Saturday, June 15, 2019

Umasikini chanzo kikubwa cha ukatili wa watoto Moshi

“Watoto wenye ulemavu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na kufanyiwa matukio ya ukatili ikiwamo matukio ya kubakwa na kulawitiwa. Naomba jamii ya watanzania kuwapenda na kuwasaidia ili wafikie malengo yao ya kuwa na maisha bora kama watanzania wengine, kama mnavyojua wengi wanatoka katika familia maskini," Dotto Olafsen.

Imeelezwa umaskini ni sababu kubwa inayochangia kuvunjwa kwa haki za watoto hali ambayo imewafanya wazazi na walezi kukosa muda maalum wa kuwasikiliza watoto katika changamoto na kujikuta wakiingia katika ukatili.

Ukatili huo umesababisha watoto hao kuathirika kimwili, kimaadili au kihisia ikiwemo vipigo, kutukanwa matusi, kubaguliwa, kutojaliwa unyanyasaji wa kingono na utumikishwaji.

Hayo yalizungumzwa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa hiyo Magret Reuben mwishoni mwa wiki iliyopita katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya Majengo iliyopo katika Manispaa ya Moshi kwa ushirikiano kati ya ofisi ya Manispaa ya Moshi na azaki zisizokuwa za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya haki za watoto.

“Kama mnavyojua, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizoadhimisha siku ya mtoto wa Afrika duniani ikiwa na lengo la kumkomboa mtoto kimaisha, matatizo ya ukatili mkoani hapa hasa katika Manispaa ya Moshi yanaonekana kuongezeka kila kukicha, hivyo nawaomba tuendelee kushirikiana kutokomeza hilo…” alisema Magret.

Afisa huyo alizidi kufafanua kuwa, wazazi wengi wamejikita zaidi kwenye uzalishaji ili waweze kuongeza uchumi wao na kusahau wajibu wa malezi na ulinzi wa watoto kitendo kinachowafanya kukosa muda wa kuwalinda watoto wao ili wasikumbwe na athari hizo.

“Matukio mengi ya wazazi kutelekeza watoto wao kwa kutowapatia mahitaji muhimu kama chakula, mavazi na malazi yaliripotiwa katika kipindi cha mwaka 2018/19,” aliongeza Afisa huyo.

Kwa upande wake, Wakili Mwandamizi wa Serikali ambaye pia ni Mwanasheria kutoka ofisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali Tamari Mndeme, alifafanua kwa kutambua umuhimu wa Mahakama za Watoto (Juvenile Court), serikali imetenga mahakama hizo maalumu katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mahakama za watoto ni muhimu sana, ila changamoto kubwa tunayoipata  ni wakati wa kutekeleza vifungu vya adhabu kwa watoto kwani wazazi wenye watoto waliotendewa makosa kama ya ubakaji ama ulawiti hawatuelewi; wengi hutamani kuona mtoto aliyetiwa hatiani akipewa adhabu ya Kifungo cha miaka 30 kama watu wazima ilhali watoto wote wanalindwa na wana haki zao kisheria hata pale inapobainika kuwa wametenda makosa ya jina,” alisema Mndeme.

Akihutubia mamia ya watoto, walimu, wanaharakati wa haki za binadamu kutoka Asasi mbalimbali zisizo za kiraia zinazojihusisha na masuala ya Haki za watoto kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba, Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi (DAS) Angelina Marko alisema, “Elimu kwa watoto ndio imekuwa mada kuu kwa nchi nyingi katika kumuinua mtoto wa Afrika, ambapo wadau hutumia siku hii kutoa nasaha zinazolenga kuhamasisha serikali na mashirika binafsi na yale ya kimataifa kusaidia watoto wa mitaani na wale yatima walioachwa na wazazi wao kutokana na sababu mbalimbali kama vile maambukizi ya virusi vya HIV na ukimwi.”

