Mtafiti wa Taasisi ya utafiti wa Kahawa Tanzania TaCRI Dkt. Jeremiah Magesa akitoa maelekezo kwa mwandishi wa habari Omar Mlekwa kuhusu mbegu mpya za kahawa zilizofanyiwa utafiti. |
Zao la kahawa nchini Tanzania limekuwa likiinua hali ya maisha ya wakulima pamoja na familia zao, ambapo wakulima wamekuwa wakihimizwa kupanda miche bora ya kahawa yenye tija zaidi na inayostahimili magonjwa hatari kama vile chulebuni (CBD). Kwa kutilia maanani umuhimu wa zao hilo, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa nchi TaCRI iliyopo Lyamungo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, imekuwa ikiwashirikisha wakulima kupanda mbegu bora zitakazo mpa tija na mafanikio mkulima.
Kilimo cha Kahawa mkoani Kilimanjaro, kimeanza kuwekewa mikakati kabambe itakayowawezesha wakulima kurejesha imani ya kuendelea kulima zao hilo la kibiashara. Kwa kulitambua hilo Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa nchini (TaCRI) kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), zimeandaa mpango mkakati wa miaka mitatu ambao wamepanga kuzalisha miche bora ya kahawa zaidi ya milioni 23 ambayo wataisambaza kwa wakulima wa zao hilo.
Mkurugenzi mtendaji wa TaCRI Dkt Deusdediti Kilambo, anayasema hayo wakati alipokuwa akizungumza katika ziara ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari mkoani Kilimanjaro waliotembelea kituo hicho kwa ajili ya kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo.
Dkt Kilambo anasema Mkakati wa TaCRI kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa TCB umelenga kuzalisha miche bora ya kahawa katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2018/ 2019, 2020/ 2021.
Anasema kwa mwaka 2018/2019 TaCRI imepanga kuzalisha miche ya kahawa milioni sita ambapo hadi sasa wameshafikisha asilimia 80 ya uzalishaji wa miche ya kahawa ambapo wanazalisha kwa kutumia mbegu Chotara, vikonyo pamoja na upachikizaji.
Anasema moja ya mafanikio makubwa ambayo TaCRI imeyapata katika tafiti zake za kitaifa ni kuwa na aina bora za mpya Chotara za kahawa aina ya Arabika na Robusta , katika tasnia ya kahawa ambapo TtaCRI imefanikiwa kutoa aina bora mpya 19 Chotara za Arabika na aina 4 za Robusta zenye ukinzani dhidi ya magonjwa sugu ya kutu ya majani na chulebuni kwa kahawa aina ya Arabika na mnyaukoo fuzari kwa kahawa aina ya Robusta, zenye tija kubwa punje kubwa na muonjo mzuri.
Dkt Kilambo anazishauri halmashauri ambazo zao la kahawa linazalishwa kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu katika kuzalisha miche bora ya kahawa ili kuweza kuwafikia wakulima walio wengi kiurahisi na kukua kwa uzalishaji wa zao hilo.
“TaCRI kama mdau nazishauri halmashauri zinazolima zao la kahawa ziweze kuzalisha miche kwa wingi kwa ajili ya wakulima na kwa halmashauri ambazo hazijaanzisha vitalu tunazishauri ziweze kuanzisha vitalu vya miche kwa haraka zaidi ili waweze kuzalisha miche hiyo ya kahawa,” anasema Dkt Kilambo.
Mtafiti wa Usambazaji wa Teknolojia na mafunzo kutoka Taasisi ya utafiti wa Kahawa Tanzania TaCRI Dkt Jeremiah Magesa anasema kuwa idara ya usambazaji na teknolojia kwa njia ya mafunzo imekuwa kiungo muhimu kati ya utafiti na wakulima wa zao la kahawa.
