Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI) imetengewa fedha
zaidi ya Shilingi milioni 800 zitakazotumika kuboresha utafiti wa
kahawa nchini kwa nia ya kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa nchini kwa
ujumla.
Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, aliyabainisha hayo
katikati ya wiki wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi za
TaCRI zilizoko Lyamungo Wilayani Hai mmkoani Kilimanjaro.
“Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa sasa imeegemea kwenye
Sayansi na hii ni kwa sababu ya utafiti ukiwemo ule wa zao la
Kahawa, ambayo ndio njia pekee itakayoboresha kilimo nchini na kwamba mgao wa
fedha hizi ni ongezeko kutoka mgao wa awali wa zaidi ya milioni 300,”alisema
Mavunde.
Alisema “Matarajio yetu ni kwamba TaCRI itapata watafiti wengi
zaidi na wengine kwenda kupata utaalamu wa ziada iwe ndani au nje ya nchi ili
wakulima wetu waweze kuzalisha zaidi; serikali itaendelea kuwekeza katika eneo
hili la utafiti”, aliongeza.
Aidha Mavunde aliendelea kusema kuwa ongezeko la fedha za
utafiti kwa TaCRI ni sehemu ya bajeti ya ziada kwa ajili ya utafiti ndani ya
Wizara ya Kilimo katika mwaka huu wa fedha ambapo alisema bajeti ya jumla ya
utafiti ndani ya wizara hiyo imeongezwa kutoka shilingi bilioni
11. mwaka 2021/2022 hadi kufikia kiasi cha shilingi
bilioni 39.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TaCRI (EDR), Dk. Deusdedit
Kilambo alisema Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine inalenga
kutekeleza agizo la Serikali la kuzalisha zaidi ya miche milioni 20 ya kahawa
ambayo itasambazwa kwa wakulima na baadaye kuongeza uzalishaji wa kahawa
nchini.
“Mikakati iliyopo ambayo itatuwezesha kufikia azma hiyo ni
pamoja na kuwekeza katika maeneo mapya ya uzalishaji wa kahawa ambayo yameainishwa
na wataalamu kama Sirari mkoani Mara pamoja na Mkoa wa Morogoro”, alisema.
Kuhusu uzalishaji wa milioni 20 kwa ajili ya miche ya Arabika na
Robusta kama ilivyoelekezwa na Serikali, Dk. Kilambo alisema kuwa taasisi hiyo
iko tayari kutekeleza agizo hilo, ambapo aliishukuru Serikali kwa kutenga fedha
zaidi kwa ajili ya bajeti ya taasisi hiyo.
“Kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB),
nakuhakikishia Naibu Waziri kuwa tutafikia lengo la kuzalisha zaidi ya miche
milioni 20 bila shaka yoyote kuanzia mwaka 2022/2023”, alisema.
0 Comments:
Post a Comment