Thursday, July 21, 2022

Ithibati ya Kimataifa Hospitali ya Kibong'oto mkombozi kwa Watanzania

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali Maalum ya Afya ya Jamii na Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto Dkt. Leonard Subi  
Hospitali Maalum ya Afya ya Jamii na Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto, Siha mkoani Kilimanjaro imejizolea ithibati nne za kimataifa hatua ambayo itakuwa mkombozi kwa watanzania waliokuwa wakipeleka sampuli zao nje ya nchi kwa ajili ya kuzichakata.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo Dkt. Leonard Subi alisema hatua ambayo makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufungua Maabara ya Kisasa hospitalini hapo ni ukombozi kwa watanzania waliokuwa wakienda nje ya nchi kupeleka sampuli za magonjwa ambukizi  kwa ajili ya kuzichakata.

“Hautapeleka sampuli nje, kwa mfano uliyokuwa ukipeleka nje kwa shilingi laki moja sasa unaweza kupata kwa shilingi elfu arobaini au elfu hamsini ndani ya nchi bila usumbufu kwasababu huduma kama hiyo inafanyika hapa Kibong’oto,” alisema Dkt. Subi.

Dkt. Subi alisema uchunguzi wa magonjwa ya ini, figo, moyo yatakuwa yakifanyika katika hospitali hiyo ya Afya ya Jamii.

“Mimi na wataalamu wenzangu tumeweza kupata ithibati nyingine ya kimataifa kutoka vipimo vinne hadi 28, kwa maana sasa majibu tutakayokuwa tunayatoa Kibong’oto katika eneo la Kemia Uhai yatakuwa yanatambulika kimataifa,” alisema Dkt. Subi

Aidha Dkt. Subi alisema ithibati nyingine wameipata katika eneo la seololojia ikiwa na maana ya kuangalia kinga za mwili.

“Kama mnavyofahamu unapochukua damu ukizungusha kidogo utaona majimaji yanayobaki juu, hayo ni kinga ya mwili, na penyewe tumepata ithibati,” alisema.

Hospitali ya Kibong’oto imepata ithibati ya tatu katika uchunguzi wa kifua kikuu cha kawaida na kifua kikuu sugu.

Dkt. Subi aliongeza, “Pia tumepata ithibati ya kimataifa katika uchunguzi wa sampuli za magonjwa yoyote yanayosababishwa na vimelea aina ya protozoa kwa maana ya parasaitoloji au vidudu vingine vya parasaitoloji vinavyosababisha maradhi kama malaria.”

Hospitali hiyo ya maalum ya Kibong’oto imepata ithibati nyingine katika uchunguzi wa vijidudu vidogo vidogo hususani kwenye uoteshaji na kuvichakata kwa maana ya microbaolojia.

“Tumemuahidi Makamu wa Rais (Dkt. Philip Mpango) kuwa vipimo vyote vinavyotolewa katika hospitali hii vinapata ithibati ya kimataifa,” alisisitiza Dkt. Subi.

Julai 16, 2022 Makamu wa Rais Dkt. Mpango alifungua jengo jipya la kisasa la Maabara katika Hospitali Maalum Kibong’oto ambapo wataalamu hospitalini hapo watajikita kuangalia vimelea na kufuatilia magonjwa ya kuambukiza nchini na ulimwengu kwa ujumla.




1 comment:

  1. Hakika watanzania tuna Jambo la kujivunia

    ReplyDelete