Lions Club Moshi Kibo imekabidhi jengo la Chuo cha Ufundi Stadi katika Shule ya Viziwi ya Msandaka hivyo kuweka ya kwanza Tanzania kwa shule za msingi mahitaji maalum kuwa na chuo cha ufundi stadi.
Ufunguzi wa Chuo hicho cha ufundi stadi ulifanywa na Mkurugenzi wa Elimu Mahitaji Maalum Tanzania Dkt. Magreth Matonya.
Katika hotuba yake Dkt. Matonya aliwashukuru wahisani kwa mchango mkubwa walioutoa kufanikisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Msandaka.
“Tumekuta hapa wanajifunza ufundi cherehani, wanajifunza ufundi seremala, tumeona wanatengeneza viti vizuri, stuli nzuri lakini wana vifaa vya kisasa ambavyo wamepewa na wahisani kutoka Lions Club International, kituo hiki ni muhimu sana,” alisema Dkt. Matonya.
Aidha Dkt. Matonya alisema uwepo wa Chuo hicho kilichojengwa kwa zaidi ya shilingi mil. 700 utaifungua jamii kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Awali mratibu wa Viziwi Tanzania Selemani Chamshama alisema miaka ya hivi karibuni mtazamo wa jamii kuhusu wanafunzi wenye uhitaji maalum umebadilika na kuwa chanya ukilinganisha na miaka mingi iliyopita.
“Chuo hiki ni adimu kwa nchi yetu. Kama mnavyokumbuka miaka ya nyuma jamii ilikuwa haina uelewa mkubwa juu ya wanafunzi viziwi lakini sasa kumekuwa na uelewa mkubwa juu ya wanafunzi wenye ulemavu hususani viziwi,” alisema Chamshama.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Rashid Gembe alisema haikuwa kazi rahisi kupatikana kwa chuo hicho cha ufundi stadi Msandaka.
“Shule hii ilipata usajili baada ya kupitia changamoto mbalimbali na kuwezesha kuzitatua. Ofisi ya Mkurugenzi (Manispaa ya Moshi) inatoa shukrani za dhati kwa ufadhili mkubwa kutoka Lions Club Moshi kwa kushirikiana na wadau wengine kuwa na wazo la kujenga chuo cha ufundi,” alisema Gembe.
Aidha Gavana wa Wilaya wa Lions Club aliyepo Tanzania Mustansir GhulamHussein alitoa shukrani zake za dhati kwa Lions Club wa Ubelgiji kwa kufanikisha ujenzi wa chuo hicho.
“Ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kutuunga mkono, Pamoja tumesimama na Pamoja tumeuungana…ndoto tuliyoota pamoja sasa imekuwa halisi,” alisema GhulamHussein.
Hata hivyo Profesa Jerome Sheridan kutoka Ubelgiji alisema elimu ndiyo kitu muhimu cha kuwasaidia wenye mahitaji maalum kutokana na changamoto wanazopitia.
“Ndugu wanafunzi, chuo chenu cha ufundi stadi sasa ni halisi. Kwanini tumefanya hivi? Kwasababu tuna imani nanyi…licha ya changamoto lakini mnaweza kuzikabili endapo mtasoma katika chuo hiki,” alisema.
Aidha Profesa Sheridan alisisitiza kuwa chuo cha ufundi Stadi Msandaka kitaenda mbali zaidi ya kujihusisha na kilimo ili kuwajengea uwezo zaidi wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“Kilimo ni muhimu lakini chuo hiki cha ufundi kitaenda mbali zaidi ya kilimo kwa kuwapatia ujuzi mwingine ili wajitegemee katika maisha yao,” alisema Prof. Jerome
Mbali na hilo Mkuu wa shule ya Viziwi Msandaka Rosada Shayo alisema sababu kubwa ya kuanzisha ujenzi wa chuo hicho ni baada ya kubaini kuwa wanafunzi wao wanapomaliza shule ya msingi na kujiunga na sekondari wanapofika kidato cha pili hurudishwa nyumbani kutokana na matokeo mabaya hivyo kuangukia tena katika changamoto.
Mwenyekiti wa Lions Club Moshi Kibo Sarah Mandara Jones na Katibu wake Inderjeet Rehal walitoa shukrani zao kwa wote walioshiriki kufikia mafanikio hayo.
“Asante sana kwa kile mlichofanya kwa ajili ya Msandaka; mtakumbukwa kwa miaka mingi ijayo, katika historia ya Msandaka majina yenu siku zote yatakuwa yakiandikwa. Asante sana.”
MORE PHOTOS OF THE EVENT CLICK HERE: MSANDAKA VTC