Ukweli na Kuheshimiana ni kiini ujenzi wa jamii zetu

Ulimwenguni kwa sasa kumejaa habari potofu na upotoshaji, ni muhimu kuhakikisha kwamba ukweli na kuheshimiana vinakuwa kiini kwa ujenzi wa jamii zetu.

Mapambano dhidi ya Habari za Uongo hayapaswi kukoma

Habari za uongo, habari za uongo zinazosambazwa kwa lengo la kumdhuru mtu au jambo fulani, huifanya jamii kuwa na sintofahamu. Zinaweza kutumika kwa madhumuni ya kiitikadi, kisiasa au hata uhalifu, kama vile ulaghai mtandaoni unaolenga kuiba data ya kibinafsi.

Utandawazi na Athari zake katika Uandishi wa Habari

Katika jamii yetu ya kisasa, ambapo habari ziko kila mahali na zinaweza kupatikana kwa kila mtu, mara nyingi ni ngumu kutofautisha kati ya vyanzo vya kuaminika na habari bandia.

Uandishi wa Habari nguzo msingi mkuu kwa ujenzi wa jamii inayojitambua

JAIZMELA blog ni miongoni mwa vyanzo vya habari, zilizochakatwa kwa kuzingatia miiko ya uandishi wa habari.

Mila na Desturi ni nguzo muhimu

Mila na desturi ni nguzo muhimu sana katika utamaduni wa jamii yoyote ile; mila ni sawa na sheria zisizoandikwa. Mila ni taratibu za maisha na mwenendo zinazofuatwa na jamii fulani katika utendaji kulingana na historia na utamaduni wao. Mila zinatambulisha maadili ya jamii husika, huelezea namna jamii inavyoendesha mambo yake.

Tuesday, February 28, 2017

Mabaraza la Madiwani Mkalama, Singida latimua watumishi

NA MWANDISHI WETU
Mkalama, Singida; Mei 2016 (Picha na Maktaba)
BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida limewafukuza kazi watumishi wake watatu na kumsimamisha kwa muda mmoja kwa tuhuma mbalimbali, ikiwamo utoro kazini.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo James Mkwega amewataja watumishi waliokumbwa na adhabu hiyo ni James Kidumo Moses  aliyekuwa Afisa Mifugo Msaidizi, Sera Ogoti  ambaye ni Afisa Muuguzi na  Selemani Ntunga  aliyekuwa Fundi Sanifu wa Maabara.
Mkwega amekiambia Kikao cha Baraza la Madiwani Mjini Nduguti kuwa watumishi hao watatu wamefukuzwa kazi kutokana na kushindwa kuonekana kwenye vituo vyao vya kazi bila taarifa yoyote kwa miezi miwili kinyume cha sheria za Utumishi wa Umma.
Pia Halmashauri hiyo imemsimamisha kazi Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF awamu tatu katika Wilaya hiyo, Athuman Dule kutokana na tuhuma za kusajili kaya 28 zisizokuwa na sifa za kuingizwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya masikini ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Mwisho wa 'viroba' Machi 1

NA MWANDISHI WETU
January Makamba
SERIKALI imewataka wazalishaji  na wafanyabiashara kuacha kuilalamikia kwa hatua iliyochukua ya kutangaza marufuku ya uzalishaji, usambazaji na matumizi ya viroba kuwa imekuja ghafla huku wakijua kwamba tamko hilo lilitolewa tangu Mei mwaka jana.
Hayo yanajiri ikiwa imebaki siku moja kuanza marufu ya uzalishaji,uingiaji, usambazaji na matumizi ya viroba pamoja na pombe kali nchini.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba amesema mpaka sasa serikali imepokea maombi ya wazalishaji tisa pekee ambao wameonyesha ushahidi wa kuelekea kuhamia kwenye teknolojia ya chupa na hivyo watahitaji muda mchache kufanya hivyo na ambao watatimiza masharti na kupata kibali maalum.
Makamba amesema serikali imekuwa ikipoteza shilingi  bilioni 600  kutokana na ukwepaji kodi na  utengenezaji wa viroba hivyo kufuatia katazo hilo litakaloanza rasmi kesho itakuwa mkakati wa kupunguza upatikaji wake kirahisi ili kiwango cha unywaji wa viroba kwa watanzania kiendane na mapato ya taifa, kulinda afya ya jamii pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Aidha wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hilo la upigaji marufuku matumizi ya viroba kwa kutoa taarifa kwenye vyombo husika ili wale wanaozalisha, kuuza na kuhifadhi waweze kuchukuliwa hatua stahiki na zawadi kutolewa kwa watakaotoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwao.

