Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Thursday, April 30, 2020

Wananchi wafunguka Mghwira kujitangaza kuambukizwa Corona


Wananchi mkoani Kilimanjaro wamewataka wakuu wa mikoa wengine nchini kuiga mfano wa Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Anna Mghwira kutokana na uamuzi wake wa kujitangaza kupata maambukizi ya virusi vya Corona na kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi hayo wakiwa katika utendaji wao wa majukumu yao ya kiserikali. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema kumekuwa na sintofahamu kwa baadhi ya viongozi wengi nchini kuhusu afya zao hali ambayo imekuwa ikiwafanya kupata vifo vya ghafla.

“Alichokifanya mama ni jambo la kuungwa mkono na wakuu wa mikoa wengine katika mapambano ya maradhi haya ya corona kwa kweli sikufichi viongozi wengi wamekuwa na tabia ya kutoweka bayana afya zao kitu ambacho kuna baadhi yao hufa vifo vya ghafla,” alisema Noela Lyimo wa Rombo.

Wananchi hao waliongeza kuwa wakuu wa mikoa wamekuwa mbele katika kufuatilia mambo ya watu wao huku wakisahau afya zao na kuziweka wazi pindi wanapokutwa na maradhi.

“Nafikiri viongozi wengine hususani wakuu wa mikoa wanatakiwa kuiga mfano wa mkuu wetu wa mkoa kwa kutangaza hali yake ya afya hasa kipindi hiki cha maradhi ya corona,” alisema Elizabeth Mallya wa Moshi.

Hata hivyo wananchi waliongeza kuwa uwazi unahitajika zaidi katika kukabiliana na maradhi haya ili kuchukua tahadhari ya maambukizi ya corona badala ya kujikita katika kujifariji tu.

“Unajua siku hizi dunia ni kijiji huwezi kumdanganya mtu kuhusu yanayoendelea duniani hivyo kuweka wazi kuhusu maambukizi haya ni jambo jema kwani hii Tanzania tusipojijali wenyewe hakuna wa kutujali,” alisema James Mtui.

HULKA YA DKT. MGHWIRA
Licha ya wengi kuunga mkono wakuu wa mikoa wengine na viongozi wa serikali kuweka wazi taarifa zao za afya hawakusita kufunguka kuwa kuambukizwa kwa mkuu huyo wa mkoa kunatokana na hulka aliyonayo katika ya ukarimu. 

“ Mama ni kiongozi mzuri sana anawajali watu wake, amekuwa mkarimu na ndio maana akasema haelewi aliipatia wapi. Binafsi namfahamu kuwa hupenda kusalimia na kuonana na watu kila wakati sasa kipindi hiki cha Corona ni hatari kwa kweli,” alisema Ayubu Temu wa Hai.

Kwa upande wake mwananchi aliyejitambulishwa kwa jina la Eliakunda Mosha wa Siha alisema Dkt. Mghwira atakuwa amepatia maambukizi ya Covid-19 katika ziara zake za mara kwa mara za kuwatembelea baadhi ya watu ikiwamo katika mafuriko ya hivi karibu na kuongeza kwamba ni funzo kwa wakuu wengine wa mikoa ambao hawachukui tahadhari ya ugonjwa huo.

Pia Dkt. Massawe wa Mjini Moshi anayejishughulisha na tiba mbadala amesifu afya ya Mkuu huyo wa mkoa ya kupenda kufanya mazoezi na kula vyakula vya kuujenga mwili.

“Hakika mama yuko imara kwani nilimsikia akisema hakuona dalili zozote hadi alipopima, hiyo ni kutokana na kufanya mazoezi na kula vyakula vya kuujenga mwili. Hiyo inaweza kutufundisha kitu kuwa yatupasa kuzingatia afya zetu ili kuinua kinga za miili dhidi ya maradhi mbalimbali sio tu corona hata magonjwa mengine,” alisema Dkt. Massawe

HALI IKOJE KATIKA MASOKO MJINI MOSHI?
Awali kabla ya taarifa za mkuu wa mkoa kuathirika kwa corona katika masoko maarufu ya Mbuyuni na Memorial kulikuwa na sura mbili kuhusu uvaaji wa barakoa na kunawa mikono.

Mfanyabiashara wa soko la Memorial aliyetambulisha jina moja la Shayo alisema zoezi la kunawa mikono linakwenda vizuri isipokuwa barakoa.

“Kunawa wengi wamekuwa wakilazimishwa kunawa kabla ya kupata huduma ndio maana unaona limeelewa kwa uzito mkubwa, barakoa imekuwa ikienda mwendo wa pole sasa kitendo cha Mama yetu (Dkt. Mghwira) kujiweka wazi kimeongeza uzito wa uvaaji wabarakoa kwani kuna watu walianza kuzembea kutokana na taarifa mbalimbali walizokuwa wakipata,” alisema.

