Thursday, May 30, 2019

MAKTABA YA JAIZMELA: Jonas Savimbi 1934-2002



Jonas Malheiro Savimbi ni moja ya wanasiasa na Wapigania Uhuru katika moja ya mataifa yaliyopo kusini mwa Afrika yaani Angola. Aliuawa kinyama Februari 2002 kwa kumiminiwa Risasi na vikosi vya jeshi la Angola. 

Sasa ni miaka 17 mzozo umeibuka baina ya serikali ya Angola na upinzani juu ya mipango ya kuzika upya mwili wa aliyekuwa kiongozi wa vugugu la waasi wa Unita ambaye kifo chake kilitokea miaka 17 iliyopita na kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa takribani miongo mitatu.

Serikali ilikuwa inataka kuukabidhi mwili wa Savimbi kwa wawakilishi wa Unita, ambacho sasa ni chama cha upinzani, ili waweze kuuzika mwili wake nyumbani kwao Juni Mosi mwaka huu.  Hata hivyo, makabidhiano ya mwili hayakufanyika na kila upande sasa unamlaumu mwingine. Helena Savimbi, mmoja wa watoto wa kike wa kiongozi huyo wa waasi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali haikuheshimu mkataba. 

Serikali nayo imeishutumu Unita kwa kushindwa kuuchukua mwili Jumanne, kama walivyokubaliana. Kikiwa ndio chama kikuu cha upinzani , Unita kimekuwa kikifanya kampeni ya kutaka mwili wa Savimbi uzikwe kwa heshima. Mwili wake uliofukuliwa ulitakiwa kukabidhiwa na serikali kwa Unita siku ya Jumanne. Jonas Savimbi ni nani katika ardhi ya Taifa la Angola na nje? Fuatana nami katika makala haya.

Jonas Savimbi alizaliwa Agosti 3,1934 katika eneo linalojulikana kama Munhango Jimboni Bie Angola wakati wakoloni wa Kireno wakilitawala Taifa hilo. Kwa miaka zaidi ya 30 Savimbi alipigana msituni hii inamfanya kuonekana mpiganaji hodari wa vita vya msituni. Aliuawa kinyama karibu na Lucusse katika jimbo la Moxico nchini Angola. Jonas Savimbi alikuwa ni mwanasiasa na kiongozi wa muda mrefu Wa Kikosi cha Askari wapigania Uhuru Wa Msituni. Angola ni moja ya mataifa yaliyojinyakulia uhuru kwa mtutu wa bunduki ikisaidiwa na mataifa yaliyokuwa mstari wa mbele (Frontline States) kama Tanzania , Zimbabwe n.k .

Jonas Savimbi alipigania Uhuru kutoka kwa Wakoloni wa Kireno na baada ya Uhuru Wa Angola mwaka 1975 yeye aliendelea kupigana na Serikali ya Angola kwani katika fikra zake aliamini bado watu wa Angola hawajapata Uhuru kamili.

Kihistoria yeye ni mtoto Wa Mfanyakazi wa Reli ya Benguela ,Alikuwa ni Mkuu wa kituo cha Reli. Kitaaluma alisoma katika shule za kidini za misheni ambazo kwa wakati huo zilikuwa ngumu sana Kuwapokea watu weusi kutokana na moja ya ndugu yake Savimbi kuwa moja ya machifu Wa kabila la Ovimbundu basi ikawa rahisi kufanya Urafiki na wamishionari Wa Roman katoliki na kufanikiwa kuhitimu masomo yake ya awali na baadaye alipata ufadhili wa kimasomo na kwenda ng'ambo (Ulaya). Savimbi alisoma taaluma ya Madawa(Udaktari) katika chuo kikuu cha Lisbon nchini Ureno mnamo mwaka 1958-1960, Chuo Kikuu cha Fribourg mwaka 1961- 1964 na baadaye alijiunga na chuo kikuu cha Lausanne nchini Uswisi huku akibobea katika Sayansi ya Siasa mnamo mwaka 1964-1965. 

