Tuesday, July 5, 2022

NDELE SOLOMON: Nyota wa soka anayevutiwa na utendaji wa Samatta

 

Ndele Solomon akiwa na Endumet FC

Maya Angelou alikuwa mshairi wa Marekani, mwandishi wa kumbukumbu, na mwanaharakati wa haki za kiraia.

Alichapisha tawasifu saba, vitabu vitatu vya insha, vitabu kadhaa vya mashairi, na anasifika kwa orodha ya michezo, sinema, na vipindi vya televisheni vilivyochukua zaidi ya miaka 50.

Mzaliwa huyo wa St. Louis huko Missouri amekuwa mtu wa kufuatiliwa na watu mbalimbali katika kazi zake, miongoni mwa nukuu zake alisema.

“Nimejifunza kuwa watu wanaweza kusahau ulichosema, watu wanaweza kusahau ulichofanya lakini watu hawawezi kukusahu namna ulivyowafanya wajisikie.”

Ni kweli kwamba huwezi kujifunza kila kitu kutoka shule, kutoka mtandao au kutoka maktaba. Wakati mwingine njia pekee ya kusonga mbele ni kujifunza moja kwa moja kutoka kwa mtu anayejua.

Hili lina ukweli ndani yake kwa nyota wa soka anawatumikia mabingwa wa soka wilaya ya Siha msimu wa mwaka 2021/2022 Endumet FC.

Nyota huyo anayefahamika kwa jina la Ndele Solomon mkazi wa Kijiji cha Matadi anasema, “Katika maisha yangu ya soka nimekuwa nikijifunza sana kwa kepteni wetu wa Taifa Stars Mbwana Samatta kwa namna anavyopambana katika soka lake na nimekuwa nikimfuatilia kwa karibu.”

Ndele aliyezaliwa Novemba 18, 1994 na kusoma elimu yake ya msingi katika shule ya Lemosho na baadaye shule ya sekondari ya Matadi zote za wilayani Siha anaongeza,

“Wengine wanaweza wasimwelewe Samatta, lakini juhudi na kujipambana na watu wenye nia njema waliokuwa wakimwongoza imekuwa chachu ya mafanikio yake hadi sasa anacheza soka la Ulaya.”

Ndele anasema Samatta ni nahodha mzuri katika kikosi cha Taifa Stars, sio mvivu na amekuwa na upendo wa dhati kwa kila mchezaji ambao umekuwa na hamasa kubwa kwa watanzania.

“Ninapomuona anapokuwa uwanjani, najisikia vizuri, amekuwa kepteni mzuri mfano wa kuigwa hata kama Taifa Stars inafungwa, upendo ndio kila kitu katika maisha yake,” anasema Ndele.

Ndele alianza kuhudumu na klabu ya Mawenzi ambako alitwaa Kombe la Sandewa mnamo mwaka 2010 na miaka mine baadaye alitwaa  Kombe la Kiazi.

Mnamo mwaka 2016 Ndele alichukuliwa na timu iliyotisha sana mkoani Kilimanjaro ya Forest ambako misimu miwili mfululizo (2017/18, 2018/19) walitwaa mataji ya wilaya na kwenda katika fainali za mabingwa wa wilaya wakiambulia nafasi ya pili.

Baada ya kuhudumu na Forest, nyota huyo ambaye ni mahiri katika safu ya ushambuliaji na ulinzi alichukuliwa na Endumet FC tangu msimu wa 2020/21.

Akiwa na Endumet ametwaa manne yakiwamo Kombe la Wilaya msimu wa 2021/2022 na Highlands 2022 ambapo kwa sasa anajiandaa kwenda katika Ligi ya Mabingwa mkoa wa Kilimanjaro.

 


 

0 Comments:

Post a Comment