Thursday, July 14, 2022

Kanali Mstaafu Lubinga: Mapigano mashariki wa DRC yanachochewa na mataifa makubwa

Mapigano makali yanayoendelea kwa muda mrefu sasa mashariki na kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baina ya makundi mbalimbali ya waasi dhidi ya majeshi ya serikali yanachochewa na maslahi ya mataifa yaliyoendelea duniani imeelezwa.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari hivi karibuni mkoani Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga alisema Wakongo wanauana wenyewe kwa wenyewe pasipo kutambua kuwa wanafanya kwa maslahi ya wachache.

“Hivi mnajua Kongo ile vita siyo ya Wakongo pamoja na Wakongo wanauana? Watu wametengeneza pale mahali pa kuchukulia...” alisema Kanali Mstaafu huyo.

Kanali Mstaafu Lubinga ambaye hakuyataja moja kwa moja mataifa hayo alibainisha kuwa katika bara la Afrika misitu ya Kongo ni tajiri kwa kila kitu hivyo mataifa ya nje yamekuwa yakitolea macho utajiri huo.

“Hakuna nchi tajiri Afrika kama Kongo, pale Kongo vita haviishi. Hakuna nchi Afrika yenye mbao duniani kama Kongo. Hakuna watu wenye asali nzuri duniani kama asali iliyoko Kongo kwenye misitu  na hakuna watu wenye senene nzuri zinakotoka zaidi ya Kongo….haya ndiyo yao. Vita hii inatengenezwa,” alisema Lubinga.

Aidha Lubinga alisema viwanda vya silaha duniani vimekuwa sababu ya kuinua uchumi wa nchi husika kuliko viwanda vya pembejeo za kilimo.

“Niwaeleze, dunia ya leo vita vimebadilika vimekuwa na faida kubwa kuliko…wanasema viwanda vya silaha … viwanda vya kuzalisha bidhaa za kijeshi vina faida kuliko viwanda vinavyozalisha bidhaa za kawaida,” alisisitiza Lubinga.

Mmajumuhi huyo wa Afrika aliongeza, “ Wewe shati ukilinunua unasubiri pasaka au krismasi…lakini dunia ya leo inapigana vita; buti vifungo…vyote vinatengenezwa askari waende vitani. Kifaru hakikai , lakini trekta inakaa miaka 20 sasa utapataje faida kwenye kitu kinachokaa miaka 20? Kwa hiyo wanatengeneza vurugu ili kuinua Uchumi wao.”

Majuma kadhaa yaliyopita mvutano uliongezeka na nchi jirani ya Rwanda tangu mashambulizi ya M23 yalipoongezeka mashariki mwa nchi hiyo. Mnamo Juni 5, Rais wa DRC Félix Tshisekedi alisema "hana shaka" juu ya uungaji mkono wa Rwanda kwa waasi ambao walikuja "kushambulia" nchi yake, madai ambayo Kigali inakanusha.

Ukizungumzia M23, inawakumbusha wengi kuwahusu watu kama Sultani Makenga na wengine kama Bosco Ntaganda, huku wengine wakirudi nyuma na kumkumbuka Laurent Nkunda.

Tangu mwaka 2004, Jenerali Nkunda amejiondoa katika jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na wanajeshi wake katika vilima vya Rutshuru na kuunda CNDP, ambayo imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali na mji wa Goma.

Wote watatu walikuwa wanachama wa waasi wa zamani wa APR waliochukua mamlaka nchini Rwanda mwaka 1994, kabla ya kuendeleza vita vyao nchini DR Congo mwishoni mwa miaka ya 1990.

Nkunda alikamatwa nchini Rwanda mapema mwaka 2009 na kufungwa, huku CNDP ikiongozwa na Ntaganda ikijadiliana na serikali ya Kabila katika makubaliano ya Machi 23, 2009.

Miaka minne baada ya kusitishwa kwa mapigano, kundi la watu wanaojiita wapiganaji wa M23 lilizaliwa mwaka 2012, likiongozwa na Ntaganda na Makenga, ambao wanasema makubaliano ya serikali na CNDP Machi 23 hayajafuatwa.


Katibu wa NEC na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga 


0 Comments:

Post a Comment