Saturday, May 25, 2019

Mifumo ya urutubishaji shirikishi wa ardhi inayofanywa na TaCRI



Udongo ni maliasili  ya kipekee ambayo ndio chanzo cha maisha ya viumbe na mimea yote iliyopo ulimwenguni,  udongo una manufaa mengi katika maisha  ya binadamu, wanyama na viumbe wengine.

Kwa binadamu  udongo ndio chanzo cha  chakula cha  binadamu kupitia shughuli za kilimo zinazofanyika  kupitia udongo , faida yake kwa binadamu  ni chanzo cha  makazi.
Lakini pia kwenye udongo  madini yote yanapatikanahuko, hivyo asilimia kubwa ya shughuli zinategemea udongo, vyanzo vyote vya maji viko juu  udongo, kama vile ziwa, bahari na mito basi  maisha ya binadamu  yanategemea udongo. 
Udongo ni nini? ‘Udongo’ ni tabaka juu ya ardhi ambalo hufanya kazi kama chombo cha kukuzia mimea, udongo hujengwa kutokana na shughuli zinazoendelea za hali ya hewa kulingana na vipengele kadhaa vya mazingira.
Udongo umetengenezwa na nini na unafanya nini? Vitu vya msingi vinavyotengeneza udongo ni madini, mabaki ya viumbe hai, maji na hewa, udongo unaofaa kwa ajili ya kukuza mimea mingi huundwa kwa asilimia takribani 45 ya madini, maji 25 %, hewa 25 %, na mabaki ya viumbe hai 5 %.
Makala yetu kwa leo  inaangazia Mifumo ya urutubishaji  shirikishi wa ardhi inayofanywa na taasisi ya Utafiti wa kahawa Tanzania (TaCRI).
Mtafiti Mkuu  wa idara inayohusika na kuongeza tija na ubora wa zao la Kahawa (TaCRI) Suzan Mbwambo, anasema, idara ya udongo imegawanyika katika sehemu kuu tatu, ambayo ni mifumo ya urutubishaji shirikishi wa ardhi (ISFM), mifumo mbalimbali ya makuzi ya kahawa na udhibiti husishi wa visumbufu vya kahawa (IPM).

Anasema maabara ya udongo  iliyopo TaCRI, imekuwa ni nyenzo kubwa katika kuhakikisha kuwa lishe ya Kahawa inaboreshwa na hivyo kutimiza lengo la kuongeza tija ya kahawa kwa mti.

“TaCRI ilianza kwa kuboresha maabara yake kwa kununua  vifaa  ambavyo ni bora na vya kisasa kabisa, hivyo  maabara inauwezo wa kutoa huduma bora na yenye kuaminika ya uchanganuzi wa uongo, majani na maji kwa wateja  mbalimbali ndani na nje ya tasnia ndogo ya kahawa, lakini kutoa ushauri wa kitaalamu wa matumizi ya mbolea kulingana na hali halisi ya udongo katika shamba husika,”anasema Mbwambo.

Mbwambo anafafanua kuwa “Tumefanikiwa pia kufanya tathmini ya rutuba ya udongo katika maeneo karibu yote yanayolima kahawa hapa nchini hii ikijumuisha mikoa takribani  16 katika kanda tano zinazolima kahawa hapa nchini ambapo tayari ripoti zimeshawasilishwa katika wilaya husika, tathmini hii ya udongo imetuwezesha kubaini maeneo mbalimbali yenye upungufu wa uchachu yaani (LOW PH),”anasema.

Anafafanua kuwa katika maeneo hayo hata mkulima akitumia mbolea hawezi kupata mavuno tarajiwa hivyo mkulima atakuwa anatumia gharama kubwa kununua mbolea na huduma zingine katika shamba lake  bila mafanikio yeyote.

Anasema idara hiyo imeanzisha mradi wa majaribio katika maeneo ya wilaya ya Hai, Rombo, Moshi, Mwanga, Same na Meru kwa upande wa Kahawa aina ya Arabika na upande wa Robusta  ili kuja na mkazo wa jinsi gani ya kurekebisha uchachu katika maeneo husika na wanatarajia kuanza kufungasha matokeo hayo kuanzia mwaka ujao.

Mifumo mbalimbali ya makuzi ya kahawa 

Mbwambo anasema, Lengo la idara hii ni kuhakikisha kuwa  mkulima anaongeza tija kwa mti lakini pia kwa eneo na hivyo basi lishe ni kitu muhimu sana katika kufikia haya lakini pia idadi ya miti inayopandwa kwa eneo ni muhimu sana.

Anasema  idara hiyo imeshafanya tafiti katika eneo hilo na kubaini kuwa idadi ya miti kwa eneo ina tofautiana endapo kama kahawa ni aina fupi ambayo huhitaji nafasi ndogo, TaCRI imekuwa ikiwashauri wakulima kuzingatia idadi ya miti katika mashamba yao ili kuweza kupata faida katika kilimo wanachofanya.

“Yapo majaribio mengi katika eneo hili ambayo kwa sasa yanayendelea kutunzwa na tunatarajia kuanza kufungasha matokeo ya awali mwaka huu, tumeweza pia kufungasha teknolojia ya kilimo mseto na migomba , ambapo mkulima anatakiwa kupanda mistari kitatu ya kahawa  yake ndani ya mistari miwili ya migomba,”anasema Mbwambo.

