Monday, July 4, 2022

Wanachama waibana mbavu KNCU (1984) Ltd

 

Wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU) wamegomea mpango wa chama hicho wa kukata shilingi mia moja kwa kila kilo moja ya kahawa kwa ajili ya uendeshaji wa shuguli za chama hicho.

Mpango huo wa KNCU (1984) Ltd ulikwama, baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Philemon Ndosi,  kuwaomba wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 37 wa KNCU uliofanyika katika ukumbi wa Coffee Tree Hotel mjini Moshi, kuridhia kupitisha azimio la kukatwa shilingi mia moja kwa kilo moja ya kahawa kutoka vyama vya msingi kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa chama hicho.

Kwa mujibu wa Mwenyekti huyo,amesema  KNCU imedhamiria kutoa huduma bora kwa vyama, hivyo nawaomba mridhie ombi la wakulima kukatwa shilingi mia moja kwa kila kilo moja kwa lengo la  kukamilisha huduma zote kwa vyama vinavyohusika.

Ndosi amesema  kwa sasa  hali ya KNCU ni mbaya hata ulipaji wa mishahara ya wafanyakazi unachangamoto kubwa, lakini yako mambo ambayo wanatarajia kuyafanya na kuwaomba wajumbe wa mkutano huo kuridhia kuipatia KNCU  shilingi mia moja tu kwa kila ya kahawa.

Amesema vyama vya msingi vinaidai KNCU shilingi  Bilioni 1.2 lakini pia KNCU inavidai vyama vya msingi sh bilioni 1, huku akidai kila ukaguzi unapofanyika kupitia  Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini (COASCO) chama hicho kimekuwa kikipewa hati chafu, kutokana na kushindwa kusimama kwenye nafasi yake.

Mwenyekiti huyo akawasilisha ombi kwa wajumbe wamkutano huo mkuu kuomba ridhaa yao ya kuyafuta madeni hayo kwa KNCU kusamehe madeni inayodai kutoka vyama vha msingi vya ushirika na vyama hivyo navyo vifute madeni ambayo vinaidai KNCY ombi ambalo wachama hao walikataa.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa  chama cha ushirika Masama Sawe, Jublethe Ndosi amesema  hoja  ya Mwenyekiti wa KNCU kwamba deni linalofikia bilioni 1.2 lichangiwe kutoka kilo ya kahawa sh mia 100 yeye kama kiongozi anayewawakilisha wanachama wa chama  hawezi kuunga mkono hoja hiyo.

Amesema kama deni lipo na wapo waliosababisha madeni haya ndio wanaotakiwa kutafutwa kote waliko ili walipe madeni hayo na si KNCU kuomba yafutwe bila kueleza ni nani walisababisha madeni hayo kufikia hapo yalipofikia.

Naye Mwenyekiti wa  chama cha ushirika cha Uru Kusini, Everesti Siriwa,  amesema deni hilo linatakiwa  kulipwa na waliosababisha kuwepo kwa deni hilo na kushauri kuvitumia vyombo vya uchunguzi ili wahusika wachukuliwa hatua za kisheria.

Amesema kutokana na madeni yaliyopo  KNCU sio rahisi mtu kuchangia hiyo shilingi 100 kwa ajili ya kufuta madeni, watu wenye madeni wanafahamika kwa nini kunakuwa na kigugumizi cha kuyafuatilia hayo madeni ili waweze kulipwa? alihoji.

Amesema haitawezekana wakulima kubebeshwa mzigo wa kukatwa shilingi 100 kwakila kilo moja ya kahawa  kusaidia uendeshaji wa shughuli za chama hicho bila kuwepo na maelezo ya kutosha juu ya waliohusika kulfikisha deni hapo lilipo.

Mwenyekiti wa chama cha msingi Uru Patrick Ngowi amesema wao kama viongozi wanaowakirisha wanachama  wa vyama vya msingi vya ushirika hawaweza kukubali wanachama wao  kubebeshwa mzigo wa kulipa madeni ambayo hawakushiriki kuyasababisha.

Akizungumza Mwenyekiti wa kikao hicho Martine Mallya, ameitka KNCU kuwafuatilia wadaiwa wote inaowadai, huku akikataa ombi la kufutiwa madeni ambayo inadaiwa na vyama vya msingi vya ushirika.

KNCU (1984) Ltd inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo deni la shilingi bilioni 2.43 ingawa haijawekwa bayana ni taasisi zipi zinaidai.

 

0 Comments:

Post a Comment