Wakazi wa Kijiji cha Uchira, wilayani Moshi wakitoa heshima
zao za mwisho kwa marehemu Yohana Laizer (30) aliyeuawa kwa kudhaniwa kuwa ni mwizi (Picha na Kija
Elias).
Wahenga
walisema “Ukistaajabu ya Musa, utayaona ya Firauni”, ndivyo unavyoweza kusema
katika tukio la Mmasai mmoja kuuawa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni katika
harakati za kudai fedha yake iliyobaki (chenji) baada ya kula chipsi za
shilingi 2500.
Kijana mjasiriamali anayefahamika kwa jina la Yohana Laizer (30) mkazi wa Uchira wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro ameuawa kwa kipigo kutoka kwa walinzi wa baa moja iliyopo karibu na soko la Uchira akidhaniwa kuwa ni mwizi.
Ilikua hivi, usiku wa Julai 13, 2022 majira ya saa nane usiku walinzi hao walimkamata Laizer na kuanza kumpa kipigo na kwa madai ya kuwa ni mwizi na baadaye kumtembeza katika maeneo ya kijiji huku mwili wake ukiwa umetapakaa damu hatimaye kumtelekeza pembezoni mwa barabara kuu ya Moshi –Arusha.
Laizer ambaye alikuwa mbebaji wa mizigo ‘Kibega’ katika soko la Uchira inadaiwa majira ya mchana wa Julai 13 alikwenda katika baa hiyo ambayo hukaanga na kuuza chipsi, aliagiza kiasi cha kumtosha cha shilingi 2500, hatimaye alitoa shilingi 10,000.
Baada ya kutoa kiasi hicho cha fedha aliambiwa na muuzaji wa chipsi kuwa hana fedha ya kumrudishia (chenji) hivyo aje baadaye kuchukua kiasi cha fedha kilichobaki.
Mashuhuda
wa tukio hilo walisema, marehemu kwasababu alikuwa akifahamika na sio mara yake
ya kwanza kwenda kula hapo aliondoka akitarajia baadaye aje achukue kiasi cha
fedha kilichobaki.
Hata hivyo marehemu alirudi usiku baada ya kumaliza kazi zake za kujitafutia kipato na kwenda kwa muuzaji wa chipsi akiwa na matumaini ya kuchukua kiasi cha fedha kilichobaki, lakini hali haikuwa hivyo.
Shuhuda mmoja (jina tunalihifadhi), alisema marehemu alipohitaji kiasi cha fedha kilichobaki aligeuziwa kibao kuwa hakuna fedha yoyote aliyoiacha baada ya kula chipsi
“Mzozo uliibuka baina yao, ambapo muuza chipsi alimgeuzia kibao, na kuanza kupiga kelele za mwizi ambapo watu wasiojulikana wakimo walinzi walimtoa nje na kuanza kumpa kipondo,” alisema shuhuda huyo.
Hata hivyo inadaiwa kuwa mzozo huo uliendelea mpaka majira ya usiku ambapo mashuhuda walidai walinzi wa baa hiyo wanahusika moja kwa moja na mauaji ya kijana huyo.
"Walifika karibu na nyumbani kwangu majira ya saa nane, saa tisa usiku hivi, watu waliposikia makelele walikuja tulifungua mlango tukawakuta vijana waliokua wanampiga marehemu kisha wakamuuliza marehemu Said uliyekuwa naye ndiye huyu, marehemu alikataa na kusema sikuwa na Said, msinilazimishe nimtaje mtu wakati sikuwa naye, alipowajibu hivyo ndipo waliendelea kumpa kipigo, "alisema shuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Said Msangi.
Shuhuda huyo alisema baada ya marehemu kukataa kumtaja aliyekuwa naye aliwataka vijana waliokuwa wanampiga marehemu kumchukua na kuondoka naye kwani marehemu alikuwa tayari ameishiwa nguvu.