Mtafiti wa Taasisi ya utafiti wa Kahawa Tanzania TaCRI Dkt Jeremiah Magesa akizungumza na mwanahabari Safina Sarwatt |
“Kwa mwaka wa 2018/ 2019 tulikuwa na mpango wa kutoa mafunzo kwa maafisa ugani 709 kwa nchi nzima , lakini hadi sasa hivi tumekwisha kutoa mafunzo kwa maafisa ugani 332, pia tulikuwa tumepanga kutoa mafunzo kwa wakulima wahamasishaji 423 hadi sasa hivi tumeshawafikia wakulima wawezeshaji 269,”anasema Dkt Magesa.
Dkt Magesa anasema malengo ya kutoa mafunzo kwa wakulima wawezeshaji hao, wao pia watakwenda kutoa mafunzo kwa wakulima wenzao ili waweze kuitumia teknolojia hiyo mpya.
“Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha kwamba teknolojia za kahawa, zinamfikia kila mkulima kwa njia mbalimbali, moja wapo ikiwa hiyo ya kutoa mafunzo hayo kwa vikundi vya wakulima vijijini, mafunzo kwa maafisa ugani wa wilaya kuanzia ngazi zote,”anasema Dkt Magesa.
Anaongeza kusema kuwa TaCRI imeendelea kuwekeza kwenye uzalishaji wa miche ya kahawa bora ambapo kwa nchi nzima TaCRI inavyo vikundi zaidi ya 200, huku mkoa wa Kilimanjaro pekee ukiwa na vikundi 70 vinavyozalisha miche ya kahawa.
Anasema kupitia mafunzo hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa mkulima ambapo kwa sasa mche mmoja, mkulima anaweza kuvuna hadi kilo nne za kahawa, jambo ambalo limeweza kumpunguzia mkulima gharama za uzalishaji kwa asilimia 30 hadi 50.
Aidha Dkt magesa anasema kuwa moja ya mikoa ambayo TaCRI imeamua kuwekeza kwenye miche ya kahawa ni mkoa wa Kilimanjaro ambapo wana zaidi ya mbegu za miche bora ya kahawa laki nne iliyopo kwenye vitalu kwenye halmashauri za mkoa huo.
Anasema kwa mwaka 2019 TaCRI imepanga kuzalisha miche bora ya kahawa milioni sita ambapo hadi sasa wamefikia asilimia 80 ya uzalishaji wa mbegu za kahawa, ambapo wanaizalisha kwa kutumia mbegu Chotara , vikonyo pamoja na upachikizaji na kwamba wanazalisha kwa kushirikiana na vikundi mbalimbali.
Pia Dkt Magesa anafafanua kuwa TaCRI imeendelea kuwekeza kwenye uzalishaji wa miche, ambapo inafanya kazi kwa karibu na halmashauri 52 nchi nzima, ambapo tayari halmashauri 14 zimeshaanzisha bustani za miche ya kahawa Chotara.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo Omari Mlekwa ambaye ni Mwandishi wa gazeti la Mtanzania, anasema wakulima hawana budi ya kukata tama ya kuendelea kulima zao hilo , badala yake wazingatie ulimaji bora unaotolewa na watafiti kutoka TaCRI.
Mbegu mpya katika vitalu vya TaCRI Lyamungo mkoani Kilimanjaro. |
Safina Sarwatt ambaye ni mwandishi wa gazeti la Rai amewataka wakulima kushirikiana na maofisa ugani ili waweze kuwatembelea na kuwapa ushauri wa kitaalam juu ya kuitumia teknolojia mpya ya uzalishaji wa kahawa inayotolewa na watafiti wa TaCRI.
Sarwatt anasema ili wakulima wa zao la kahawa waweze kuvuna mazao bora wana kila sababu ya kutumia mbegu za kahawa zinazozalishwa na TaCRI zenye uwezo wa kuzaa zaidi.
“Ili wakulima wa kahawa waaweze kuongeza mavuno lazima wakulima wapande miche mipya ya kisasa, ambapo tumeelezwa na wartaalam hapa kuwa mche mmoja hutoa kilo nne za kahawa kwa mkupuo mmoja na utaendelea kuzalisha kahawa kwa mikupuo mingine,”anasema.
FEATURE STORY BY: Kija Elias
0 Comments:
Post a Comment