Lions Club Moshi Kibo mkoani Kilimanjaro imefadhili ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi kwa wenye uhitaji maalum ambacho kimegharimu kiasi cha shilingi mil. 700
Akizungumza hivi karibuni Mwenyekiti wa Lions Club Moshi Kibo Sarah Mandara Jones alisema ujenzi wa chuo hicho umekamilika na wapo mbioni kukikabidhi kwa wahusika ili kufikia malengo ya kuwasaidia watoto wenye uhitaji maalum.
“Kwa sasa Vocational Training Centre imetugharimu zaidi ya shilingi mil. 700 ambapo katika fedha hizo Lions Club International imetupa dola za kimarekani 95,000 na asilimia nyingine imechangiwa na partners wetu wa Belgium,” alisema Sara Mandara Jones
Aidha mwenyekiti huyo alisema jamii inatakiwa kuangalia jamii yenye uhitaji na kuweza kuwapatia misaada mbalimbali ambayo itakuwa endelevu ili kujenga jamii inayoweza kujitegemea.
“Jambo kubwa ambalo wanatakiwa watarajie ni kuweza kuangalia jamii yenye uhitaji na kuwapatia misaada endelevu ili waweze kufanya mambo yao wenyewe bila kuwa na utegemezi katika taifa,” alisema.
Hata hivyo Sarah Mandara Jones aliweka bayana kuhusu kuwanyanyapaa kwa kuwaficha wenye mahitaji maalum hususani wenye uoni hafifu.
Mwenyekiti wa Lions Club Moshi Kibo, Sarah Mandara Jones
“Watoto wanaozaliwa na ulemavu sio jambo la aibu ni Mwenyezi Mungu ameweka kwao lakini tujue kwamba Mwenyezi Mungu ana makusudi na kila kiumbe …ni bora tuwatoe tuwalete shule, tuwapeleke kwenye hatua mbalimbali ambazo wanaweza wakafundishwa ,” alisisitiza.
Kwa upande wake Katibu wa Lions Club Moshi Kibo Inderjeet Rehan ‘Nitu’ alisema, “Malengo yake (kuanzisha chuo cha ufundi stadi) hasa ni kuwezesha vijana wetu wanaomaliza darasa la saba waweze kuishi maisha mazuri baada ya kumaliza mafunzo ya chuo.”
“Tumegundua watoto hususani wa kike wanapomaliza darasa la saba wengine wanatupwa, wanapata ujauzito kuepukana mambo haya tukaona tuwawezeshe wapate elimu waweze kujiendeleza bila kutegemea watu na wasiaibike,” aliongeza Nitu.
Lions Clubs ilianzishwa mnamo mwaka 1917 kwa miaka mingi sasa imekuwa ikijishughulisha na watu wenye uhitaji maalum hususani uoni hafifu kwa kujitolea misaada ya aina mbalimbali kwa jamii tofauti ulimwenguni kwa miradi ikiwamo kuanzisha vyuo vya ufundi stadi kuwawezesha wenye changamoto hizo.
0 Comments:
Post a Comment