Huku akiwa masomoni huko Lisbon miaka ya 1950 alianza kuupinga utawala katili wa Kireno nchini Angola. Mnamo mwaka 1961 Savimbi alipata kiu kubwa sana na kuamua kufanya harakati za kulikomboa Taifa la Angola kutoka katika makucha ya wakoloni Wa Kireno hivyo akajiunga na moja ya kundi la wapigania Uhuru lijulikanalo kama Popular Union of Angola (UPA). Baadaye National Liberation Front Of Angola (FNLA) lililokuwa chini ya Uongozi wa Holden Roberto. Alijiunga kama mpiganaji wa kawaida asiye na ujuzi mkubwa katika mapambano ya Msituni. 

Mnamo mwaka 1965 alipata nafasi ya kwenda nchini China na kupata mafunzo makubwa ya kijeshi akibobea Katika mapambano ya vita vya msituni (Guerrilla war) .Mwaka huo alikutana na kiongozi wa Taifa la Uchina Mao Tse Tung ,Viongozi wa Kijeshi na wanasiasa wa chama cha Kikomunisti ambao wote kwa pamoja walimpa mbinu mbalimbali za kukabiliana ktk vita vya Msituni. Savimbi aliwahi kaririwa na Gazeti la Reader's Digest akisema " Kutoka kwa Mao na Wakomunisti nilijifunza namna ya kupigana na kushinda Vita vya Msituni. 

Lakini vilevile nilijifunza kuendesha Uchumi au Taifa ,Utajiri Wa Taifa hutengenezwa na hatua zinazochukuliwa na watu Binafsi ". Baada ya mafunzo ya kijeshi huko China Savimbi alirejea nyumbani na kuendeleza harakati zake za ukombozi wa Taifa la Angola . Aliporudi alianza taratibu kuwahamasisha watu Wa jamii ya Ovimbundu ambao ni robo tatu ya nchi hiyo kuanza kujitambua na kupigania Uhuru wao kutoka kwa Mkoloni wa kireno. 

Mnamo Machi 13, 1966 Baada ya kuona kundi la FNLA ni dhaifu sana halifikii malengo yake aliamua kujiengua au kujitoa na kuunda kundi la wapigania uhuru lijulikanalo kama National Union for the Total Independence of Angola (UNITA) na kuanza kuendeleza ndoto yake ya kuung'oa utawala Wa Kireno .Udhaifu Wa FNLA ulitokana na mapigano yake dhidi ya watawala Wa Kireno kuanzia nchini Zaire kwa sasa DRC. Kutokana na sababu FNLA walikuwa dhaifu sana na kiu yake Savimbi ilikuwa ni kuanzisha mapambano kutokea ktk Ardhi ya Angola Siyo Zaire (DRC).Savimbi alishirikiana na Antonio da Costa Fernandez kuliunda kundi la UNITA ktk Eneo lijulikanalo kama Muangai kwenye jimbo la Moxico. 

Mnamo Disemba 25,1966 pambano la Kwanza La UNITA lilifanywa dhidi ya Wakoloni Wa Kireno.  Savimbi ndiye kiongozi wa wapiganaji Wa Msituni aliyesalia nchini Angola huku akipigana na Wareno kwani alikuwa amejiamini vilivyo dhidi ya utawala katili na dhalimu Wa Wareno .Mnamo Novemba 10,1975 Taifa la Angola lilipata Uhuru wake kutoka kwa Wareno. Hatimaye Harakati za kutaka kuunda Serikali huru ya Angola zikaanza na chama cha MPLA kikiwa ni miongoni mwa vyama vilivyokuwa vikipigania Uhuru dhidi ya Wareno kiliunda Serikali mpya.

Savimbi kama miongoni mwa wapiganiaji Wa Uhuru Wa Angola hakuridhishwa na ugawanaji Wa madaraka na hatimaye kuapa kupambana kwa njia ya vita vya Msituni mpaka atakapotwaa madaraka na kuiangusha MPLA .Kilichomuudhi sana Savimbi kitendo cha Wareno kukipa mamlaka chama cha MPLA kuunda Serikali mpya ambayo itakuwa inafuata misingi zaidi ya kijamaa huku washirika wake wakubwa hasa Marekani wakiwa ni waumini Wa Sera za kibepari.