Inavyoonekana sasa hali imekuwa tofauti kutokana na wengi kuingiwa na hofu kuwa maradhi yamebisha hodi mkoni humo kwa kasi tofauti na ilivyodhaniwa.

“Sikuwa nachukulia kwa uzito mkubwa sana katika uvaaji wa barakoa kwani niliona taarifa nyingi zinanichanganya tu lakini kwa sasa alivyojitangaza mkuu wa mkoa hakika naamini tuko kwenye hatari,” alisema mfanyabiashara katika soko la Mbuyuni.

Aprili 29 mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira aliweka bayana kuhusu kupata maradhi ya Corona.

“Nimepima na matokeo yamekuja yameonesha nimeambukizwa virusi vya corona, sioni dalili za ugonjwa sina homa sikohoi lakini vipimo vimeonesha, hii ni dalili kwamba Watu wengi tunaweza kuwa tunetembea tukiamini tuko salama kumbe hatuko salama, sijui niliambukizwa lini,” alisema Dkt. Mghwira.

Thursday, April 23, 2020

Miembeni Action yalia changamoto wenye ulemavu mapambano Corona


Hussein Msaki ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali Miembeni Action & Passion For People with Disability.

Watu wenye ulemavu mkoani Kilimanjaro wametoa masikitiko yao katika vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya Covid-19 wakisisitiza kuachwa nyuma katika juhudi za kuzuia maambukizi ya maradhi hayo yanayotikisa dunia kwa sasa. 

Akizungumza na JAIZMELA hili ofisini kwake Hussein Msaki ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali Miembeni Action & Passion For People with Disability yenye makao yake makuu mjini Moshi alisema, “Ili kuondokana na ugonjwa huu maana yake ni kupata maelekezo sahihi ambaye yatakuwa suluhisho la kuzuia kuenea kwa corona. Lakini kundi la watu wenye ulemavu linakabiliwa na wakati mgumu katika kipindi hiki.”

Msaki alisema changamoto katika kundi la wenye ulemavu ni kubwa kutokana na kwamba asilimia kubwa ya familia zenye ulemavu zipo katika dimbwi kubwa la umaskini na zimekuwa zikishindwa kupata huduma kama watu ambao sio walemavu.

“Sisi kama taasisi kwa muda mchache ambao ugonjwa huu umeikamata dunia na kuingia nchini kwetu,kundi la wenye ulemavu limekuwa katika mtego, umaskini umekuwa changamoto katika mapambano haya…taasisi yetu imefanya utafiti ambapo asilimia 80 ya familia ambazo zenye wenye ulemavu zimekuwa zikilelewa na mzazi mmoja; pia asilimia 70 ya familia zenye mwenye ulemavu zimekuwa chanzo cha kugawa familia hiyo,” alisema Msaki.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa maagizo yamekuwa yakitolewa na mamlaka husika lakini wenye ulemavu wamekuwa wakisahaulika hali ambayo imekuwa ikizidisha hofu kwa kundi hilo kila kukicha katika mapambano dhidi ya Corona.

“Mtu ni kiziwi maelekezo ya kujikinga na Corona anayapataje?, mtu ni kipofu anaionaje ndoo ya kunawia maji, mtu ni kiwete anaifikiaje hiyo ndoo?,nimefika katika hoteli moja nikiwa na wheelchair ndoo ya maji ya kunawa ipo juu nafanyaje sasa hapo, ndoo si rafiki, unaona jinsi gani mwenye ulemavu ametengwa, ” anahoji Msaki.

Hata hivyo Msaki anaziangukia taasisi zisizo za kiserikali, watu binafsi na serikali yenyewe kuliangalia kundi hilo la wenye ulemavu ili kutatua changamoto hizo wakati dunia ikiwa kwenye mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya Corona.

“ Tunaiomba serikali na mamlaka zake iliangalie suala hili ili kutafuta namna ambavyo wanaweza kuwasaidia watu wa kundi hili, nao wanahitaji kuishi. Wizara husika zishirikiane na taasisi husika za wenye ulemavu; gharama za vifaa vipo juu mashirika ya kijamii yajitokeza kutusaidia. Katika kipindi hiki kigumu kundi ambalo linaweza kuangamia kwa kasi kubwa ni la wenye ulemavu,” alisisitiza Msaki.
Hussein Msaki ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi isiyo ya Kiserikali Miembeni Action & Passion For People with Disability akinawa mikono kabla ya kuingia ofisini kwake.

