Madiwani wa
halmashauri zote mkoani Kilimanjaro wamepigwa msasa wa kazi yao kwa wananchi
waliowapigia kura huku wakitakiwa kutunza familia zao vizuri.
Akizungumza
katika semina ya siku moja iliyofanyika katika makao makuu ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro Katibu wa NEC na Uhusiano wa Kimataifa Kanali
Mstaafu Ngemela Lubinga alisema madiwani wanatakiwa kujitambua
“ Madiwani
mnatakiwa kujua hitajio la jamii…ambalo ni kujenga jamii yenye usawa,
kuheshimiana na haya yote hayawezi kufanyika kama nyinyi wenyewe hamjijui,”
alisema Lubinga.
Lubinga
alisema madiwani wana dhamana kubwa kwani maendeleo ya nchi yapo mikononi mwao,
utulivu na amani katika maeneo yao ni muhimu kuzingatia.
Aidha Kanali
huyo Mstaafu aliwataka madiwani hao kutambua kuwa wakitimiza wajibu wao kwenye
familia zao hata jamii wanayoiongoza itakuwa
na maendeleo ya kweli.
“Diwani ni
lazima uwe mvumilivu, kuwa kiongozi wa kisiasa sio tafrija, ni lazima uwe
mvumilivu na muungwana kwa kila mtu; walio wengi familia hatuzijali na wengine
walipopata udiwani walihama na nyumbani,” aliongeza Lubinga.
Kanali
Mstaafu Lubinga aliongeza, “ Sio kuku wanapotea kijijini, wanasema nenda pale
kwa diwani ana watoto wanaoiba kuku… nanyi kina mama mlipopata udiwani
hakikisha kiatu cha mumeo hakijachubuka akitoka waseme yule ni mume wa diwani,”
Pia Lubinga alisisitiza
ugomvi baina ya mke na mume ndani ya nyumba sio mzuri huku akitaka usiri mkubwa
pindi inapotokea mitafaruku baina yao ili kulinda dhamana ya uongozi waliopewa.
“Tutofautishe
nguo ya kuanika ndani na ya kuanika nje…hakuna jamii yoyote duniani isiyo na
siri; chutama kwenye mambo ambayo hutaki kila mmoja ajue, sio kila kitu kwako
kionekane kwa mtu. Ukila nawe mdomo,” alikumbusha Lubinga.
Hata hivyo Kanali
Mstaafu Lubinga aliwataka madiwani hao kwenda mbali zaidi katika utunzaji wa
siri ikiwamo vikao vya ndani ya chama.
“Mmemaliza
kamati ya madiwani watu wanawasubiri kijiweni. Na wakikupa bia mbili basi tena
unasukumwa…unabinuka, ukisukumwa usibinuke wewe una dhamana. Siri ndio
inayojenga jamii bora,” alisema Lubinga.
Kwa upande
wao madiwani walipongeza juhudi za chama chao kuwapa semina kwani kuna baadhi
ya mambo walikuwa hawayajui na kuanza hapo wamepiga hatua muhimu katika ujenzi
wa chama chao na jamii kwa ujumla.
Awali katika ufunguzi wa semina hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi alisema licha ya changamoto kujitokeza tangu uchaguzi wa 2020 lakini madiwani hao wamekuwa waaminifu katika kutenda haki kwa kila mmoja kwa kadiri inavyotakiwa.
0 Comments:
Post a Comment