Savimbi alipenda uchumi Wa Soko huria ambao kila mtu anakuwa huru kumiliki Ardhi ,Biashara na Viwanda. Savimbi aliingia Msituni na kusababisha Serikali ya Chama Tawala -MPLA kuomba msaada wa kijeshi kutoka nchini Cuba na Urusi ambapo haikuchukua muda sana vikosi vya majeshi ya Cuba na Urusi vilianza kujipenyeza nchini Angola kwa njia mbalimbali ikiwemo njia ya maji ,Ardhini na Angani .Majeshi ya Cuba na Urusi yakiwa na hamasa kubwa sana ya kutaka kuulinda ukoministi nchini Angola yalitumia nguvu kubwa sana kupambana na Vikosi vya kijeshi vya Savimbi vilivyokuwa vikipokea mafunzo ya Hali ya juu kutoka kwa jeshi la Marekani. Savimbi akiwa Msituni alinusurika Mara kadhaa kuuawa lakini vikosi vya Marekani vilivyoingia kwa siri nchini Angola vilimuokoa kutokana uhodari wa vikosi hivyo. 

Hadi mwaka 1975 Jonas Savimbi alikuwa ameongeza wafuasi wengi wa msituni huku akiwa na dhamira ya dhati ya kuchukua udhibiti kamili Wa nchi hiyo .UNITA kwa sehemu kubwa ilijikita katika maeneo makubwa ya Kusini -Mashariki ya nchi hiyo na Asilimia kubwa Savimbi alipata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa watu Wa Jamii ya Ovimbundu na ndio Wengi sana nchini Angola. Kikosi kikubwa cha wapiganaji wa Savimbi kilitokana na watu jamii ya Ovimbundu. 


Je, Jonas Savimbi alipata wapi msaada kiwango cha kutikisa Serikali ya Kikoloni ya Ureno na Hatimaye Serikali ya MPLA baada ya Uhuru? Kiufupi Mwanasiasa na mpiganaji huyu Wa Msituni alipokea msaada Wa Silaha, Mavazi ya kijeshi, Chakula, Madawa kutoka kwa nchi ya China, Afrika kusini na Marekani wakati Serikali ya Angola chini ya chama Tawala -MPLA ikisaidiwa na uliokuwa muungano Wa Urusi (USSR). Marekani ilikuwa ikihamasisha Serikali za Zambia, Israel, Bulgaria, Saudi Arabia, Zaire (DRC), Morocco, Ufaransa ili kuwasaidia wapiganaji Wa UNITA. Savimbi alipokea msaada mkubwa kutoka kwa marais kadhaa Wa Marekani akiwemo Ronald Reagan kuna wakati Gazeti la Marekani la Washington Post lilimnukuu akisema "Savimbi ni mpigania Uhuru ambaye anapambana kuvitoa Vikosi vya Kijeshi vya Serikali ya Cuba na Muungano Wa Urusi kutoka nchini Angola". Katika utawala wa Rais Reagan inadaiwa Savimbi alikuwa akipokea msaada wa kifedha hadi Dola millioni 15 ($15million ) na Silaha za kupambana na Ndege vita na makombora ya Urusi. 


Savimbi alipata marafiki wengi sana nchini Marekani na wengi walimwamini na kumpa msaada ili kuuondoa utawala wa Kireno na baadaye utawala wa chama Tawala MPLA chini ya Rais José Eduardo dos Santos. Utawala wa Santos kwa wamarekani waliona kama ni wakidikteta .Katika Harakati zake bwana Savimbi alishutumiwa vikali na mashirika ya haki za Binadamu Barani Afrika na Duniani hasa Kutokana na mbinu zake za kukabiliana na vikosi vya Serikali ya Angola vikisaidiwa na Cuba na Urusi.