MECKI yawaangukiwa wadau vifaa vya Corona


Mwenyekiti wa MECKI Bahati Nyakiraria
Klabu ya Waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro (MECKI), imewaomba wadau mbalimbali kuweza kuwasaidia vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona pindi pale wanapotekeleza majukumu yao.

Akizungumza na wanahabari mkoani hapo Mwenyekiti wa MECKI, Bahati Nyakiraria alisema wadau mbalimbali wamekuwa wakielekeza juhudi zao kwa wananchi huku wakiwasahau wanahabari kitendo ambacho sio sahihi kwa wanahabari nao ni wananchi wanaopaswa kulindwa.

“Katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona nchini,  vitakasa mikono kwa waandishi wa habari vinahitajika sana, ili viwasaidie kuwakinga na ugonjwa huo, sote tunatambua kazi kubwa inayofanywa na mwandishi wa habari hasa katika kutoa elimu kwa umma kuhusu Corona hivyo ni kuna umuhimu mkubwa kwa wanahabari na wao wakapatiwa vifaa hivyo ili kuweza kujikinga na kuwa salama zaidi,” alisema Nyakiraria.

Nyakiraria alisema mwandishi wa habari ni anatakiwa kwenda na kufika katika eneo la tukio kwa ajili ya kuandika na kutangaza kile kilichotokea katika tukio hilo tofauti na kada nyingine ambao wanaweza kufanya kazi zao akiwa nyumbani.

“Vita vinapotokea askari lazima atatoka na kwenda kuimarisha usalama katika eneo husika, vilevile na mwandishi wa habari ni lazima atoke ili kwenda kuandika habari zilizotokea katika eneo husika hivyo anahitaji kujikinga na usalama wake hivyo wadau wanapaswa kutambua umhimu wa wanahabari  katika kuhabarisha umma wa Watanzania  masuala mbalimbali yanayotokea hapa nchini,” alisema.

Hata hivyo ameitaka jamii kuondoka na fikra potofu kuwa wanahabari wanaishi maisha mazuri kuliko watu wengine katika jamii akisisitiza kuwa umahiri na umaarufu wao usiwafanye kuona kama hawastahili huduma kama kada nyingine.

“Tumekuwa tukitumika penye uhitaji lakini kuna wakati maisha yanakuwa magumu kutokana na kuonekana kuwa ni kazi ya kujitolea na kuonekana ni watu wenye maisha mazuri hali ambayo imekuwa ikiwaacha wanahabari njiapanda katika maisha,” alisisitiza Nyakiraria.

Klabu ya Waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro (MECKI), imewaomba wadau mbalimbali kuweza kuwasaidia vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona pindi pale wanapotekeleza majukumu yao.

Akizungumza na wanahabari mkoani hapo Mwenyekiti wa MECKI, Bahati Nyakiraria alisema wadau mbalimbali wamekuwa wakielekeza juhudi zao kwa wananchi huku wakiwasahau wanahabari kitendo ambacho sioi sahihi kwa wanahabari nao ni wananchi wanaopaswa kulindwa.

“Katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona nchini,  vitakasa mikono kwa waandishi wa habari vinahitajika sana, ili viwasaidie kuwakinga na ugonjwa huo, sote tunatambua kazi kubwa inayofanywa na mwandishi wa habari hasa katika kutoa elimu kwa umma kuhusu Corona hivyo ni kuna umuhimu mkubwa kwa wanahabari na wao wakapatiwa vifaa hivyo ili kuweza kujikinga na kuwa salama zaidi,” alisema Nyakiraria.

Nyakiraria alisema mwandishi wa habari ni anatakiwa kwenda na kufika katika eneo la tukio kwa ajili ya kuandika na kutangaza kile kilichotokea katika tukio hilo tofauti na kada nyingine ambao wanaweza kufanya kazi zao akiwa nyumbani.

“Vita vinapotokea askari lazima atatoka na kwenda kuimarisha usalama katika eneo husika, vilevile na mwandishi wa habari ni lazima atoke ili kwenda kuandika habari zilizotokea katika eneo husika hivyo anahitaji kujikinga na usalama wake hivyo wadau wanapaswa kutambua umhimu wa wanahabari  katika kuhabarisha umma wa Watanzania  masuala mbalimbali yanayotokea hapa nchini,” alisema.

Hata hivyo ameitaka jamii kuondoka na fikra potofu kuwa wanahabari wanaishi maisha mazuri kuliko watu wengine katika jamii akisisitiza kuwa umahiri na umaarufu wao usiwafanye kuona kama hawastahili huduma kama kada nyingine.