Google yakubali mchango wa ‘Malaika wa Rehema’ Abdul Sattar Edhi

CALIFORNIA, MAREKANI
Abdul Sattar Edhi enzi za uhai wake
KAMPUNI ya Google iliyo maarufu kwa utoaji wa huduma za intaneti na bidhaa zake imemkumbuka mwanzilishi wa Edhi Foundation aliyejitolea maisha yake kuwasaidia watoto maskini tangu akiwa na miaka 20 kwa kuchapisha picha za mfano kwenye nembo yake. 
Google walivyokubali mchango wake Februari 28, 2017 katika nembo yao.
Huyo ni Abdul Sattar Edhi ambaye alifariki mwaka uliopita akiwa na miaka 88, baada ya figo kushindwa kazi. Angekuwa hai leo ingekuwa siku ya kusheherekea kuzaliwa kwake miaka 89 iliyopita.Kinachostaajabisha kwa Edhi maarufu  ‘Malaika wa Rehema’ hakuwahi kupata Tuzo ya Amani ya Nobel kutokana na mchango wake mkubwa kwa watu maskini.
Hata alipokuwa anasumbuliwa na maradhi ya figo alikataa kwenda kutibiwa nje na huduma zote alizipata katika hospitali ya serikali nchini humo.Mwaka 2015 kupitia Edhi Foundation alifanya changizo la hiari la dola 100,000 za Marekani kwa ajili ya waathirika wa kimbunga cha Katrina.Edhi alizaliwa katika mji wa Bantva Gujarat nchini India kabla ya mgawanyiko wake na Pakistan Februari 28, 1928.
Google imetambua thamani ya mwanzilishi huyo kwa kusambaza nembo yake yenye mfano wa sura yake na magari ya wagonjwa ya Edhi Foundation. Akiwa amesambaza magari ya wagonjwa zaidi ya 1,800 kwenye maeneo mbalimbali nchini Pakistan, mwaka 1997 aliingia katika rekodi za dunia za Guiness kwa kuwa na shirika kubwa la kujitolea lenye magari ya wagonjwa.  
Edhi ataendelea kukumbukwa kwa kauli zake kuwa hakuna dini kubwa kama utu, hata kama mtu akisoma bado utu ni muhimu. 
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa nchini humo mwezi ujao Benki Kuu ya Pakistan inatarajia kutengeneza sarafu ya rupia 50 yenye picha ya Edhi ikiwa ni ukumbusho tosha na kutambua kazi yake nchini humo.

Monday, February 27, 2017

Waziri Mkuu Majaliwa kufanya uzinduzi Feb 28

NA MWANDISHI WETU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Kassim Majaliwa kesho atafungua mkutano wa siku moja wa Watendaji Wakuu na Wenyeviti wa Bodi za Mashirika ya Umma utakaojadili nafasi za Mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Mpango wa II wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Mkutano huu ambao umeandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina utafanyika Ikulu jijini Dar es Salaam ukiwakutanisha zaidi ya washiriki 100.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph Semboja amesema kwamba malengo ya mkutano ni kukusanya maoni ya viongozi kuhusu nafasi ya Mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano; kuzungumzia changamoto tarajiwa katika utekelezaji wa majukumu haya na; kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo.
Profesa Semboja amesema Mashirika ya Umma yana nafasi na uwezo mkubwa wa kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano, 2016/17–2020/21 wenye kaulimbiu ‘Maendeleo ya Viwanda kwa Mabadiliko ya Kiuchumi na Maendeleo ya Watu’,” .

Pamoja na mambo mengine, mkutano utajadili namna ya kuboresha mifumo ya  kiundetaji ndani ya mashirika na mahusiano miongoni mwa mashirika na taasisi za Serikali; kufungamanisha mipango ya mashirika ya Umma na Mpango wa Pili wa Maendeleo; kutathmini kiwango na aina ya rasilimali zinazohitajika kuwezesha utekelezaji wa mipango na; kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mipango.

Mauzo soko la Hisa yaongezeka

NA STELLA JOSEPH
Soko la Hisa
Mauzo katika soko la hisa yameongezeka kwa shilingi Bilioni 8.5 kutoka shilingi milioni 228 kwa juma lililopita ukilinganisha na shilingi Bilioni 8.6 kwa juma linaloishia Februari 24.
Meneja Mauzo wa Soko la Hisa na Biashara (DSE), Patric Msusa amesema idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa imeongezeka kutoka hisa laki mbili elfu na hamsini na saba hadi hisa milioni 1.2
Amesema kutokana na ongezeko la bei za hisa, ukubwa wa mtaji wa soko umepanda kwa takribani shilingi Bilioni 100 kutoka shilingi Trilioni 20.
Amesema kiashiria cha kampuni zilizoorodheshwa katika soko yaani DSEI kimepanda kwa pointi 14 kutoka pointi 2294 hadi pointi 2308 kutokana na ongezeko la bei za hisa zilizoingia sokoni.
Sekta ya huduma za kibiashara (CS) imebaki kama awali huku sekta ya viwanda ikipanda kwa pointi 340 kutoka pointi 4194 hadi pointi 4534  na sekta ya huduma ya  kibenki na kifedha (BI) ikishuka kwa pointi 100 kutoka pointi 2642 hadi 2542.