"Niliwaambia waondoke na mtu wao maana walinikuta nyumbani na familia yangu, wakamchukua na kumtembeza kwenye baadhi ya maeneo na kisha wakamtelekeza barabara kuu, ambapo asubuhi tuliukuta mwili wake pembezoni mwa barabara, hakuna aliyemgusa hadi Polisi walipokuja kuchukua," alisema Msangi.
Elizabeth Kimario, mkazi wa kijiji hicho alionyesha kushangazwa na mauaji hayo kutokana na kijana huyo kutokuwa na historia ya udokozi katika kazi zake za ujasiriamali sokoni hapo.
"Tulishangaa kusikia kuwa alipigwa na ameuwawa kwasababu kaiba lakini hatujawahi kusikia kama ana tabia ya wizi, hajawahi kuiba kitu cha mtu, alikuwa mwaminifu maana anaweza kupewa laki mbili hadi tatu akanunue mizigo ya watu ya dukani, hata siku moja hatujawahi kusikia tukio lake la wizi hapa mtaani," alisema Kimario.
Mwili wa marehemu ulichukuliwa na jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro mnamo Julai 14, 2022 na kuhifadhiwa katika hospitali ya KCMC kwa uchunguzi zaidi.
Ndugu wa marehemu kutoka Ngage Simanjiro mkoani Manyara walipata taarifa za kifo cha ndugu yao Julai 15, 2022 na kufunga safari kwa ajili ya kujua sababu za kifo cha kijana wao.
Msemaji wa familia hiyo, Saitoti Karuduni alisema kuwa familia imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha ndugu yao ambaye amekatishwa uhai wake na kuiomba serikali kulivalia njuga suala la watu kujichukulia sheria mkononi .
" Leo hii ameuawa ndugu yangu, serikali isipolivalia njuga kesho atauwawa mwingine asiye na hatia, niombe sana vyombo vya ulinzi na usalama vichukue hatua ili waliokatisha uhai wa ndugu yetu waweze kupatikana" alisema Saitoti.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Julius mkojera alisema kuwa kilichofanyika kukatisha uhai wa Laizer ni ukatili ambao umepelekea watu kujichukulia sheria mkononi.
Aliongeza kuwa iwapo kijana Laizer alikua amefanya uhalifu wowote ilipaswa kupelekwa kwenye ofisi ya serikali ili hatua za kisheria zichukuliwe lakini sio kuchukua sheria Mkononi.
"Napenda kumwambia kuwa serikali ina mkono mrefu sana, hivyo kwa waliohusika tuwaachie mahakama na polisi waendelee na uchunguzi wao ili haki ya ndugu yetu Yohana iweze kupatikana"
Akiongoza ibada ya kuuaga mwili wa kijana huyo Mchungaji wa Kanisa la Uamsho, Uchira Meshack Karani ameitaka jamii kuwa na hofu ya Mungu na kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani hatua hiyo ni hatari na haimpendezi Mungu.
"Sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, hatupaswi kuchukua sheria Mkononi, ipo serikali, vipo vyombo vya ulinzi na Usalama, tuviache vifanye kazi yake, Tupendane pia, upendo ungekuwepo leo hii tusingekatisha uhai wa kijana huyu asiye na hatia.
Wahenga
hawakukaa kimya “Mla kuku wa mwenziwe miguu humwelekea” ndivyo Jeshi la Polisi
mkoani Kilimanjaro kupitia Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (ACP) Simon Maigwa alithibitisha kuwakamata watu
ambao hakutaja idadi yake kuhusika na mauaji ya Mmasai huyo kwa ajili ya hatua
zaidi za kisheria.
Mchungaji wa Kanisa
la Uamsho, Meshack Karani, akiongoza ibada ya kuuaga mwili wa Yohana Laizer (30) aliyeuawa kwa kudhaniwa kuwa mwizi.
(Picha na Kija Elias).
0 Comments:
Post a Comment