“Tumekuwa tukitumika penye uhitaji lakini kuna wakati maisha yanakuwa magumu kutokana na kuonekana kuwa ni kazi ya kujitolea na kuonekana ni watu wenye maisha mazuri hali ambayo imekuwa ikiwaacha wanahabari njiapanda katika maisha,” alisisitiza Nyakiraria.

Tuesday, April 21, 2020

Rest in Peace Father German

Father German
 






CHANZO: REGGAEVILLE



Utunzaji miti kikwazo Kampeni Moshi ya Kijani

Diwani wa Kata ya Kilimanjaro Priscus Tarimo
Imeelezwa kikwazo kikubwa katika kuifanya Moshi ya Kijani ni usimamizi wa zoezi zima la upandaji wa miti katika mitaa ya Manispaa hiyo.
Akizungumza na gazeti hili Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya Kiserikali inayojishughulisha na Utunzaji wa Mazingira mjini Moshi (Moshi Green Campaign) Priscus Tarimo wakati wa zoezi la ugawaji wa miti kwa wenyeviti wa mitaa ya Shiri-Matunda na Mjohoroni alisema kampeni ya ugawaji wa miti imekuwa ikifanyika mara kwa mara lakini inakabiliwa na changamoto ya usimamizi katika utunzaji wa miti hiyo.
“Wananchi wengi waishio maeneo ya vijijini wanategemea sana kuni kwa ajili ya kupikia, hivyo wawekezaji wa gesi wanatakiwa  kujikita zaidi kupeleka huduma hiyo vijijini, lakini katika upandaji wa miti tunakabiliwa na changamoto ya usimamizi wa hiyo miti tunayowapa ili wakaipanda kwani hadi sasa kwa takribani miaka mitatu tumetoa miti 30000,” alisema Tarimo.
Tarimo alisema viongozi wa serikali za mitaa wamekuwa nyuma katika kuhakikisha miti hii inasimama na kwa kufanya hivyo watakuwa wamefikia malengo ya kuifanya Moshi ya Kijani.
“Wenyeviti vya serikali za mitaa ndio nguzo yetu kubwa katika kuifanya Moshi ya Kijani, lakini kinachotokea ni usimamizi hafifu hali ambayo imekuwa ikisababisha miti kufa na malengo ya kampeni kwenda kwa mwendo wa pole kuliko vile tunavyotaka,” alisema Tarimo.
Hata hivyo Tarimo aliongeza kuwa wanaendelea kutoa elimu kuhusu namna ya utunzaji wa miti hiyo ambayo wanapewa ikiwamo namna ya kuitunza wakati wa kiangazi kikali kwa kutumia mbinu mbadala zenye faida na zisizotumia nguvu nyingi.
“Tumekuwa tukiwaelekeza namna ya kunyeshea miti wakati wa kiangazi kwa mfano kuna ile ya kutumia mabobo (chupa za plastiki) na kufunga na sponji kasha kutoboa tundu  na kujaza maji na kulifunga pembezoni mwa mti ambapo lita moja inaweza kukaa siku tatu na mti hautaweza kufa kwa namna hiyo,” alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Kilimanjaro Gudila Kimboka ambaye ni Katibu wa Kampeni ya Moshi ya Kijani alisema kwa mwaka huu wamefanikiwa kugawa miti zaidi ya 4,000 katika mitaa mbalimbali mjini hapo huku wakitarajia kuongeza mingine 2,000.
“Miti mbalimbali tumefanikiwa kugawa kwa wenyeviti wa mitaa ambao watapanda na kusimamia hadi kukua kwake kwani madhumuni makubwa ni kupunguza matumizi ya kuni na mkaa hali ambayo itasaidia utunzaji wa mazingira kwa ujumla,” alisema Kimboka.
Pia Kimboka alisema miaka ya zamani kabla ya 1980 hali ya mvua mkoani Kilimanjaro ilikuwa ikinyesha bila kusuasua kama ilivyo miaka ya hivi karibuni na joto lililikuwa kiasi tofauti na ilivyosasa.
Kwa upande wake Afisa Mazingira Mkoa wa Kilimanjaro, Emanuel kiyengi, aliwataka viongozi wa  Wilaya za  Kilimanjaro, kulinda misitu iliyopo kwenye maeneo yao ili kurudisha asili ya Mkoa wa Kilimanjaro kwenye hali ya kijani.
Kauli Mbiu  ya kuifanya Moshi ya Kijani ni  “Panda mti leo kwa ajili ya kumbukumbu ya Kesho.”