'Nokia 3310' New Model yazinduliwa

BARCELONA, HISPANIA
Toleo jipya la Nokia 3310 

KAMPUNI ya simu za Nokia imeingia tena sokoni kwa kuishangaza dunia baada ya kutambulisha toleo za zamani la simu yao Nokia 3310 ambayo lilikuwa maarufu sana mwanzoni mwa karne ya 21.
Aina hiyo ya simu kwa ukanda wa Afrika Mashariki hususani Tanzania ilikuwa maarufu kwa jina la ‘Jeneza’ kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuhimili mikikimikiki ikiwamo kutunza chaji.
Uzinduzi wa toleo hilo ambalo limeboreshwa umefanyika mjini Barcelona nchini Hispania ambako ulionyeshwa kwenye kioo kikubwa wakati wa Kongamano la Simu za Viganjani la Dunia.
Bei yake itakapoingia sokoni ni dola 52 sawa na Shilingi Laki moja na ishirini za Tanzania.
 Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema kuingia sokoni kwa toleo hilo kutashusha thamani ya simu za smart ambazo zimetapakaa kwa wingi duniani kwa sasa hususani kwa nchi zinazoendelea.
Ikumbukwe Nokia wana matoleo manne ya simu zake kwenye soko zinazoanzia euro 139 hadi 299.
Mkurugenzi Mkuu wa Nokia Rajeev Suri aliuambia mkutano huo kuwa ujio wa toleo hilo utawavuta wengi isivyo kawaida.
Nokia 3310 ya kwanza iliuza simu milioni 126 na kuwa ya 12 katika historia ya mauzo ya simu za viganjani duniani.
Kongamano la Simu za Viganjani la Dunia litatia nanga Machi pili mwaka huu huku ikitarajiwa Juni 28 hadi Julai Mosi mwaka huu kufanyika tena jijini Shanghai, China.
Toleo la kwanza la Nokia 3310 




Saturday, February 25, 2017

Facebook yakiri kusaidia mkutano wa Republican

MARYLAND, MAREKANI
Mark Zuckerberg wa Facebook
WAKATI washauri wa juu wa Rais Donald Trump wakisisitiza kuwa wataendelea kumshawishi kiongozi huyo wa Marekani kutekeleza ahadi zake alizoahidi wakati wa kampeni, imeelezwa Facebook ilichanga dola 62,500 za Marekani kufanikisha Kongamano la Siasa lenye mrengo wa Kihafidhina (CPAC).
Kongamano hilo linafanyika National Harbor, Maryland nchini humo likiwaleta pamoja wanasiasa wa chama cha Republican na wanaharakati takribani 10,000 akiwamo makamu wa serikali ya Trump Mike Spence.
Mapema kabla ya kongamano hilo la siku nne Msemaji wa Facebook alithibitisha kujihusisha kwao kwa kutoa semina za kiufundi na maeneo ya kustarehe.
Hata hivyo Facebook imeendelea kusema kuwa mchango wake huo hauna maana ya kuwa ni kampuni lenye mrengo wa kisiasa na kwamba litabaki kujihusisha na masuala ya jamii bila kujali itikadi za kisiasa.
Kuthibitisha hilo Facebook imesema inatarajia kuunga mkono makongamano mengine mawili ya kisiasa ya Netroot Nation na PDF ikiwa ni sehemu ya utafiti wao namna ambavyo siasa na teknolojia inaweza kufanya kazi pamoja.
Mapema mwezi huu Facebook ilikuwa ikisheherekea miaka 13 tangu kuanzishwa kwake huku mapato yake kwa mwaka jana yakiwa dola za Kimarekani Bilioni 27.6
Donald Trump akiwasili katika Kongamano la CPAC 2017

Friday, February 24, 2017

'iPhone 8' njiani mwaka huu

CALIFORNIA, MAREKANI

Kampuni linalojihusisha na kusanifu, kutengeneza, kuendeleza na kuuza kwa wateja vifaa vya elektroniki, programu za kompyuta na huduma za mtandao la Apple linatarajia kutoa simu iPhone 8 baadaye mwaka huu.
Hayo yanajiri ikiwa leo ni siku ya kuzaliwa mwanzilishi wa kampuni hilo, Steve Jobs aliyefariki Oktoba 2011 huku kampuni hilo likitarajia kuongeza aina hiyo ya simu ikiwa na maboresho zaidi ya matoleo yaliyopita.
Kampuni hilo limesema vioo vyenye kutumia LCD vitaendelea kubaki kwa miaka kadhaa ijayo licha ya kuingiza teknolojia mpya ya OLED.
Toleo hilo litajumuisha chaji isiyotumia waya, kioo chenye muundo wa OLED na kihisio cha Three D.
Apple imekuwa ikipanda kila siku katika kuingiza matoleo yake sokoni kutoka iPhones milioni 220 hadi 330. Jarida la Investor limesema kuingizwa kwa iPhone 8 sokoni kutachangia mauzo kwa asilimia 30.
Mwaka 2015 Apple walitumia kiasi cha dola Bilioni 1.8 katika matangazo, ikiwa ni kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2007 walipotumia dola Milioni 467 kutangaza ingizo la kwanza la iPhone sokoni.
Nchini Tanzania wengi wamekuwa na matumizi makubwa ya simu za iPhone kwa sasa baadhi yao wakiona kuwa ziliwahi kuingia mno hivyo kuendelea kuwatia umaskini kwani vipato vyao na bei za simu hizo havilingani na baadhi wakionekana kufurahi huduma zake.
Steve Jobs alifariki akiwa na miaka 56, huku waanzilishi wengine wa kampuni hilo Ronald Wayne na Steve Wozniak wakiwa bado hai.
Steve Jobs enzi za uhai wake