Anafafanua  teknolojia hiyo imepokelewa vizuri sana na wakulima wengi wa kahawa kwani maeneo yanayolimwa kahawa na migomba pia hustawi vyema, kilimo mseto cha kahawa na migomba ambacho kinampangilio ambao TaCRI imeufanyia tathmini unafaida sana kwa mkulima.

Anaongeza kusema kuwa “Kwanza mkulima anauhakika wa kupata chakula kutoka katika migomba  lakini kipato pia, mkulima anauhakika wa kupata kipato kutoka katika kahawa, msimu ambao sio wa kahawa mkulima atakuwa anaendelea kupata kipato kutokana na ndizi,”anasema.

Mtafiti huyo anasema, kutokana na  mabadiliko ya tabia nchi kumekuwa na joto sana lakini mvua pia zimekuwa haba, hivyo mkulima ambaye analima kilimo mseto anaweza kuwa na kilimo endelevu licha ya mabadiliko ya hali ya hewa, hii ni kwa sababu migomba inatoa kivuli na hivyo basi jua litakuwa halifiki moja kwa moja katika kahawa na hivyo basi kile kiwango cha maji kupotea kinapungua kwa kiasi kikubwa.

Anasema ili mti wa kahawa uweze kuwa na tija ya kutosha msimu hadi msimu na  kuendelea kutunzwa vizuri katika maeneo mbalimbali , matokeo ya awali yanaonyesha tija kubwa imepatikana katika mibuni yenye mashina mengi ukilinganisha na ile ya shina moja.

Anasema  TaCRI inaendelea na utafiti wa kubaini faida mbalimbali zitokanazo na miche ya kahawa itokanayo na mbegu za upachikizaji,  vikonyo na njia ya chupa, matokeo ya awali yanaonyesha kuwa mibuni yote inauwezo sawa katika kutoa mavuno na matokeo hayo yanaonyesha kuwa wadau wa kahawa wanazo njia zaidi ya moja ya kuongeza miche ya kahawa ili kuhakikisha kuwa tunakidhi haja ya miche ya kahawa kwa wakulima wa kahawa.

Hivyo mtafiti huyo kutoka taasisi ya utafiti wa kahawa nchini TaCRI  Suzan Mbwambo,   anawashauri  wakulima kupima afya ya udongo wa mashamba yao kabla ya  msimu wa kilimo kuanza ili  kubaini mapungufu yaliyopo katika udongo na  kupata ushauri wa aina gani ya mazo na mbolea zinazoo paswa kutumika ili kuongeza uzalishaji na tija.

“Ni muhimu  sana wakulima wa zao kahawa  kufanya zoezi la kupima udongo kabla ya kutumia mbolea kwani  itampa majibu ya kiasi  gani  cha mbolea kitumike shambani kwake,”anasema Mbwambo.

Anaongeza kusema kuwa “Wakulima wengi  hawana tabia ya kupima udongo wa mashamba yao ili kujua  tatizo lililopo kabla ya kutumia mbolea na wengi wamekuwa wakitumia  mbolea kwa mazoea  bila kujua tatizo la udongo,”anasema.

Mkuu wa idara ya uboreshaji wa zao la Kahawa kutoka Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa nchini TaCRI Dkt Damian Mtenga anasema TaCRI imeweza kutafiti aina  19 za kahawa aina ya Arabika chotara zenye ukinzani kwa chulebuni (CBD) na kutu ya majini  CLR.

Anasema TaCRI ina aina nne bora za Robusta zenye ukinzani kwa mnyauko fuzari (CWD), ambazo zinauvumilivu wa magonjwa wa nyauko fuzari, “Aina hizi kwa kweli zimetafitiwa na zimezalishwa zikizingatia sana  ubora na zile sifa zinazoifanya kahawa iweze kunyweka,”

Dkt Mtenga anasema kahawa iliyofanyiwa utafiti na TaCRI ina sifa za kuzaa sana na muonjo wake ni mzuri na zina uvumilivu wa magonjwa, na kwamba kahawa ya  Tanzania zaidi ya  asilimia 90 inauzwa nje huku matumizi ya ndani yakiwa ni chini ya asilimia 10.

Dkt Mtenga anasema  wakulima wamewezeshwa kuzalisha mbegu mpaya za kahawa chotara ambapo  zinashabikiwa sana , licha ya kwamba TaCRI haijaweza kuwafikia wakulima wote.
“Kwa upande wa idara yetu kwa sasa katika mkakati wetu wa kuendeleza tafiti tumekuwa pia tukiangalia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi kwa kiwango kikubwa,”anasema.

Dkt Mtenga anasema kwa sasa TaCRI ipo kwenye mkakati wa kutoa aina  nyingine za kahawa  za matazamio ya aina  tatu hadi nne ambazo zina uvumilivu wa ukame.

“Yapo maeneo ambayo tulikuwa tunalima kahawa, lakini kutokana na  mabadiliko ya tabia nchi kahawa sasa  hivi haioti tena katika maeneo hayo na kama ikiota inaota  kwa shida, na changamoto hiyo inatokana na  upungufu wa maji, hivyo tunataka katika maeneo hayo yote tuwe na  aina ambazo zinaweza kuendelea kuota,”anasema Dkt Mtenga.

Anasema  ili kuwezesha zao la kahawa kufika katika  uchumi wa kati, TaCRI , imesaidia kuchangia mkakati wa uzalishaji wa miche ya mbegu chotara za kahawa ambazo zinachangia uzalishaji wa teknolojia.

STORY & PHOTO BY: Kija Elias



0 Comments:

Post a Comment