STORY BY: Kija Elias & Jabir Johnson
ALL PHOTOS BY: Jabir Johnson
EMAIL: jabirjohnson2020@gmail.com
DATE: Aprili 21, 2020
Afisa Mtendaji wa Kata ya Kilimanjaro Gudila Kimboka na Diwani wa kata hiyo Priscus Tarimo wakikagua miti kwa ajili ya kugawa kwa wananchi ili iweze kupandwa.
Muonekano wa habari hii katika Gazeti la LaJIJI Aprili 23, 2020 katika ukurasa wa 7
Gazeti LaJIJI Aprili 23, 2020 katika uk. 7

Nyumba 30, bajaji, magari, mifugo vyasombwa na maji


Jumla ya nyumba 30, bajaji sita, gari moja, na mifugo ambayo idadi yake haijafahamika mara moja imesombwa na maji katika kata ya Mji Mpya mjini Moshi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha tangu juzi. 

Aidha mvua hizo zimesomba pikipiki zaidi ya 20 ambazo ni za wakazi wa kata hiyo ambayo imeathirika zaidi na mvua za siku tatu katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza katika eneo la tukio diwani wa kata ya Mji Mpya Abuu Shayo alisema idadi hiyo inaweza kuzidi kutokana na mvua za masika ambazo zinaendelea kunyesha mkoani hapo.

“Ni kweli mvua zimeanza kunyesha tangu majuzi, zinatokea ukanda wa juu nyumba zaidi ya 30, magari, bajaji na miundombinu imesombwa na mvua, mifugo kama nguruwe, bata, kuku,” alisema Shayo.

Shayo aliweka bayana kutoka siku ya kwanza ya mvua hizo ambazo zilianza kuathiri mtaa wa Kwa Komba ambako nyumba sita zilianza kusomba na maji  alikwenda kwa mkuu wa wilaya ya Moshi Kippi Warioba kuhusu hali hiyo lakini hakuridhishwa na majibu ya mkuu huyo wa wilaya.

“Juzi nimekwenda kwa mkuu wa wilaya, hakunisikiliza ningeomba wakati tunapofika kuwapa taarifa watusikilize kwa haraka kiukweli nimekwazika jibu alilonipa kama ni suala la mafuriko nalijua sasa kulijua kwenyewe ndio huo leo ni maafa makubwa,” aliongeza diwani huyo

Hata hivyo diwani huyo aliitaka serikali kuchukua hatua za haraka kwani utabiri wa mvua hizi ulitolewa na mamlaka ya hali ya hewa tangu awali kuwa msimu wa masika ungekuwa na mvua nyingi ambazo zinaweza kuleta maafa.

“Serikali ichukue hatua kunusuru maisha ya watu hawa kwani ndio mwanzo tu wa mvua za masika,” alisema.

Usiku wa kuamkia Aprili 21 mwaka huu watu wa kata ya Mji Mpya na Msaranga walijikuta katika kipindi kigumu baada ya mvua hizo zilizoendelea kunyesha hadi usiku wa manane kuzoa mali za wakazi hao.

Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto zilionyesha ushirikiano mkubwa baada ya kupokea taarifa za maafa hayo ambapo lilikwenda na kutoa msaada wa kuwatoa watu waliokuwa wamepanda katika miti na mapaa ya nyumba kunusuru maisha yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti waathirika wa mvua hizo baadhi yao walisema kwa mara ya mwisho kuziona ilikuwa ni mwaka 1960 na kuongeza kuwa serikali iwasaidie kwa sasa mahali pa kujihifadhi.

Aidha waathirika hao walizionyeshea kidole cha lawama mamlaka za serikali za Tanroads na Tarura ambazo zimekuwa zikitengeneza miundombinu na kuielekeza katika sehemu za makazi na pindi mvua zinapoanza kunyesha zinamwaga maji kwa wingi katika maeneo hayo.

Kwa upande Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba alisema serikali imeunda timu ya wataalamu wa afya kwa kushirikiana na Msalaba Mwekundu ili kuangalia wahitaji na kufanya tathmini ya waathirika wa maafa hayo.

“Ni kweli kuna makazi, vifaa vimesombwa na maji hivyo kupitia wataalamu wataweza kuleta taarifa ili waweze kuwasaidia ikiwamo ni pamoja na kuwatafutia makazi kwa waathirika wa maafa haya,” alisema Warioba.

Friday, April 17, 2020

Wakurugenzi watakiwa kutunga sheria ndogondogo kudhibiti Corona


Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira amewataka wakurugenzi wa halmashauri mkoani humo kutunga sheria ndogondogo ambazo zitatumika kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Corona ikiwamo kupulizia dawa bodaboda na mabasi kila siku katika halmashauri husika.