Mkurugenzi mmoja Wa Shirika la haki za Binadamu ajulikanaye kama Rakiya Omaar hapa Afrika alivishutumu vikali vikosi vya Bwana Savimbi .Omaar alinukuliwa akisema " Shirika la Haki za Binadamu hapa Afrika limebaini kuwa Lengo la UNITA ni kutisha watu ili waiunge mkono au kuwaadhibu kwa sababu wanaunga mkono majeshi ya Serikali " .Mashariki mwa Angola ,Mbinu nyingi za UNITA zililenga kuwafanya Raia wateseke na njaa kwa kuchoma mazao ktk mashamba mengi huku ikizuia misaada ya kibidamu kutoka umoja Wa mataifa na Afrika.

Mnamo miaka ya 1970 na 1980 Savimbi aliendelea na mapambano makali ya vita dhidi ya Serikali ya Chama Tawala -MPLA .Haikuwa rahisi kumpiga Savimbi .Mawazo yake ya kuitawala Angola yalikuwa sana kwa kasi ndani na nje ya mipaka ya Taifa hilo Tajiri kwa mafuta ,Dhahabu na madini ya chuma .Mawazo ya Savimbi yalikuwa ni Kutengeneza Uchumi Wa Soko Huria ,Uchaguzi Wa vipindi na mabadiliko makubwa ya katiba ya Angola. 


Savimbi alimchukulia Rais José Eduardo dos Santos kuwa ni dikteta kwani kwa muda mrefu Angola baada ya Uhuru haikuwa na Uchaguzi Wa vyama vingi. Mwaka 1991 vikosi vya Jonas Savimbi vilingia mji Mkuu Luanda na kuudhibiti vikali ambapo umeme na miundo mbinu yake viliharibiwa vibaya sana, Barabara yakiwemo madaraja yalivunjwa ,Reli iliharibiwa vibaya na hatimaye gharama takribani dola billioni 20 zilitumika kurejesha miundo mbinu hiyo muhimu. Taifa liliingia katika deni kubwa pasipokutarajia na hivyo hatua kadhaa za kuleta amani zilianza kuchukuliwa kwa maslahi ya watu wote wa Angola. 

Baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya muongo mmoja Mei 30,1991 Savimbi alikubali na kusaini mkataba na chama Tawala -MPLA hatimaye Amani ilirejea na kisha uchaguzi wa mfumo Wa vyama Vingi uliitishwa mwaka 1992 ambapo chama cha UNITA kupitia Savimbi kilianza kufanya kampeni za Uchaguzi .Savimbi aligombea Kama Rais kupitia chama cha UNITA .Savimbi ktk kampeni za Urais aliahidi Kuhakikisha uchaguzi kufanyika kwa vipindi tofauti na awali ambapo hakukuwa na uchaguzi wa kdemokrasia ,watu kumiliki Ardhi ,Watu kumiliki Biashara na Uwepo wa Soko Huria nchini Angola. 

Katika uchaguzi mkuu huo Savimbi alinukuliwa mbele ya Umati mkubwa wa watu Jijini Luanda akisema "Nguvu ya UNITA haipimwi kwa Majeshi yake bali ni kwa Uwepo wake Kisiasa " Ktk Uchaguzi huu Chama cha MPLA kikiongozwa na Rais José Eduardo dos Santos killibuka kidedea maeneo mengi ya nchi hiyo . Baada ya Uchaguzi huu bwana Savimbi hakuridhika na matokeo akidai uchaguzi uligubikwa na udanganyifu ndipo UNITA ilirudi Msituni ili kutaka kuitawala nchi hiyo ambapo vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka upya tena na kusababisha kwa kiwango kikubwa maeneo ya vijijini kudhibitiwa na kuwa chini ya Wapiganaji Wa Bwana Savimbi .Maefu ya watu walikufa na kujeruhiwa vibaya ,Visa vya ubakaji vilishamiri ,Njaa kubwa ilitokea ,Miundo mbinu kama Reli, Barabara, Madaraja yalivunjwa ,Viwanda viliripuliwa n.k .Vilikuwa ni vita vibaya sana kuwahi kutokea kusini mwa Afrika. 