Wafanyabiashara Sukari ya Magendo Mbeya wakamatwa, wapigwa faini

NA MWANDISHI WETU
Sukari ya Kilombero katika pakiti zake
Zaidi ya shilingi milioni tisa zimekusanywa na wakala wa vipimo mkoani Mbeya baada ya  kupigwa faini wafanyabiashara waliokamatwa wakiuza sukari iliyofungashwa katika ujazo usiokubalika kisheria.
Kwa mujibu wa sheria ya vipimo ya mwaka 2002 sura namba 340; ufungashaji, usafirishaji na uuzaji wa bidhaa yoyote katika ujazo usio stahili ni kosa na adhabu yake ni faini kuanzia shilingi laki moja mpaka shilingi milioni 20.
Meneja wa Kanda Richard Mbonabucha amesema wafanyabiashara kumi na wawili wamekamatwa katika operesheni ya kukamata bidhaa zinazofungashwa kinyume na taratibu iliyoanza jana mkoani humo.
Amesema baada ya kukamatwa na kukiri makosa wafanyabiashara hao wametozwa faini ya kati ya shilingi laki tano na shilingi milioni moja kwa kuwa ni kosa lao la kwanza na kwamba watakaporudia kosa hilo hawatatozwa faini na badala yake watafikishwa mahakamani.
Meneja huyo wa wakala wa vipimo mbeya ametoa tahadhari kwa wananchi juu ya matumizi wa bidhaa zisizo la nembo ya ubora wala mahala inapozalishwa kama ilivyo kwa sukari iliyo kamatwa.

Baadhi ya wafanyabiashara waliokamatwa wamesema sukari hiyo inafungashwa kwenye vifuko vinavyoonyesha kuwa ni gramu mia tano lakini kiuhalishia ni kati ya gramu 320 na 350 na kwamba wao wanaipata kutoka kwa wafanyabiashara waliowataja kwa jina maarufu la Njemke.

Thursday, February 23, 2017

King Salman kuzuru Indonesia

JAKARTA, INDONESIA
Mfalme Salman wa Saudia Arabia
Indonesia imetangaza kuwa Mfalme Salman wa Saudia Arabia atazuru nchi hiyo mapema mwezi ujao akiwa na ujumbe watu 1,500.

Taarifa nyingine zinasema ufalme huo unatarajia kutumia mabilioni ya pesa kwa ajili ya kukaa kwenye hoteli na maeneo ya starehe kwenye visiwa vya Bali.Wafuatiliaji wa kiuchumi wanapinga ziara za starehe za kiongozi huyo huku akilia kuwa Saudia imekuwa ikishuka kiuchumi kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta.Katibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Indonesia Pramono Anung amesema kuwa ujio wa Mfalme Salman unatarajiwa kuanzia Machi Mosi hadi tisa na kwamba ujio huo wa pili utashuhudiwa kwa kuzuru kisiwa cha Bali.Maofisa wa Riyadh hawajathibitisha kuhusu ziara hiyo licha ya kwamba Mfalme Salman hajawahi kuficha ziara zake za kustarehe katika nchi mbalimbali.Mwaka uliopita Mfalme Salman alizuru Uturuki akiwa na ujumbe wa watu 80 na kwamba taarifa za nchini Uturuki zilisema kuwa alitumia kiasi cha dola milioni 10 katika hoteli huku akiwa amekodi magari 500 katika jiji la Ankara na Istanbul na kufanya wastani wa dola Milioni 18 katika safari hiyo.Ikumbukwe mwaka 2015 Salman alikamata vyombo vya habari kwa kitendo chake cha kwenda kula starehe kwenye ufukwe uliopo Kusini mwa Ufaransa wa Cote d’Azur baada ya ufukwe huo kufungwa kwa ajili ya watu wake zaidi ya 500 alisafiri nao.

Yoweri Museveni, Danny Faure kuzuru Tanzania

NA FELISTA HENRY
Yoweri Museveni, Rais wa Uganda
WAKAZI wa jiji la Dar es Salaam wametakiwa kutumia fursa ya kibiashara kupitia ujio wa viongozi wa juu wa Uganda na Visiwa vya Shelisheli kwa maendeleo ya nchi.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Danny Faure wa Ushelisheli watazuru nchini kwa siku mbili kwa shughuli mbalimbali zinazogusa nyanja za kiuchumi, diplomasia na ushirikiano mwishoni mwa mwezi huu.
Akizungumza ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda leo amesema ujio wa marais hao unadhihirisha kuwa serikali ya awamu ya tano inaheshimiwa na kuthaminiwa katika siasa za Kimataifa.
Danny Faure, Rais wa Shelisheli
Museveni atazuru nchini Februari 25 hadi 26 huku uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Uganda ukizidi kuimarika ambapo mwaka 2016 Tanzania ilifanya mauzo ya nje nchini Uganda na kupatikana kiasi cha Shilingi Bilioni 126 zaidi ya kile cha Shilingi Bilioni 99 mwaka 2015.

Faure atazuru nchini Februari 27 na 28.   