Mghwira aliyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari jana wakati akitangaza kifo cha mtu mmoja aliyepoteza maisha kwa ugonjwa wa Corona katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi mkoani humo.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alisema ni halmashauri moja pekee ya Moshi Mjini ambayo imejitahidi kupulizia dawa katika vyombo vya usafiri ikiwa ni kuunga mkono juhudi za kudhibiti maambukizo hayo.

“Serikali imeweka nguvu kubwa katika stendi kuu ya mabasi mjini Moshi, magari yote yanapuliziwa wakati wa usiku na kuanza safari alfajiri isipokuwa huko yanakotoka kuja Moshi hayapewi huduma hiyo hali ambao ni kikwazo katika udhibiti wa huo. Mwarobaini wa hilo ni wakurugenzi wa halmashauri nyingine kutunga sheria ndogondogo ili kuvibana vyombo hivyo vya usafiri kupulizia dawa,” alisema Dkt. Mghwira.

Mbali na hilo Dkt. Mghwira aliwataka wamiliki wa maeneo ya starehe mjini Moshi ikiwamo Moshi Pazuri na Hugos Pub kufika ofisini kwake kujieleza ni sababu zipi zinazowafanya kuendelea kukusanya watu katika maeneo hayo katika kipindi hiki cha udhibiti wa maambukizi ya Corona.

“Moshi Pazuri, Hugos Pub bado yanaendelea kujaza watu sasa nawataka wamiliki wa maeneo hayo kufika haraka ofisini kwangu kujieleza,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.




Tuesday, April 14, 2020

KNCU yalirejesha Shamba la Lerongo lisiloendelezwa

Shamba za Lerongo ambalo halijaendelezwa kwa takribani miaka mitatu kutoka mwaka 2016-2020. (Picha na Kija Elias)

Chama Kikuu cha Ushirika wa Kahawa mkoani Kilimanjaro (KNCU) limepokea shamba la Lerongo lililokuwa mikononi mwa mwekezaji ambaye hakuwa kulipa kodi  kwa takribani miaka mitatu.

Hayo yanajiri ikiwa ni baada ya kushtukia mchezo mchafu wa mwekezaji waliyempa kushindwa kulipa kodi inayofikia kiasi cha Shilingi Milioni 250.

Kaimu Meneja wa KNCU (1984) Ltd Godfrey Massawe alisema  mwekezaji Otaru Manufacturing & Trading Co. Ltd alipewa kuwekeza shmba hilo mwaka 2016 kwa makubaliano ya kuliendeleza lakini ndani ya miaka mitatu hakukuwa na mafanikio ambayo walitarajia kuyapata kutoka kwa mwekezaji huyo.

“Tangu mwaka 2016 Mwekezaji hakuwahi kulipa kodi na hivyo hadi kufikisha deni la Tsh Ml 250 , KNCU ilifikia hatua ya kutumia Wakala wa kukusanya madeni ambaye tulikuwa tukimdai mwekezaji huyo ambaye hadi kufikia Desemba 2019 KNCU ilikuwa inamdai kodi ya takriban dola za Marekani 100,900 Sawa na Tsh Ml 250 ambayo ni limbikizo la kodi ya miaka mitatu,” alisema Massawe.

Hata hivyo Massawe aliweka bayana kuwa shamba hilo la Lerongo linarejeshwa kwa mara ya pili baada ya mwekezaji mwingine mwaka 2004 kushindwa kufikia malengo waliyoingia mkataba na KNCU.

“Mwaka 2004 KNCU ilimilikisha mwekezaji  kwa ajili ya kuliendeleza kwa nyakati tofauti, na ilifika wakati mwekezaji huyo alishindwa kabisa kuliendeleza kama ambavyo mkataba ulivyomtaka  na kufanyika mashauriano mbalimbali. Ili kuhakikisha kuwa yeye anarudisha kwenye nguvu yake ya kuendeleza eneo hilo,” aliongeza.

Massawe alisema mwekezaji huyo alikuwa hajailipa KNCU ambapo alipewa notisi ya siku 30 kuanzia Desemba 27, 2019 hadi Januari 31, 2020 ili kukamilisha deni hilo na walipoona ameshindwa waliamua kulirejesha mikononi mwao kwa ajili ya kutafuta mwekezaji mwingine.

“Tupo katika hatua za kutafuta mwekezaji mwingine mwenye dhamira ya kuwekeza kwenye shamba hili ili tuweze kuendeleza zao la kahawa  na kutoa ajira kwa wananchi,” alisema Massawe

Shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 541 ni miongoni mwa mashamba yanayomilikiwa na KNCU mengine ni Gararagua, Lerongo, Lyamungo na Molomo.

