Tuesday, July 5, 2022

UCHAGUZI CCM 2022: Makada Moshi Vijijini waweka rekodi ya kuchukuwa fomu za kugombea

 

Ofisi cha Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro

Joto la uchaguzi ngazi ya  Wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro, limezidi kupanda moto, huku idadi  kubwa ya Makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza  kwa wingi kuchukua fomu za kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo pamoja na Jumuiya zake na kuweka rekodi kuelekea katika uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Katika hali isiyoyatarajiwa na wengi, majina ya wanasiasa vigogo na wale wanaochipukia katika medani za siasa yameendelea kutawala katika vinywa vya watu kutokana na kujitokeza kwa wingi, huku idadi kubwa ya wanaowania kuteuliwa na chama hicho katika uchaguzi  huo ndani ya chama hicho ikitajwa kuwa ni kubwa kuliko kawaida.

Katibu wa  CCM Wilaya ya Moshi Vijijini Ramadhana Mahanyu, ameyasema hayo Julai 04,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na mchakato wa uchukuaji fomu ngazi ya wilaya unavyoendelea.

“Kwa wilaya yetu ya Moshi vijijini makada wa CCM wamejitokeza kwa wingi sana katika uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama chetu, uchaguzi huu kama ambavyo mnafahamu tulianza mapema sanatangu mwezi Machi mwaka 2022, ambapo tulianza kwenye mchakato wa ngazi za Mashina, Matawi, Kata na sasa tuko ngazi ya Wilaya watu wamehamasika sana na chaguzi hizi,”amesema Mahanyu.

Amesema kwa upande wa ngazi ya kata kwa sasa chama kipo katika hatua ya kuwachuja wagombea wa nafasi hizo na kwamba  ifikapo Agosti 3 mwaka huu watakwenda kwenye uchaguzi ngazi ya Kata.

Amesema nafasi zote tulizozitangaza makada wa CCM wamejitokeza kuchukua fomu na zote zimepata wagombea,

Amesema ziko nafasi mbalimbali za kuomba kugombea  ikiwemo nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya, nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi, nafasi ya mkutano mkuu wa Taifa, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya , kundi la Vijana, na kundi la Wanawake, ambapo makada wengi wamejitokeza kuomba nafasi hizo.

Katika hatua nyingine Mahanyu ametoa wito kwa watu wanaoishi na ulemavu ambao ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi  (CCM) kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu  ili kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ngazi ya Wilaya na Jumuiya zake.

Aidha amesema watu wenye ulemavu hawana sababu ya kuogopa kuomba nafasi za kuchaguliwa katika uchaguzi  unaoendelea ndani ya chama hicho kuanzia ngazi za Matawi,  Kata na Wilaya kwani wana haki sawa ya kushiriki katika kuchagua au kuchaguliwa sawasawa na watu wengine wasio na ulemavu.

Majina hayo yanahusisha wasomi wa vyuo vikuu, waandishi wa habari pamoja na kada nyingine wanaendelea kujitokeza wakichukua fomu zinazoendelea kutolewa hadi hapo  dirisha hilo litakapofungwa Julai 10 mwaka huu.


 

0 Comments:

Post a Comment