Chifu Frank Marealle (kushoto) akipokea fimbo ya uchifu kutoka kwa Chifu Omary Mwariko Mhelamwana katika hafla fupi ya kukabidhiwa iliyofanyika Marangu mkoani Kilimanjaro
Kutokana na
utendaji wa kazi wa Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan ndani na nje ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chifu wa Kizigua Omary Mwariko ‘Mhelamwana’
amependekeza cheo cha Rais kifutwe na kiwepo cha malkia.
Akizungumza
wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi fimbo Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu na
Wazee wa Mila na Desturi Tanzania (UMT) Frank Marealle, Chifu Mhelamwana
alisema, “Nimefikiria kwa machifu wenzangu, tugeuze jina la Rais (Samia Suluhu)
naye akapata heshima ya kuitwa Malkia wa Tanzania.”
Chifu
Mhelamwana alisema jamii zilizo nyingi barani Afrika zimekuwa zikimkandamiza
mwanamke na kumuona sio chochote kwa muda mrefu sasa hivyo ni vema Tanzania
ikaongeza juhudi dhidi ya mapambano hayo kwa vitendo.
“Hii ndio
sababu ya kutaka mama huyu (Rais Samia Suluhu)
aitwe malkia na iwe mwanzo wa kumpa nafasi mwanamke wa kushika nyadhifa za juu
katika serikali,” alisema.
Chifu
Mhelamwana aliongeza, ‘Sisi machif tunapendekeza Rais Samia aitwe Malkia wa
Tanzania, kwasababu ndiye mwanamke pekee na wa aina yake na hata barani Afrika
iwe inasikika hivyo. Sio kwamba yeye alipenda hivyo, ni kwamba aliandikiwa na
Mungu.”
Aidha chifu
huyo alisisitiza Waingereza licha ya kuitawala ardhi ya Tanzania lakini bado
hawakumpa nafasi mwanamke wakati wao kwa miaka mingi wamekuwa wakiongozwa na
Malkia.
“Malkia
Elizabeth ni mfano mzuri kwa waingereza katika ardhi yao, cheo cha juu kabisa
ambacho ni lazima awe mwanamke, sisi hapa Afrika tunataka tuwe wa kwanza ili
kuondoa ukandamizaji wa wanawake kwenye jamii zetu,” alisisitiza chifu huyo.
Chifu huyo
alisema katika mchakato wa kupata katiba mpya unavyoiendelea ni vema cheo cha
malkia kikapata nafasi na kuvunja utaratibu wa miaka mingi ambao umeshindwa
kumsaidia mtanzania na kuwafaidisha wachache.
“Sisi
hatutaki tena wanaume watawale hata kama mimi mwenyewe ni mwanaume…hili
tunalitaka katika katiba mpya liingie , licha ya kwamba wengi wanataka
apatikane Rais Mwanaume,” alisema Chifu Mhelamwana.
Awali wakati
akikabidhi fimbo yake kwa mwenyekiti wa UMT, Chifu Mhelamwana alisema, “ Mimi
Chifu Omary Mhelamwana natoa fimbo hii iliyo takatifu kwa ajili ya shughuli za
uchifu wa Marealle .”
Kwa upande
wake Chifu Marealle alisema, “Wewe umenijengea heshima kubwa sana ya
kunikabidhi fimbo hii. Asante Sana , Asante Sana; Tumekuwa tukifanya mikutano
mikuu ya machifu ya kila mwaka , sijawahi
kupokea zawadi yoyote kutoka kwa machifu.”
Chifu Mhelamwana
ndiye aliyetengeneza kifimbo cha baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1922-1999) na kukabidhi kwa ajili ya
uongozi wa taifa hili.
Mwaka 2021 Chifu
alipendekeza kuwapo kwa noti ya shilingi 50,000 au shilingi 100,000 ambayo
itakuwa na picha ya Rais wa awamu ya Tano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
kutokana kazi alizozifanya.
0 Comments:
Post a Comment