Vifungashio vipya kutengenezwa Tanzania

NA MWANDISHI WETU
Nembo ya Toyo Seikan Group
Kampuni ya Toyo Seikan Group Holding Ltd kutoka nchini Japan imeonyesha dhamira ya kuwekeza nchini kwa kuzalisha vifungashio vya vinywaji vilivyotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa na maofisa wa kampuni hiyo walio nchini kwa ajili ya utafiti wa masoko.
Ujumbe wa maofisa wake umetembelea kiwanda cha bia Tanzania (TBL), kwa ajili ya kujifunza jinsi kinavyofanya kazi ikiwemo kuonyesha vifungashio vilivyotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa ambavyo kampuni hiyo inazalisha.
Meneja Mkuu wa  Uendelezaji wa Biashara wa Kampuni hiyo, Yashimasa Ito, ambaye ameongoza ujumbe huo ameelezwa kuvutiwa na hatua kubwa ya kiteknolojia ambayo kampuni ya TBL imefikia na kuwa  wanayo dhamira ya kuwekeza nchini.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa kiwanda cha TBL cha Ilala, Calvin Martin, amesema ujumbe wa maofisa wa kampuni hiyo wana mikakati mbalimbali inayotekelezwa ili kuhakikisha inaenda sambamba na teknolojia za kisasa zinazotumiwa na viwanda vyote vikubwa vya kutengeneza bia na vinywaji vingine duniani.

Wednesday, February 22, 2017

Raia 14 wa India wapandishwa kortini Kisutu

NA MWANDISHI WETU
Raia wa India wafanyakazi kwenye Kampuni la Quality Group Ltd wakiwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Februari 22, 2017.
Raia wa 14 wa India ambao wanafanya kazi Quality Group wamefikishwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu likiwemo la kufanya kazi nchini bila ya kuwa na kibali.
Hati ya mashtaka, iliyosomwa na mwendesha Mashtaka Method Kagoma mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha imewataja washtakiwa hao kuwa ni Rojat Surkar na wenzake kumi na watatu.
Imedaiwa mahakamani hapo kuwa Februari 13, mwaka huu, katika ofisi ya Quality Group Ltd iliyopo katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikutwa wakiwa na viza zilizoghushiwa.
Katika shtaka la pili imedaiwa kuwa siku na mahali hapo washtakiwa hao wakiwa raia wa India walikutwa wakiishi nchini Tanzania bila ya kuwa na kibali.
Hata hivyo, washtakiwa hao ambao wanatetewa na mawakili watatu, Alex Mgongolwa na Hudson Ndusyepo wamekataa kujihusisha tuhuma hizo na wako nje kwa dhamana.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 7, mwaka huu.

NASA kutangaza 'Nje ya Mfumo wetu wa Jua'

NEW YORK, MAREKANI
Mchoro wa msanii ukionyesha sayari Kepler -452b
NA MWANDISHI WETU
Shirika la Anga za Juu la Marekani (NASA) leo linatarajiwa kutangaza ugunduzi "mkubwa" kuhusu mambo yaliyomo ‘Nje ya mfumo wetu wa jua’.

Hafla ya kutangaza ugunduzi huo itapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya NASA na katika mtandao wa shirika hilo mwendo wa saa tatu Afrika Mashariki.

Habari kuhusu tangazo hilo pia zitachapishwa katika jarida la kisayansi la Nature na baadaye katika Reddit.

Mwaka 2015, Dkt Joe Michalski wa Makumbusho ya Historia ya mambo Asilia London alisema, "Duniani, popote unapopata maji, huwa kuna uhai."


Moja ya viashiria vya kuwepo na viumbe hai anga za juu au katika sayari nyingine ni uwepo wa maji.

CHANZO: BBC

Shahidi Namba 5 kesi ya Scorpion atinga mahakamani leo

NA MWANDISHI WETU
Salum Njwete (katikati) akitoka katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Oktoba 19, 2016
USHAHIDI wa kesi inayomkabili Salum Njwete maarufu Scorpion umeendelea kusikilizwa leo katika mahakama ya wilaya ya Ilala huku shahidi wa tano ambaye ni daktari akidai kuwa mlalamikaji angechelewesha kufikishwa hospitalini angepoteza maisha.

Imedaiwa mahakamani hapo kuwa Septemba 6 mwaka jana Scorpion mwenye miaka 34 akiwa Buguruni Shell alimchoma kwa kisu mlalamikaji Said Mrisho machoni, mabegani na tumboni kisha kumnyang’anya vitu vya thamani na fedha taslimu.

Mwendesha Mashtaka Gloria Mwenda akisaidiwa na Sylivia Mitanto, mbele ya Hakimu Mkazi Flora Haule wamedai kuwa kesi ya mshtakiwa huyo mwenye miaka 34 inaendelea kwa mashahidi kuisaidia mahakama kufikia mwafaka wa shauri hilo.

Shahidi huyo ambaye ni daktari wa kitengo cha upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ameiambia mahakama kuwa jeraha la mlalamikaji upande wa kushoto wa tumbo lilitokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali ikiwa ni sentimeta 30 kutoka kwenye utumbo mwembamba.

Pia ameongeza alimpeleka mgonjwa katika chumba cha upasuaji na kulifumua tumbo zima ili kujua kama damu ilisambaa na baadaye alimshona utumbo wa ndani uliokuwa umepasua kisha akamalizia kumshona nje na kumpeleka wodini kuendelea na matibabuu ya kawaida.
Kesi hiyo itatajwa tena Machi 8 na kuendelea kusikilizwa Machi 13 mwaka huu.


