Balozi wa Sweden nchini Tanzania Anders Sjoberg amewataka Wanachama wa Klabu za Waandishi wa habari hapa nchini kubuni miradi mikubwa itakayo wainua kiuchumi na kuacha kuendelea kuwategemea wafadhili pekee.
Balozi Sjoberg, aliyasema hayo jana wakati wa ziara yake mkoani Kilimanjaro, yenye lengo la kujionea shughuli za Klabu ya waandishi wa habari mkoani humo, jinsi inavyojiendesha, ambapo alisomewa taarifa ya Klabu hiyo na Katibu wa (MECKI) Nakajumo James.
Balozi Sjoberg, aliwataka Wanachama wa Klabu za Waandishi wa habari kote nchini kutafuta miradi ambayo italenga kuwainua kiuchumi na kuwasaidia wanahabari bila kuvunja sheria za nchi.
“Lengo kubwa la ziara yangu iliyonisukuma kufika katika Klabu yenu ya MECKI, ni kutaka kufahamu mazingira halisi ya ufanyaji kazi wa waandishi wa habari pamoja na kupata maoni juu ya sheria ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016,”alisema.
Aliongeza kuwa “Napenda niwapongeze Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Kiliamnjaro kwanza kwa taarifa yenu nzuri, ila napenda niwape changamoto kwenu ni vyema sasa mkaanza kufikiria kuwa na miradi yenu ya Klabu ambayo italenga kuwainua kiuchumi na kuwasaidia wanahabari bila kuvunja sheria za nchi.,”alisema Sjoberg.
Akitolea mfano wa miradi ambayo kama Klabu inaweza kuianzisha ni miradi ya masuala ya Afya na Elimu, ambayo ni maeneo muhimu sana katika jamii, na miradi hiyo iwe ya miaka mitano, Klabu zitafute wafadhili na kuacha kutegemea chanzo kimoja tu, hicho hakiwezi kuwa kwamua kiuchumi.
Vilevile Balozi Sjoberg, alisema miradi kama hiyo itaweza kuwapatia fedha nyingi ambazo zitawawezesha kuendesha Klabu pamoja na maisha ya kiuchumi ya waandishi wa habari ambao ni wanachama wa Klabu tu, ambao ndio watakuwa wanufaika na wasimamizi wa miradi hiyo.
“Waandishi wa habari mnazo fursa nyingi sana za kiuchumi, lakini hamtaki kuzitumia fursa hizo kwa mfano Klabu ya MECKI, mnaweza kuanza na mradi wa masuala ya Afya, ama Elimu wa miaka mitano mkaandika andiko lenu, wafadhili wapo tu, mtapata fedha nyingi na zitaweza kupunguza ukali wa maisha, lakini pia itawezesha kuwavutia hata waandishi ambao sio wanachama wavutiwe kujiunga na Klabu yenu,”alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Kilimanjaro MECKI, Bahati Mstapha alimweleza Balozi huyo, changamoto kubwa inayowafanya wanahabari wengi kutokujiunga na Klabu yao ni uwepo wa ada kubwa jambo ambalo limewafanya waandishi wengi kutokujiunga na Klabu hiyo.
“Sisi kama Klabu ya MECKI tunajiendesha kwa utaratibu wa chini ya mwamvuli wa UTPC, kupitia mpango kazi wa mwaka 2016/2020 kama matakwa ya mfadhili yanavyotutaka,”alisema Mstapha.
Aidha Mwenyekiti wa Klabu hiyo Bahati Mstapha, alimuomba Balozi huyo kuwapatia wanachama wa Klabu ya MECKI ziara ya kwenda nchini Sweden kwa lengo la kubadilishana uzoefu na waandishi wa habari nchini humo jinsi wanavyo fanya kazi, ambapo Balozi huyo alisema ni wazo zuri ambalo atalifanyia kazi na atawapatia majibu
0 Comments:
Post a Comment