Tuesday, May 21, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Utabiri wa Harold Camping washindwa kutimia Mei 21, 2011


Mei 21, 2011 Mtangazaji wa Redio maarufu duniani Harold Camping alitabiri kuwa dunia ingefika kikomo tarehe hiyo sasa ni miaka minane imepita tangu tangazo lake hilo. Leo tutamwangazia Harold Camping alikuwa mtu wa namna gani. Na sababi gani zilimfanya afikie kutabiri kuwa dunia ingefika mwisho Mei 21, 2011.

Wanasayansi hutumia pesa nyingi na vifaa vya kisasa kutabiri mambo mbalimbali kama vile, madhara yatakayoletwa na uchafuzi wa mazingira au kutabiri hali ya hewa.

Wachanganuzi hutabiri kuhusu hali ya biashara na siasa. Warren Buffett, mmoja kati ya watu matajiri zaidi ulimwenguni, amesifiwa sana kwa uwezo wake wa kuchanganua na kufanikiwa kibiashara. Mchanganuzi mwingine Nate Silver, huchanganua takwimu ili kutabiri mambo mengi kutia ndani siasa za Marekani na hata tuzo za waigizaji wa filamu za Hollywood.

Maandishi ya kale yamefafanuliwa kuwa unabii. Watu fulani husema kwamba mambo yaliyoandikwa na Michel de Notredame (Nostradamus) katika karne ya 16 yanatimia sasa. Kalenda ya Wamaya iliyokwisha Desemba 21, 2012, ilifafanuliwa na wengi kuwa ishara ya kipindi cha msiba mkubwa duniani.

Wabashiri hudai kwamba wana uwezo wa kipekee wa kutabiri kuhusu wakati ujao. Edgar Cayce na Jeane Dixon walitabiri kwa usahihi matukio fulani ya karne ya 20. Hata hivyo, mambo mengi waliyotabiri hayakutimia. 

Kwa mfano, Dixon alitabiri kwamba Vita vya Tatu vya Ulimwengu vingetokea mwaka wa 1958, na Cayce alisema kwamba jiji la New York lingezama na kuingia baharini katika miaka ya 1970.

Viongozi wa kidini mara kwa mara hutabiri kuhusu matukio yenye kutisha ulimwenguni ili kuwaonya wanadamu na kujipatia wafuasi. Harold Camping na wafuasi wake walitangaza kwa bidii kwamba ulimwengu ungeangamizwa mwaka 2011. Lakini mpaka sasa bado mwisho haujafika.

Jina lake halisi ni Harold Egbert Camping. Alizaliwa Julai 19, 1921 na kufariki dunia Desemba 15, 2013 ikiwa ni miaka miwili baada ya utabiri wake kushindwa kutimia.  Huyu alikuwa ni Mkristo wa nchini Marekani, mwandishi wa vitabu na mwinjilisti wa Neno la Mungu. Akiwa na miaka 37 alianza kuitumikia Family Radio, hiyo ilikuwa mwaka 1958. 

Redio hiyo iliyopo California nchini Marekani alianza kuhudumu hapo kama Rais wake. Redio hiyo ilikuwa ikisikika katika maeneo ya masoko zaidi ya 150 nchini Marekani. Oktoba 2011 alistaafu kuwa kama rais wa redio hiyo kutokana na kupata STROKE. 

Licha ya kupata changamoto hiyo aliendelea kuhudumu katika redio hiyo hadi kifo chake mwaka 2013. Camping alijichotea umaarufu kutokana na msimamo wake kwenye kile alichokitabiri ‘Nyakati za Mwisho’.
Harold Camping
1921-2013
Katika kampeni yake alipata uungwaji mkono duniani ambapo alipata matrilioni ya shilingi ili kufanikisha kampeni yake ya nyakati za mwisho.  Alitabiri kuhusu siku ya hukumu ulimwenguni ambayo ingetokea Mei 21, 2011. 