Tuesday, February 21, 2017

Happy Birthday Robert Mugabe

Robert Mugabe
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe anatimiza miaka 93 ya kuzaliwa kwake (Alizaliwa Februari 21, 1924). Mugabe amekuwa akijulikana kwa kauli kali tangu alipoipa uhuru nchi hiyo mwaka 1980.
Jina lake halisi ni Robert Gabriel Mugabe, Baba yake alikuwa fundi seremala na mama yake Bona alikuwa mtumishi wa kanisa akihudumia watoto. Katika familia yao walizaliwa  sita Miteri (Michael), Raphael, Robert, Dhonandhe (Donald), Sabina na Bridgette.
Alimwoa mwanadada Sally Hayfron mwaka 1967 aliyedumu naye hadi mwaka 1992 alipofariki.
Mwaka 1996 alimwoa Grace Marufu ambaye anaishi naye hadi sasa.
Aprili 17, 1980 alikabidhiwa kijiti cha kuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo. Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye uwanja wa Rufaro allitangaza rasmi kuwa haitaitwa Rhodesia ya Kusini bali itaitwa Zimbabwe.
Kiongozi huyo ambaye kwa sasa anashikilia rekodi ya kukalia kiti hicho kwa muda mrefu tangu mwaka 1987  kwa tiketi ya ZANU-PF.
Mwaka 1980 hadi 1987 alikuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo.
Mugabe ni wa kabila la Washona. Alizaliwa kutoka kwenye familia maskini ya Kutama nchini humo wakati huo ikiitwa Rhodesia ya Kusini.
Alisoma katika Chuo Kikuu cha Fort Hare na baadaye kuwa mwalimu katika nchi ya Zambia na Ghana.


Monday, February 20, 2017

Happy Birthday ya Robert Mugabe, kesho

HARARE, ZIMBABWE
Robert Mugabe
Kesho Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe anatimiza miaka 93 ya kuzaliwa kwake huku akisisitiza kuwa hajamuona mtu sahihi wa kumkabidhi kijiti.
Kiongozi huyo aliyepo madarakani tangu walipojipatia uhuru mwaka 1980 amekaririwa akisema wanaopaswa kusema aondoke madarakani ni chama chake, lakini mpaka sasa Kamati Kuu imemtaka asimame kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Mugabe ambaye amekuwa mahiri kwa kauli kali ameongeza walio wengi katika nchi yake wanataka aendelee kwani hawaoni mbadala wa atakayepokea kijiti.
Hata hivyo amekana kuwa na matatizo ya kiafya licha ya kuwa na safari za mara kwa mara za kwenda Dubai na Singapore.
Katika hotuba amekuwa akisoma kwa muda mfupi na taratibu tofauti na walivyozoea. Ikumbukwe Septemba mwaka jana alisoma hotuba ambayo ilikuwa sawa na ile aliyoitoa mwezi mmoja kabla bila kujua, hali iliyoibua maswali kuhusu hali yake ya afya.
Aidha Mugabe alimsifia Rais wa Marekani Donald Trump kwa kuendelea kuimarisha sera za utaifa ambazo ameziita kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya Zimbabwe.
Mugabe ambaye ni mwenyekiti wa ZANU-PF atasimama kwa uchaguzi wa mwaka 2018, ambapo juma lililopita mkewe Grace Mugabe aliibuka na kusema kuwa anaweza kuwa mtangulizi wake huku akikaririwa kwa kauli tata kuwa endapo Mungu ataamua Mugabe kufa basi wataipitisha maiti yake ipigiwe kura.
Endapo kiongozi huyo atachaguliwa na kumaliza muhula wake mwingine atafikisha miaka 100.

Mtoto wa miaka saba aomba kazi Google

HEREFORD, ENGLAND
Chloe Bridgewater
Mtoto wa miaka saba ameomba kazi katika kampuni ya Google, kwa kumwandikia barua yenye maneno takribani 260 Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hilo.
Mtoto huyo wa kike anayefahamika kwa jina la Chloe Bridgewater ambaye anaishi Hereford nchini England amemwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Google nchini Marekani Sundar Pichai kuwa anataka kufanya kazi.
Baba wa mtoto huyo Andy Bridgewater alimsaidia mwanaye kwa kuipeleka barua hiyo ambayo ilichapishwa kwenye gazeti la Bussiness Insider ikionyesha madhumuni ya mtoto huyo.
Mtoto huyo ambaye aliandika katika barua hiyo kuwa anapendelea kucheza na maroboti ambapo baba yake alimwambia kuwa ili aweze kujua zaidi atapaswa kujifunza kompyuta na mahali sahihi anapopenda ni Kampuni la Google.
Pia binti huyo alisisitiza kuwa ana uwezo mkubwa na walimu na baba yake wanamwambia kuwa ana akili darasani.
Barua ya Chloe Bridgewater kwenda Google
Kwa upande wao Google walimjibu binti huyo kuwa aendelee kuishi katika ndoto hiyo na wanatarajia kuwa atakapomaliza masomo wanasubiri barua ya kuomba kazi katika kampuni hilo.
Baba yake ni muuzaji wa majokofu na vifaa vyake


