Vyuo vya Ufundi Stadi nchini (VETA) vimetakiwa kuendelea
kuhakikisha vijana wanaoingia katika mafunzo hayo wanapata ujuzi na maarifa
katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Akizungumza katika Mahafali ya Pili ya kuanzishwa kwa Programu
hiyo ya “Make A Difference Now” Mdhibiti wa Ubora wa Shule Kanda ya
Kaskazini Exaud Mtei alisema kujiajiri ndio mpango mzima kwa vijana
wakishahitimu masomo yao lakini hawawezi kujiajiri kama hawana ujuzi wa Tehama
katika zama za utandawazi.
“Tunasisitiza sana katika elimu wanayopewa vijana waweze
kuangalia zaidi katika masuala ya ujuzi , Veta inatakiwa kuhakikisha kwamba
inajikita zaidi katika kuboresha vyuo vya Ufundi na vile ambavyo vinatoa ujuzi
hasa katika masuala mazima ya Tehama ili vijana waweze kupata elimu ya Tehama,”
alisema Mtei.
Mtei aliongeza kuwa katika taasisi mbalimbali haiwezekani
kufanya kazi bila kuwa na ujuzi wa kompyuta na Tehama kwa ujumla.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Njoro kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Rashid Gembe, Florian
Mutashobya aliipongeza Taasisi ya Make kwa kuwafadhili wasichana 26 ili kuweza
kupata mafunzo ya komyuta pamoja na ujasiriamali kwa muda wa miezi minne.
“Elimu waliyoipata itawawezesha katika maisha yao ya
kujitegemea na imesaidia kuwapunguzia mzigo wazazi wao kuwategemea,”
alisema Mutashobya.
Hata hivyo Mutashobya aliwasihi wahitimu hao kwenda kuangalia
fursa zilizoko vijijini na kuweza kuzichangamkia kwani maeneo mengi ya
yanakabiliwa na changamoto kubwa ya wataalamu wa masuala ya Tehama.
Aidha Mkurugenzi wa Taasisi ya Affordable Computers And
Technology For Tanzania (Actt) Robert Mafie alisema taasisi yake imejikita
zaidi kuwasaidia kusaidia vijana wa kike ili waweze kufikia malengo,
kuwasaidia katika masomo ya ujasiariamali ili kuepukana na changamoto za mimba
za utotoni.
“Tangu kuanzishwa kwa (Actt) mwaka 2011 hadi sasa tumeshazifikia
shule zaidi ya 400 Kwa ajili ya kuzisaidia kuwapatia kompyuta na vifaa vyake ,
kutoa mafunzo ya kompyuta na teknolojia katika kuboresha elimu,” alisema Mafie.
Baadhi ya wahitimu Mwanaidi Athuman na Hiyari Hemedi
wameishukuru kwa Make Kwa ufadhili wao, ambao wameweza kupata elimu ya
ujasiariamali na ujuzi wa kusoma masoko ya kompyuta ambapo wazazi wao hawakuwa
na uwezo wa kuwasomeaha kutokana na changamoto ya kifedha.
0 Comments:
Post a Comment