Akitoa tathmini ya matokeo hayo Julai 22,2022 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bi. Mwajumba Nasombe, amezitaja shule hizo kuwa ni shule ya sekondari Usangi day iliyoshika nafasi ya kwanza kiwilaya na kimkoa na shule ya sekondari ya Vudoi iliyoshika nafasi ya pili.
Amesema shule ya sekondari ya Usangi day, imeshika nafasi ya kwanza kiwilaya na Kimkoa, ambapo kitaifa imeshika nafasi ya 18, na kuongeza kuwa jumla ya watahiniwa 133 sawa na asilimia 93.7 walipata ufaulu wa daraja la kwanza na tisa sawa na asilimia 6.3 walipata daraja la pili.
Nasombe amesema kuwa jumla ya watahiniwa 829 katika wilaya hiyo walifanya mtihani huo kutoka shule 11 za wilaya hiyo ambapo amesema kati ya shule hizo sita ni za Serikali na tano ni shule za kibinafsi, ambapo pia alitumia fursa hiyo kutoa ujumbe kwa shule zinazomilikiwa na watu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Usangi day, Irene Lema, Joyce Bashungwa na Hosiana Mziray, wamesema moja ya changamoto inayowakabili shule hipo ni pamoja na ukosefu wa walimu wa mchepuo wa sayansi, vitabu masomo ya biashara, bwalo la chakula pamoja na uchakavu wa miundomnbinu ya majengo ya shule.
Kwa upande wake afisa elimu sekondari wilaya ya Mwanga Ashimun Reuben Mnzava, amewapongeza walimu kwa kushirikiana katika malezi na usimamizi wa masomo kwa wanafunzi wote na kuwataka waendeleze mbinu hizo kwa wanafunzi wengine waliobaki ili wilaya ya Mwanga ije kushikea nafasi ya juu kitaifa.
Awali akisoma taarifa kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Usangi day Emmanuel Masanja, amesema kuwa shule hiyo imeendelea kufanya vizuri kwenye mitahihani ya kitaifa kutokana na matokeo ya watahiniwa wa shule hiyo kuendelea kuwa mazuri kila mwaka.
Masanja amesema kuwa mbali na mafanikio hayo ambayo amesema yanaendelea kukua mwaka hadi mwaka, bado shule hiyo, inakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo amesema ni pamoja na ukosefu wa bwalo na maktaba shuleni hapo.
Aidha mkuu huyo wa shule ameipongeza serikali kwa miradi iliyotekelezwa shuleni hapo kupitia fedha za mfuko wa Uviko-19 ambapo shule hiyo ilipata madarasa mawili, matundu 12 ya vyoo, ongezeko la kiwango cha maji pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kunawia mikono.
0 Comments:
Post a Comment