Friday, February 17, 2017

Thursday, February 16, 2017

Gereji ya kurekebisha vifaa vya kijeshi yazinduliwa

PHNOM PENH, CAMBODIA

Gereji ya Vifaa vya Kijeshi iliyojengwa kwa msaada wa Serikali ya China imezinduliwa nchini Cambodia.Ujenzi wa gereji hiyo ambayo itatumika kurekebisha vifaa vya kijeshi ilianza kujengwa mwaka 2015.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa Cambodia Jenerali Tea Banh akiwa na Balozi wa China nchini humo Xiong Bo wamezindua gereji hiyo katika Kikosi magari ya kijeshi Namba 99 kilichopo mjini mkuu Phnom Penh. Taarifa kutoka nchini humo zinasema gereji hiyo yenye teknolojia mpya ina ukubwa mita za mraba 500 ambayo itakuwa muhimu kwa Jeshi la Ulinzi la nchini hiyo. Uhusiano wa Cambodia na China uliimarika baada ya kumalizika kwa vita ya Cambodia na Vietnam mwaka 1991.

Wakati huo huo takwimu zinaonyesha kubwa idadi kuwa ya Wachina imekuwa ikiongezeka katika nchi ya Ukraine kutokana na urahisi wa kupata viza na uhusiano wake na taifa hilo la Ulaya. Takwimu hizo za Ukraine zimeonyesha raia wa China 20,555 wamezuru nchi hiyo mwaka jana ikilinganishwa na 13,602 mwaka 2015. Tangu Juni 2016 Ukraine ilianza kutoa viza ya siku 15 kwa wafanyabiashara na watalii raia wa China waliokuwa wakifika nchini humo kwa kutumia uwanja wa ndege wa Kiev Boryspil. Miezi minne baadaye Ukraine iliweza kutunga sera ya kuongeza matumizi ya viza hiyo hadi mji wa Odessa ulio kusini mwa Bahari Nyeusi.

REA kutoa mafunzo ya Nishati

NA FELISTA HENRY

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) wanatarajia kutoa mafunzo ya majuma mawili kwa mafundi na waendelezaji wa vyanzo vya umeme unaozalishwa kutokana na rasimali za nishati jadidifu.
Serikali kupitia REA imeanza utekelezaji wa mradi kabambe wa awamu ya tatu wa kusambaza nishati vijijini utakaojumuisha vijiji 7,873 katika wilaya na mikoa yote ya Tanzania Bara ambao utatekelezwa kuanzia mwaka huu wa fedha hadi 2020/21.
Mkurugenzi Mkuu wa Nishati vijijini Mhandisi Boniface Gissima amesema malengo ya mafunzo hayo ambayo yataanza mwishoni mwa Aprili  hadi Juni mwaka huu ni kuwajengea uwezo mafundi na waendelezaji wa teknolojia waliopo maeneo ya vijijini ili waweze kutoa huduma bora na endelevu.
Mikoa itakayohusika na mafunzo hayo ni Mara, Geita, Tabora, Simiyu na Arusha ambako mafunzo kuhusu nishati itokanayo na mionzi ya jua na utayarishaji wa mpango biashara yatatolewa.
Hata hivyo Gissima amewataka waombaji wa mafunzo hayo wawe na elimu ya kidato cha nne huku wenye vyeti vya ufundi VETA  daraja la kwanza watapewa kipaumbele na watume kabla ya Machi 17 mwaka huu.

Wednesday, February 15, 2017

Mfumko wa bei wapanda Misri, watalii wapungua

CAIRO, MISRI     
Utalii nchini Misri umeshuka kutokana na thamani ya fedha kukosa thamani kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ajali ya ndege iliyotokea Oktoba 31, 2015 kwenye milima ya Sinai hivyo kukatisha safari za mashirika makubwa ya ndege.
Takwimu za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), zimeonyesha bei za bidhaa nchini Misri zimepanda ghafla ukilinganisha na miaka iliyopita.
Kupanda kwa bei katika bidhaa mbalimbali nchini humo kumefika hadi asilimia 29.6 mwezi uliopita hivyo kuwa mfumko mkubwa kuwahi kutokea tangu Januari 2011.
Katika ripoti ya IMF imeonyesha Desemba mwaka uliopita nchini humo mfumko ulifika asilimia 24.3
Katika sekta ya utalii ambayo imekuwa muhimu kwenye upatikanaji wa fedha za kigeni imeshuka tofauti na ilivyotarajiwa.
Watalii nchini humo wamepungua nchini humo kutoka milioni 9.3 mwaka 2015 hadi milioni 5.3 mwaka jana.
Vyanzo vingine vinasema kupungua kwa watali nchini humo kumechangiwa na kuzuia kwa mashirika ya ndege ya Russia na Uingereza baada ya ajali ya ndege Oktoba 2015 kwenye milima ya Sinai.

Mkurugenzi wa IMF Chris Jarvis amesema walitarajia mfumko huo utajitokea na kwamba Misri imeanza vizuri kujipanga kuzuia kutokana na thamani ya pesa yake kushuka.