Baada ya mapigano makali na yasiyoisha mnamo mwaka 1994 mazungumzo ya Amani yalifanyika mjini Lusaka -Zambia ambapo mahasimu walikutana na kukubaliana kushusha chini Silaha na kuviamrisha vikosi vyao vya wapiganaji kuondoka kwenye baadhi ya maeneo ili kurahisisha mapatano. Katika makubaliano ya pande mbili Aliyekuwa Rais Wa Angola ndugu José Eduardo dos Santos alikubali kutoa nafasi mbili za umakamu wa Rais kwa UNITA hatimaye Serikali ya pande mbili ikaundwa. Mwaka 1997 Savimbi alijiuzulu nafasi hiyo na Hatimaye Serikali ya Angola ilimrejesha ktk nafasi hiyo mwaka 1998. Mwaka 1996 ilidaiwa kwamba Jonas Savimbi Alikuwa na harakati za kuchukua udhibiti Wa Eneo la kaskazini-Mashariki ambalo lilikuwa linautajiri mkubwa Wa madini ya Dhahabu ,Wapiganaji wake walidhibitiwa na kupewa kazi jeshini hatimaye mpasuko mkubwa ukaanza kujitokeza ndani ya UNITA. 

Marekani ilikuwa ikibeba utajiri mkubwa wa Dhahabu ktk Eneo hili ndio maana ilikuwa ikitoa Msaada mkubwa Wa kijeshi ili kulinda masirahi yake .Baada ya vikosi vya Serikali kulidhibiti Eneo hili Marekani ilipunguza msaada Wa Silaha na hatimaye nguvu ya Savimbi ilipungua kwa kiwango kikubwa ingawaje aliendelea kuwa imara dhidi ya Serikali ya José Eduardo dos Santos . Septemba mwaka 1998 Savimbi alikutana na upinzani mkali sana ndani ya UNITA hatimaye kundi jingine lililojiita UNITA-R lilijitokeza na kujitangazia uongozi wake. 

Tangu hapo ndipo ukawa mwanzo wa kutokea makundi matatu ndani ya UNITA. Kutokana na mgawanyiko huo Serikali ya Angola na Jumuiya ya Maendeleo kusini Mwa Afrika (SADC) walilitambua kundi la UNITA-R kama kundi rasmi linaloiwakilisha UNITA. Kwenye miaka ya 2000 Marekani ulikuwa imethibitisha kwa asilimia kubwa misaada yake ya kijeshi kwa Jonas Malheiro Savimbi kwani hakuna faida yoyote ambayo wamarekani walikuwa wanaipata kutoka kwake ikiwa migodi iliyokuwa inadhibitiwa na wapiganaji Wa Savimbi ilikuwa imetwaliwa na jeshi la Angola. UNITA ilipoteza Rasilimali kubwa kutoka nje hasa baada ya Kutwaliwa migodi ile ilyokuwa ikiwaingizia fedha za magendo uliowasaidia kupata Silaha nyingi na za kisasa kwa ajili ya kuendesha mapambano dhidi ya Serikali.  

Mwaka 2001 Jonas Savimbi hatimaye kwa hiari yake alikubali mkataba Wa Amani wa Lusaka -Zambia uliosainiwa na pande mbili ili kuleta Amani .Wakati Serikali ikitaka usimamishaji wa vita na UNITA, Savimbi alilitaka kanisa la Roman katoliki ndilo liwe msuluhishaji Wa Mgogoro ule lakini mapigano makali yaliendelea mwaka mzima hatimaye kuvuka mipaka na kuingia nchini Zambia na Namibia. Majeshi ya Serikali ya Angola yaliendelea kumfuatilia Savimbi na vikosi vyake mpaka walipofanikiwa kumkamata Mashariki mwa jimbo la Moxico na Hatimaye kumminia Risasi nyingi sana mwilini mwake na hatimaye kupoteza maisha yake mnamo Februari 22, 2002. Baada ya Jonas Savimbi kuuawa makubaliano ya Amani yalisainiwa kati ya UNITA na Serikali ya Angola hapo Mwezi Aprili 2002.

0 Comments:

Post a Comment