Hata hivyo haikuwa mara yake ya kwanza kutoa utabiri huo kwani Septemba 6 mwaka 1994 Camping aliwahi kutabiri kuwa ingekuwa Siku ya Hukumu. Utabiri wake uliposhindwa alirudia tarehe yake kuwa INGEKUWA septemba 29 na pia Oktoba 2.  Mwaka 2005 Camping alitabiri UJIO WA PILI WA KRISTO  ungekuwa Mei 21, 2011. 

Siku hii alisema kuwa waliokoka wangetwaliwa juu mbinguni na baada ya hapo kungefuata miezi mitano ya moto, mateso na magonjwa kwa waliobaki duniani. Na kwamba watu mamilioni wangekufa kila siku na Oktoba 21, 2011 kila kitu ulimwenguni kingeteketea kabisa na hapo ndipo dunia ingekuwa mwisho wa kila kitu.

Tukio la Mei 21, 2011 liliripotiwa dunia nzima kwa usimamizi wa karibu na Family Radio. Hapo ndipo kulipowaibuwa watu wengine wasioamini katika Mungu mmoja. 

Hata hivyo wauminiwa makanisa ya Kiprotestant na Katoliki hawakuamini unabii wake na Mei 22, 2011 ibada ya Jumapili ilifanyika kama kawaida. Camping alisimamia maandiko kutoka katika Biblia kitabu cha 1 Wathesalonike 4:17 kuwa, “ Baadaye, sisi tulio hai ambao tumebaki tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili tukutane na Bwana hewani.” 

Siku ikafika bila kuona kitu chochote Camping akajitetea kuwa tukio hilo limefanyika kiroho zaidi  na kwamba mwisho wake ni Oktoba 21, 2011. Itakumbukwa kwamba Mei 23, 2011 alikataa mahojiano na vyombo vya habari na baada ya hapo alipata STROKE Juni 2011. 

Baada ya Oktoba 21, 2011 kupita bila unabii wake kutimia mitandao ya kijamii ilimtaja kama “Nabii wa Uongo” na kwamba huduma yake itaanguka baada ya utabiri huo kupita. Siku tano kabla ya Oktoba 21, 2011 Family Radio iliripoti kuwa Camping amestaafu kuhudumu katika nafasi ya Urais wa kituo hicho cha redio. 

Katika mahojiano ya siri ilielezwa kuwa aliachia nafasi hiyo kutokana na ukweli kwamba hawezi kuaminiwa na mtu yeyote baada ya unabii huo kushindwa kufikiwa.

Hata hivyo Machi 2012 alikaririwa akisema kitendo alichokifanya cha kutabiri tarehe husika kilikuwa ‘dhambi’ kama ambavyo kitabu cha Mathayo 24:36 kinavyosema; “Hakuna ajuaye siku wala saa, hata malaika mbinguni wala Mwana, isipokuwa Baba peke yake.” 

Kushindwa kwa Camping kuliifanya na Family Radio kupoteza usikivu masikioni mwa wengi, upotevu wa mali nyingi pia wafanyakazi wengi waliondoka na mapato walipoteza, Huyo ndiye Harold Camping mzaliwa wa Boulder katika Jimbo la Colorado, kwa baba kutoka Uholanzi. 

Wazazi wake walikutana nchini Marekani na kuoana ndipo walipomzaa Harold Camping, Baba ni wa kutoka mji wa Groningen na mama yake alitokea mji wa Frisia nchini Uholanzi. Camping akiwa na umri mdogo walihamia California, mwaka 1942 alifanikiwa kupata Shahada ya Uhandisi kutoka Chuo kikuu cha California, Berkeley. 

Mwaka 1943 alioa. Yeye na familia yake walikuwa waumini wa Kanisa la Christian Reformed Church hadi mwaka 1988. Harold Camping alifariki dunia akiwa na miaka 92.

PREPARED BY: Jabir Johnson

0 Comments:

Post a Comment