Friday, July 1, 2022

Mabasi 8 yakamatwa Kilimanjaro yakisafirisha abiria usiku


Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro, limekamata mabasi madogo nane ya abiria kwa makosa mbalimbali likiwemo la kusafirisha abiria nyakati za usiku.

Kamishna Msaidizi wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro (ACP) Simon Maigwa, alisema kuwa mabasi hayo yalikamatwa wilayani Mwanga baada ya kufanya Operesheni ya kushtukiza katika eneo la kizuizi kilichopo wilayani humo katika barabara kuu ya Arusha-Dar es Salaam.

Kamanda Maigwa alisema ipo tabia ya baadhi ya madereva wa mabasi madogo aina ya (Coaster) ambao kwa jina maarufu “hakuna kulala” hususan katika mkoa wa Kilimanjaro kukiuka sheria za usalama barabarani kwa kusafirisha abiria nyakati za usiku kwa kisingizo kwamba wametoka kupeleka msiba.

Kamanda Maigwa alisema baada ya kuyakagua mabasi hayo walikuta yamekiuka sheria, kwa kutokuwa na kibali cha kusafirisha abiria usiku huku mengine yakionekana kuwa na hitilafu kwenye mfumo wa break.

"Magari haya yamekuwa na tabia ya kupakiwa nyakati za mchana na inapofika usiku huanza safari ya kusafirisha abiria, tayari madereva wa mabasi hayo tumeshawafikishwa mahakamani,"alisema ACP Maigwa.

ACP Maigwa, ametoa onyo kali kwa wamiliki wa vyombo vya moto na madereva  ambao wataendelea kukaidi, Jeshi la polisi halitasita kuwachukulia hatua za kisheria watu hao.

0 Comments:

Post a Comment