Wasanii wanaoishi jijini Dar es Salaam wenye asili ya Kilimanjaro wametakiwa kurudi mkoani humo kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuonyesha njia ya namna ya kuutangaza utalii kwa manufaa ya Watanzania.
Akizungumza katika kikao cha mpango kazi Mwenyekiti wa Kilimanjaro Arts Development Group (KADG), Victor Mushi ametoa wito wa wasani hususani waigizaji ambao wanaishi Dar es Salaam kurudi mkoani mwao kwa ajili ya kutangaza vivutio vilivyopo mkoani.
Mushi alisema walio wengi wamekuwa wakifahamu mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Wanyama ya Kilimanjaro (KINAPA) pasipo kufahamu kwamba kuna vivutio vingine.
“Sisi tunalenga kitu kimoja, kuutangaza utalii wa Kilimanjaro Rais (Samia Suluhu Hassan) ametuhusisha sisi kuongeza mambo mengine baada ya kuitangaza Royal Tour ameona mafanikio yake,” alisema Mushi.
Mushi alisema mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ukichangia pakubwa kutokana na wasanii wake kufanya vizuri lakini changamoto kubwa wameshindwa kuutangaza mkoa wao waliotokea.
“Wasiwe wa kuigiza katika Nyanja moja ya mapenzi, Mama (Rais Samia) ashaonyesha njia, sisi tunatakiwa kufuata njia ya Mama ili tuweze kufika mbali na mkoa wa Kilimanjaro ndio alama muhimu ya kuanzia njia hiyo,” alisema Mushi.
Kwa upande wake Katibu wa KADG Evarist Siriwa alisema sanaa imekuwa ikitumika kuelimisha, kuhamasisha jamii kutoka sehemu moja na kuipeleka sehemu nyingine kwa namna mbalimbali.
“Wasanii wana mchango mkubwa sana katika jamii kama wakipewa fursa ya kuieneza kwa vitendo, kwa maneno katika yale ambayo tumekubaliana katika jambo fulani, kwa sasa jambo lenyewe ni utalii wa mkoa wa Kilimanjaro,” alisema Siriwa.
Hata hivyo Mlezi wa KADG Chifu Omary Mwariko ‘Mhelamwana’ alisema endapo wasanii hao wanaoishi nje ya Kilimanjaro watakubali kurudi kampeni ya Rais Samia ya Royal Tour itakuwa imefanikiwa.
“Wasanii mbalimbali wakiwamo Nandy, Maua Sama, Jacquline Wolper na wengine waliozaliwa humu waliowahi kuishi humu wanaweza kurudi nyumbani kuitangaza Kilimanjaro na hii itawapa hamasa wengine wanaochipukia kuona sio tu mapenzi katika script zao bali hata utalii unaweza kuingizwa humo na ukaleta maana,” alisema Chifu Mwariko.
Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Mkoa wa Kilimanjaro uliopata hadhi ya kuitwa mkoa mnamo mwaka 1963 ulishika nafasi ya nane katika mikoa yote nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya watu takribani 124 kwa kilometa moja ya mraba.
Miongoni mwa vivutio vya utalii vilivyosahaulika ni pamoja na mahandaki yaliyotumiwa na Mangi, kaburi la Mangi Horombo aliyekuwa na kimo cha futi 8.2
0 Comments:
Post a Comment