Wednesday, May 29, 2019

Jela mwezi mmoja kwa kutelekeza familia



Mwanaume mmoja mjini Moshi mkoani Kilimanjaro amehukumiwa jela mwezi mmoja kwa kosa la kuitelekeza familia yake.

Mahakama ya Mwanzo mjini Moshi imemhukumu kifungo cha mwezi mmoja jela Mokolo Anselim Tengecha (37) kwa kosa la kuitelekeza familia yake.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo mjini Moshi Adnan Kingazi alisema mshtakiwa alikiuka kukiuka kifungu cha 166 cha makosa ya jina sura ya 16 ya kanuni ya adhabu.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa tarehe 10 Machi 2018  mshtakiwa akiwa katika maeneo ya Matindigani, Pasua bila halali na huku akijua kufanya hivyo ni kosa alimtelekeza mkewe anayefahamika kwa jina Zaina Mustapha Makame (22) akiwa na mtoto wake Omary Said (6) na Shaban Said (Mwaka mmoja na miezi tisa) bila kuwapa chochote na kutokomea kusikojulikana.

Aidha ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitafutwa kwa miezi kadhaa bila kuonekana na baada ikabainika kwamba alikuwa amepanga chumba kingine katika mtaa mwingine hapo hapo Matindigani na kuishi na mwanamke mwingine.

Ilidaiwa mahakamani hapo kutokana na kushindwa kulipa pango la nyumba mama mpangaji alimtimua mlalamikaji kwa kumtupia virago nje hali iliyomlazimu mlalamikaji kulala nje kwa mateso akiwa na watoto wake wawili.

Upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa mshtakiwa ni mtu anayejishughulisha na kupandisha watalii katika mlima Kilimanjaro.

Aidha ilielezwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka mahakama iliona ni mzito. Kwa upande wake mshtakiwa alipotakiwa kujitetea kwanini mahakama isimpe adhabu mshtakiwa alisema haoni haja ya kujitetea ndipo Mahakama ilimpomtupa jela mwezi mmoja ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hizo.

0 Comments:

Post a Comment