Kwa upande wake Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro John Henjewele, aliwataka wawekezaji wote kuhakikisha mashamba yote yanaendelezwa ipasavyo na kwamba watakwenda kwenye mashamba yote kuyakagua ili kuona kama yanaendelezwa na wale watakaoshindwa watanyang’anywa.

Henjewele aliongeza kuwa madhumuni ya mashamba hayo ni kuhakikisha kwamba mashamba yote yanaendelezwa ili kuzalisha mali, ajira kwa vijana na serikali iweze kupata kodi yake.
Afisa, Nyumba, Miradi na Mashamba ya KNCU Wilbard Lyimo



Namna ya kujiponya na uraibu wa kamari

Uraibu wa Kamari sio wazo au jambo geni miongoni mwa jamii nyingi ulimwenguni hususani Tanzania. Nafahamu kuna wengi wetu kwa sasa wamekuwa waraibu wa Kamari hadi imekuwa ni maradhi yanayowatesa wengi hususani vijana.

Watu wenye umri kuanzia miaka 45 na kuendelea nao wameonekana kuongezeka kwa wingi katika uraibu huu wa Kamari. Lakini kwa uchache, Uraibu wa Kamari ni hali ya kushindwa kuacha kucheza michezo ya kubahatisha.

Maambukizi ya virusi vya Covid-19 yamekuwa janga la dunia kwa sasa hali ambayo inazidi kutishia uchumi wa kila taifa. Hata hivyo kuna maisha baada ya janga hili kupita. Corona imeathiri kila taifa, sekta mbalimbali na mtu mmoja mmoja.

Kuanzia miaka ya 2013 suala ya Kamari za michezo maarufu kama Sports Betting lilianza kwa kasi hadi wakati wa kabla ya maambukizi ya Corona hayajazuia ilikuwa ni shida. Vijana wengi mamia kwa maelfu hawataki kufanya kazi wanaona fursa ipo katika kucheza Kamari hizo na nyinginezo. Kuna uwezekano mkubwa wa kupata uraibu wa Kamari katika michezo, katika mtandao na michezo mbalimbali.

DALILI ZA URAIBU WA KAMARI

Watu ambao wamekumbwa na matatizo ya kamri walianza na tabia ya kudanganya na baadaye kujificha au kukaa mbali na familia zao, marafiki na wengine wanaowazunguka. 

Pia watu walioingia katika Kamari walianza michezo hiyo kwa kupoteza kwa maana kila wanapocheza wanaliwa. Sasa waliendelea kutumia zaidi pesa, wakiwa na matumaini siku moja wataweza kushinda na kuibuka na kitita kikubwa cha fedha.

Lakini wakiwa na matumaini hayo wamejikuta wakiwa na madeni yasiyoisha hali ambayo imewaletea matatizo. Hata hivyo matatizo ya kamari hizi huwafanya watu wa jinsi hiyo kuwa ni watu wa kukopa.

Kama ilivyo kwa wenye uraibu wa pombe na dawa za kulevya, mtu mwenye uraibu wa Kamari atazidi kutafuta namna ya kuufurahisha moyo wake kwa kuendelea kubeti au kucheza hiyo Kamari.

Wengi wa wacheza Kamari inawawia vigumu kuachana nayo bila kujali ni kwa kiasi gani wanataka. Endapo watajaribu kujitoa wanawaza kwamba watapata matatizo mengine ya upweke na mawazo. Kwa waraibu wa Kamari wanaishia kuharibu maisha yao ya kijamii, kiuchumi na kitaaluma.
NAMNA YA KUTIBU URAIBU WA KAMARI

Katika mambo yote chini ya jua hakuna kinachoshindikana. Hivyo hata hili lina mlango wa kutokea kwa waraibu wote. Zifuatazo ni mbinu za kupambana na changamoto hii ya uraibu wa Kamari.

Mosi, Kukubali. Kama ilivyo katika uraibu mwingine hatua ya kwanza katika kuponya kabisa ni kukubali kwamba una changamoto ya uraibu wa Kamari. Ukishindwa hapo hakuna tena dawa kwani hata njia nyingine hazipenya na kuleta muarobaini wa uraibu huo. Wengi waliposhindwa kukubaliana na changamoto hiyo hakuna kilichofanikiwa na hatimaye wakateketea kabisa.

Pili, Pata usaidizi. Katika maisha tunayoishi huwezi kuwa peke yako katika changamoto zako. Ndio kuna wengine wamefanikiwa lakini kwa asilimia ndogo. Usaidizi kutoka kwa watu wako wa karibu ikiwamo familia inaweza kukusaidia kurudi katika hali nzuri na ukaendelea na ujenzi wa taifa.