Marko alitumia nafasi hiyo kuwataka watoto kusoma kwa bidii kuwaenzi watoto wenzao waliouawa kikatili huko Soweto nchini Afrika Kusini wakipigania Haki ya kupata Elimu, huku wakiitumia vyema fursa ya ‘Elimu Bure’ nchini Tanzania chini ya Uongozi wa Rais John Pombe Magufuli.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya Dees Bridal and Entertainment inayojishulighulisha na masuala ya utoaji elimu kwa vijana, wanawake na watoto kwa masuala mbalimbali ya unyanyasaji wa kijinsia mkoani Kilimanjaro, Dotto Olafsen, alisema kwa kutambua umuhimu wa elimu hasa kwa mtoto wa kike, taasisi yake imekuwa ikitoa elimu kuhusu ukatili kwa watoto kupitia sanaa na burudani mbalimbali ikiwemo muziki.

Olafsen aliongeza kuwa, katika kampeni hiyo wamekutana na changamoto mbalimbali ikiwemo kubaini baadhi ya watoto wameshakubuhu katika vitendo vya ngono hali ambayo inawalazimu kutumia nguvu kubwa ya kisaikolojia kuwaondoa.

“Pia katika kampeni yetu hiyo ya kuzuia mimba za utotoni tumegundua kuwa, baadhi ya watoto tayari wameshaathiriwa na tatizo hilo na kuachishwa masomo kwani serikali hairuhusu mwanafunzi aliyezaa kuendelea na masomo, hivyo wito wangu kwa serikali ni kuandaa shule maalumu za kuwasaidia waathirika wa aina hiyo kwani wengi wao hupata Mimba katika mazingira wasiyotarajia kutokana na kutopevuka vyema akili zao,” alisema Olafsen.

“Watoto wenye ulemavu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na kufanyiwa matukio ya ukatili ikiwamo matukio ya kubakwa na kulawitiwa. Naomba jamii ya watanzania kuwapenda na kuwasaidia ili wafikie malengo yao ya kuwa na maisha bora kama watanzania wengine, kama mnavyojua wengi wanatoka katika familia maskini," alisema Olafsen.

Akizungumza kwa niaba ya watoto wengine, mtoto Selina Mushi alisema, “Tunaomba kufikisha kilio chetu kwa serikali na jamii nzima juu ya masuala mbalimbali yanayohusu watoto katika nyanja zote ambazo ni malezi makuzi ,matunzo na usalama wa watoto; tunanyanyasika, tunatoroka majumbani, tunateswa na vipigo pia tunaomba kupatiwa walimu wazuri wa masomo ya sayansi  ili tuweze kuchangia  uchumi wa viwanda ipasavyo.”

Mnamo mwezi Novemba 20, 1989, Uamuzi wa kihistoria ulifikiwa pale viongozi wa dunia waliporidhia mkataba kuhusu haki za mtoto katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa. Tangu kuridhia kwake miaka 27 iliyopita, mkataba huu umevunja rekodi kwa kuwa mkataba wa haki za binadamu uliowahi kuridhiwa na mataifa mengi kuliko yote katika historia.

Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa zilizoridhia mkataba huu katika mwaka 1990. Kwa kufanya hivyo Tanzania ilitambua rasmi kwamba watoto wote wanayo haki ya kuishi na kukua, kupatiwa ulinzi dhidi ya vurugu, matendo mabaya na unyanyasaji, kuheshimiwa kwa mawazo yao na kuzingatiwa kwa maslahi yao katika maamuzi yote yanayohusu ustawi wao.

Mwezi wa Novemba 2009, miaka kumi na tisa baadaye, bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya mtoto ya mwaka 2009, inayozingatia kikamilifu mkataba wa haki za mtoto kulingana na muktadha wa Tanzania pamoja na kuweka mazingira ya kufanikisha kupatikana kwa haki muhimu. 

Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu na umuhimu wa mtoto duniani na maadhimisho haya hufanywa kila Juni 16 tangu ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 kutokana na tukio baya la kuuawa kikatili watoto huko Soweto nchini Afrika Kusini wakidai haki yao ya kupata elimu bila ubaguzi wowote.

FEATURING STORY BY: Kija Elias
EDITED BY: Jabir Johnson




0 Comments:

Post a Comment