Mwanasiasa mkongwe mkoani Kilimanjaro Dkt. Malisa Godfrey, amesema
mwamko wa watu kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali ndani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) kunatokana na nia zao za kutaka kukitumikia chama hicho tawala.
Dkt. Malisa ambaye amechukua fomu ya kuwania nafasi ya
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro alisema kuwa taratibu njema za kisiasa
ndani ya CCM pia ni sababu nyingine inayopelekea hali hiyo.
“Kama ilivyo maeneo mengine duniani kwenye nchi ambazo
zinazingitaia demokrasia, kinapokuja kipindi cha uchaguzi ndani ya vyama vya
kisiasa homa miongoni mwa wanansiasa huwa inapanda na kushuka na hili hupelekea
wale wanaoamini wanaweza kukitumikia chama kujitokeza kwa wingi”, alisema.
Alisema katika Tanzania ya leo demokrasia inaenda vizuri na
kwamba hilo linadhihirishwa na uwazi ulioko sasa ndani ya CCM na uongozi wa
chama hicho kuridhia yaweko mazungumzo yanayohusiana na swala la katiba mpya.
“Ile hali iliyokuweko miaka ya nyuma ambapo watu waliamini
wananyimwa haki zao inaendelea kutoweka, hata vyama vingine za kisiasa
vinaonyesha kuridhika na hali hii, ni wazi kabisa ya kuwa kukua kwa demokrasia
msingi wake ni utawala unaokuweko katika uongozi”, alisema.
“Katiba ndio msingi wa demokrasia katika nchi yoyote duniani, ndio dira ya kuongoza nchi, baada ya Watanzania kuonyesha mahitaji ya kuweko kwa katiba mpya kwa muda mrefu, CCM ambayo huwa haikurupuki imeonyesha nia yake katika swala hili tena kwa kuanzia ngazi ya chini waliko wananchi wengi”, alisema.
Alisema
kuwa wakati wa umefika kwa Tanzania kupata katiba mpya ambayo alisema ujio wake
utakiimarisha CCM yenyewe, vyama vya kisiasa hapa nchini, taasisi mbalimbali na
Taifa kwa ujumla.
0 Comments:
Post a Comment