia yao.
“Baba Askofu tumefika
hapa leo kukabidhi kitabu chenye historia ya Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanganyika
maeneo ya Kilimanjaro, Arusha, Meru na Pare; kiliandikwa mara ya kwanza na
wachungaji wawili Wajerumani baada ya
hapo mheshimiwa Marealle alimwomba mwalimu wa International School Moshi akitafsiri
kutoka kijerumani hadi kiingereza naye akakitafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili
ili watu wa Kilimanjaro na Tanzania waweze kukisoma. Kwa hiyo kitabu hiki ni
historia ya KKKT hapa Kaskazini na Tunaomba kukukabidhi kitabu hiki ili
waumini na hata watu wengine watakaopata nafasi ya kukisoma wajue historia yako
Baba Askofu nakushukuru sana Mungu akubariki.” alisema Themi Marealle.
Kwa upande wake Askofu Mkuu Dkt. Shoo alisema;
“Shukrani kwanza kwa
familia kwa kupenda kutoa kitabu hiki ambacho ni kizuri sana kwa historia ya
kanisa letu kuanzia mwaka ule wa 1902 hadi 1912 huu ni mchango mkubwa sana
ambao Mangi Mkuu Thomas Marealle ametuachia, lakini familia kipekee ikaona isibaki
na vitabu bali wavitoe sadaka yao kwa kanisa Napenda kuwashukuru sana kwa sadaka. Ni imani
yangu kwamba vitabu hivi vitatumika kwa kuwapatia watu sio kizazi cha sasa tu lakini
hata vizazi kinachokuja ufahamu wa historia ya uwepo wa kanisa letu la Kiinjili
la Kilutheri hasa katika eneo hili la Kaskazini,” alisema Askofu Shoo.
Aggrey Marealle akisalimiana na Askofu Mkuu Dayosisi ya Kaskazini Dkt. Fredrick Onael Shoo, katikati ni Themi Marealle. |
Mangi Mkuu Thomas Marealle II OBE alitafsiri kitabu hicho
akiwa na msaidizi wake Rusk Shirima Kishimba; ambapo Kitabu hicho kiliandikwa
kwa mara ya kwanza kwa lugha ya Kidachi (Kijerumani). Baada ya hapo
kilitafsiriwa kutoka Udachi hadi kiingereza na Mhisani Anthony Pyane wa London.
STORY BY: Jabir Johnson
PHOTO BY: Arnold Mrema
0 Comments:
Post a Comment