Kim Jong-nam afariki dunia

KUALA LUMPUR, MALAYSIA
Kim Jong-nam
Aliyekuwa ndugu wa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un ameuawa nchini Malyasia katika uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur.
Maafisa wa Polisi nchini Malaysia wamesema kwamba Kim Jong Nam alishambuliwa juzi wakati alipokuwa akitarajia kusafiri kwenda Macao na kuongeza kuwa kabla hajafariki dunia wakati akipelekwa hospitalini, alitoa maelezo kuwa alivutwa kutoka kwa nyuma na kumwagiwa kitu kioevu usoni mwake.
Aidha maafisa hao wamesema wakati mauti yanamkuta alikuwa anatumia pasipoti yenye jina la Kim Chol. Hata hivyo taarifa nyingine zinasema Kim Jong-nam amekuwa akijulikana kwa kutumia pasipoti bandia. Mwaka 2001 Kim Jong-nam alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Tokyo akitumia pasipoti bandia kwenda Disneyland.

Televisheni moja imeripoti kuwa Kim Jong-nam alivamiwa na watu kutoka Korea ya Kaskazini. Raia wa Malayasia na Korea ya Kaskazini wanaweza kusafiri kwenda nchi hizo bila kutumia viza.

Tuesday, February 14, 2017

Vifo vya mapema India vyatisha

NEW DELHI, INDIA
Uchafuzi wa hali ya hewa kutoka viwandani.                    
UTAFITI wa kimataifa unaonyesha kuwa vifo vya mapema takribani milioni moja na laki moja nchini India vimetokea kutokana na uchafuzi wa hewa unaokua kwa kasi huku sikukuu za Diwali nchini humo zikichangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hilo.
Aidha utafiti huo umebaini kuwa India itaipita China ambayo ilikuwa inaongoza kwa kutokea kwa vifo vya mapema kutokana na chembechembe hatari za PM2.5.
Taasisi ya Utafiti ya Boston  na ile ya Seattle nchini Marekani kwa pamoja zimesema karibu asilimia 50 ya vifo hivyo vimetokea kati ya mwaka 1990 na 2015.
Profesa Michael Brauer wa Chuo Kikuu cha British Columbia amesema kuwa kinachotokea India ni janga kubwa kutokana na uwekezaji mkubwa katika viwanda, kuongezeka kwa idadi ya watu na uwepo wa watu wenye umri mkubwa nchini humo.
Meneja wa Afya ya Mazingira na Jamii wa Taasisi ya utafiti wa sera za Afya nchini India Bhargav Krishna amesema uchafuzi wa hewa unaidhoofisha nchini hiyo kutokana na urasimu kuwa utungaji wa sera ambao serikali imekuwa iking’ang’ania kutoa mwongozo.
Marekani na Ulaya zimefanikiwa kwa kipindi hicho kupunguza asilimia 27 licha ya vifo vya mapema  kuwa 88,000 kwa Marekani na 258,000 barani Ulaya.
Asthma na vichomi vimekuwa changamoto kubwa hivyo kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi yake vizuri kutokana na chembechembe zinazotoka kwenye magari na viwanda vinayotumia injini za dizeli pia vumbi la asili kuingia katika mishipa ya damu kupitia mapafu.
Idadi ya vifo vinavyotokana na uchafuzi wa hewa nchini India imeongezeka kutoka milioni 3.5 mwaka 1990 na kufikia milioni 4.2 mwaka 2015.
Msongamano wa magari katika jiji la New Delhi, India
CHANZO: CNN

Makonda ataja moja akabidhi majina 97 ya wanaojihusisha na dawa za kulevya

NA PENDO MICHAEL
Gazeti la Habari Leo Februari 14, 2017 kuhusu Mkuu wa Mkoa Paul Makonda kukabidhi majina 97
SIKU moja baada Rais John Magufuli kumwapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga na kumtaka kusimamia kwa uadilifu mkubwa kwa mujibu wa sheria, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amemkabidhi majina 97 ya wanaojihusisha na biashara ya hiyo.
Hata hivyo Makonda alimtangaza mtu mmoja aitwaye Rashid Said maarufu Chidi Mapenzi akimtaka kufika Kituo cha Kikuu cha Polisi.
Makonda alimkabidhi majina hayo bila kuyataja katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere jana huku akisema malengo ya kuanzisha mapambano hayo ni kuwasaidia wahanga wa dawa hizo.
Katika siku za hivi karibuni Makonda amekuwa akilaumiwa na watu wa kada mbalimbali kwa namna anavyoendesha kampeni kupambana na dawa za kulevya, baada ya kitendo cha leo wadau mbalimbali wamesema huenda amepata ushauri na maoni ya namna ya kuendesha zoezi hilo.
Kwa upande wake Sianga ameahidi kutoa ushirikiano, na ameongeza kuwa atashughulikia kesi zote ambazo zimekuwa zikivurugwa na mahakimu.

Wengine waliokuwapo katika hafla hiyo ni Mchungaji George Fupe wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Sheikh Mkuu mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Alhadi Mussa, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna Simon Sirro.
Paul Makonda akizungumza jambo kuhusu dawa za kulevya.
Gazeti la Tanzania Daima Februari 14, 2017 kuhusu  Makonda na vita dhidi ya Dawa za Kulevya