Monday, May 13, 2019

Walimu watakiwa kujenga utamaduni wa kuwapatia wanafunzi maziwa badala ya kande

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai Yohana Sintoo akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Yohana Sintoo, amewataka walimu wajenge utamaduni wa kuwapatia wanafunzi maziwa shuleni badala ya kuwalisha chakula akitolea mfano wa kande na maharage.

Sintoo aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa tamasha la unywaji wa maziwa yaliyosindikwa mkoani Kilimanjaro, lililoandaliwa na Mradi wa maziwa kutoka shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) , na kufanyika katika viwanja vya  Mashujaa mjini Moshi Mkoani hapa.

Alisema mpango wa unywaji wa maziwa yaliyosindikwa kwa wanafunzi , unalenga  kuenzi uhusiano na uwiano sawa baina ya mwalimu na mwanafunzi  ili kuinua ufundishaji mzuri darasani  kwa kuwa unasaidia ufaulu wa mwanafunzi.

Alisema uhamasishaji wa unywaji wa maziwa shuleni haujafanyika vya kutosha hivyo kuna haja ya  walimu kuanza kuwajengea utamaduni wanafunzi wa kuwa wanawapatia maziwa shuleni , badala ya kuwalisha kande na maharage kama ambavyo wanafanya kwa sasa kwani maziwa ni lishe na nichakula pia.

“Upo umuhimu mkubwa sana kwa wanafunzi kunywa maziwa  shuleni na hata nyumbani , hivyo niwaombe wazazi na walezi waweze kutoa sehemu ya kipato chao ili watoto wao waweze kuwa wanakunywa kila siku maziwa yaliyosindikwa ,”alisema Sintoo.

Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa maziwa kutoka Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) Thomas Ole Seika, alisema shirika hilo limeamua kuwakutanisha wadau wa sekta ya maziwa kutoka wilaya ya Hai na Siha, ili kuwajengea uwezo katika uzalishaji na usindikaji wa maziwa.

“Shirika la Meandeleo la Uholanzi (SNV), ambalo ndio wawezeshaji wa tamasha hili limebaini kuwa hadi sasa zipo jitihada kubwa ambazo zimewezesha  kuongezeka kwa kiwango cha soko la maziwa katika wilaya ya Siha na Hai,”alisema.

Nae  Profesa Mstaafu wa kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro Prof Lusato Kurwijila alisema kituo cha kuzalisha mbegu bora za ng’ombe  wa kisasa wa maziwa (NIC), mwaka 2015/206 kilizalisha mbegu bora za ng’ombe dozi 80,000 ambapo hadi kufikia  mwaka 2017/2018 kiliongeza uzalishaji na kufikia dozi 140,000. 
Aidha alisema takwimu za uhamilishaji wa ng’ombe zinaonyesha kwamba umeongezeka kutoka dozi 200,000 katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi kufikia dozi 450,000 katika kipindi cha mwaka 2017/2018 ambazo ziliweza kutumika katika kuzalisha mifugo ya kisasa.
Vile vile Prof Kurwijila alisema kuwa Tanzania inahitaji mitamba zaidi ya elfu 80 kwa mwaka , lakini uzalishaji kwa mwaka  2015 ulikuwa ni mitamba  10,000 na mwaka 2018 umeongezeka na kufikia mitamba  13,000.

STORY& PHOTO BY: Kija Elias
EDITED BY: Johnson Jabir

0 Comments:

Post a Comment