Wednesday, July 6, 2022

Dkt. Mpango kufungua maabara ya kisasa Kibong’oto Julai 16

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango anatarajiwa kufungua jengo jipya la Maabara katika Hospitali Maalum ya Rufaa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto mnamo Julai 16 mwaka huu.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari Mkurugenzi wa Hospitali hiyo iliyopo Siha mkoani Kilimanjaro Dkt. Leornad Subi alisema ujenzi wa jengo hilo uliofanywa na serikali umegharimu kiasi cha shilingi 12 bil.

“Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango  atafika katika hospitali hii kwa madhumuni makuu ya kufungua jengo jipya la maabara ya kisasa ya ngazi ya daraja la tatu ambalo limejengwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 12.4,” alisema Dkt. Subi.

Uzinduzi wa jengo hilo lenye vifaa vya kisasa ni mwendelezo wa kuboresha afya duniani huku Kibong’oto ikichangia pakubwa kuondoa matumizi ya sindano kwa wagonjwa wa kifua kikuu sugu.

“Tunatarajia kutoa huduma bora ambazo zitazingatia sayansi na viwango...tuna imani kwamba tutachangia na tumeshaanza  kuchangia...moja ya tafiti ambazo tumeweza kuzifanya mojawapo ni ile ya kuondoa matumizi ya sindano kwa wagonjwa wa kifua kikuu sugu...tulikuwa tunachoma kwa miezi miwili na sasa tumeziondoa, badala yake tunatumia vidonge,”aliongeza.

Aidha maabara hiyo itafanya shughuli nyingi za kisayansi ikiwamo ya utengenezaji wa chanjo mbalimbali za magonjwa ambukizi na uchunguzi wa vinasaba.

“Sasa tunaweza kupata fursa ya kutengeneza chanjo, lakini pia tutapata fursa ya kuangalia usugu wa dawa, lakini pia viwango vya dawa mwilini sio unakunywa tu  dawa lakini hujui kiwango chake,” alisisitiza Dkt. Subi

Katika suala la Uviko -19 Dkt. Subi alisema maabara ya Kibong’oto imetoa mchango mkubwa kimataifa kwa kutambua anuwai za virusi mbalimbali kutokana na uwepo wa mitambo ya kisasa.

Hata hivyo Hospitali Maalum ya Rufaa kwa Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto imeendelea kujizolea umaarufu nchini kwa kuwa na wabobezi wenye viwango vya juu pale ilipotoa mwanasayansi bora wa mtafiti wa kike mwaka huu.

“Kama wiki mbili, tatu zilizopita makamu wa Rais amemkabidhi tuzo ya mwanasayansi bora mtafiti wa kike Tanzania, ametoka katika hospitali ya Kibong’oto , hatuna shaka kwamba tunafanya vizuri na tunataka tufanye mambo mazuri zaidi na makubwa na watanzania waweze kuyaona,” alisema Dkt. Subi

Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa watanzania kutambua kuwa bila sayansi katika ulimwengu huu hakuna maendeleo, kwani Kibong’oto mbali na maabara inaendelea kuboresha huduma zake ikiwamo jengo la ICU la kisasa.

Kwa miaka mingi Kibong’oto ambayo mwaka huu inatimiza miaka 96 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1926 ilikuwa ikifahamika kama Hospitali ya Kifua Kikuu nchini ambapo mwaka 2010 serikali iliipandisha hadhi na kuwa Hospitali Maalum ya Rufaa kwa Magonjwa Ambukizi  Tanzania.












0 Comments:

Post a Comment