Tatu, Tafuta mbadala wa Kamari. Unapaswa kujiepusha na kukaa katika maeneo ambayo shughuli za uchezaji wa Kamari zinafanyika. Unaweza kutafuta shughuli nyingine ya kufanya kama kukimbia au kufanya michezo mingine kama kuogelea na hibi nyingine unazozipenda nje ya Kamari. Lakini katika uchaguzi wa hobi hizo chagua zilizo chanya usijiingize katika zile ambazo zipo kinyume.

Nne, Jiepushe na marafiki wako wa zamani mliokuwa mnacheza wote Kamari itakusaidia. Marafiki wana sehemu kubwa mno ya kuathiri tabia zako hivyo uapojiepusha nao na kuwa na marafiki wapya inakusaidia na uraibu huishia hapo. Ukitaka kufanikiwa kuwa karibu na marafiki waliofanikiwa usipende kujifunza au kuwa na marafiki walioshindwa, watakuchelewesha kukifikia malengo yako ya kuondoka na uraibu wa Kamari.

Tano, Tafuta usaidizi wa Kitaalamu. Uraibu wa Kamari umebeba pia masuala ya kiafya. Hivyo tafuta wataalamu wa afya wataweza kukupa ushauri nasaha wakiwamo wataalamu wa saikolojia. Kwa kufanya hivyo haurudi tena katika uraibu huo na utakuwa mjenzi mzuri wa taifa lako.

Kipindi hiki cha makabiliano dhidi ya Corona inaweza ikawa ndio wakati mzuri kwa uliye mraibu wa Kamari kujitafakari na kutambua kuwa unaweza kurudi katika hali yako nzuri ya zamani kabla hujaanza kucheza Kamari.

H/shauri ya Rombo kufufua ngoma ya Iringi


Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ipo mbioni kufufua utamaduni wa ngoma za asili ulio hatarini kutoweka wa Iringi.

Akizungumza ofisini kwake, Afisa Idara ya Elimu Msingi wilayani humo Alice Uforo Makule alisema katika wilaya yake wanataka kuwa wa kwanza kuweka chachu hiyo kwa kabila la Wachagga.

Makule aliongeza kuwa makabila mengine yamekuwa na utaratibu mzuri wa kuendeleza ngoma zao za asili kwa kuwafundisha watoto wenye umri mdogo na kwa njia hiyo yamefanikiwa pakubwa kutunza asili ya ngoma zao ikilinganishwa na Uchaggani ambako hakuna utaratibu kama huo.

“Iringi ngoma hii iko mbioni kutoweka, ukiangalia makabila mengine watoto wenye umri wa chini wamekuwa wakijifunza ngoma zao huku Uchaggani ni mara chache sana kuona rika hilo likijifunza,vijana hawataki kabisa,  huwezi kuwaona wakiifuatilia,” alisema Makule.

Afisa huyo aliweka bayana kuwa wapo katika mazungumzo na Idara ya Utamaduni ya wilayani hapo kuona uwezekano wa kufanya kwa kuanzia wanafunzi wa shule za msingi ili kuendeleza ngoma asili ya Wachagga ya Iringi iliyo mbio kutoweka.

“Nikiangalia kwa jicho la baadaye naona ipo mbioni kutoweka lakini kupitia kitendo cha utamaduni tunaendelea kuwasiliana kuona jinsi gani tunaweza kufufua,” alisema Makule.

Hata hivyo aliweka bayana kikwazo kikubwa kinachokabilia jitihada hizo ni mgawanyiko miongoni mwa Wachagga na kuongezeka kuwa katika halmashauri ya Rombo wanaweza kufanikiwa lakini maeneo mengine kama Machame, Marangu itapaswa jitihada kufanyika kwa nguvu zote ili kutunza ngoma hiyo.

“Kikwazo kikubwa ni mgawanyiko wa wachagga wenyewe kuna wachagga wa Marangu, wa Machame, wa Rombo jitihada za makusudi zinafaa zifanyike ili kutunza ngoma hii ya Iringi,” alisema Afisa huyo.

Kabila la kichagga ni mkusanyiko wa makabila madogo madogo (ya Kichagga) yaliyosambaa kijiografia kuzunguka mlima Kilimanjaro kuanzia Mashariki Tarakea, Rombo hadi magharibi ya Kilimanjaro Siha, Machame. Makabila ya Kichagga ni Wa-Rombo, Wa-Marangu, Wa-Kilema, Wa-Old Moshi, Wa-Kibosho, na Wa-Machame. Makundi mengine madogo ya wachagga ni Wakirua-Vunjo, Wa-Uru, na Wa-Siha.