Monday, June 17, 2019

Madiwani Moshi vijijini waliotimkia CCM waapishwwa



Madiwani wateule wawili  waliopita bila kupingwa kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, wameapishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ili kuungana na madiwani wengine katika kuwahudumia wananchi.

Madiwani waliopishwa ni Diwani wa Kibosho Magharibi Deogratius Mushi na Bertin Mkami wa Uru Shimbwe, ambao kabla ya kutimkia CCM, walikuwa ni Madiwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Madiwani hao walikula kiapo  hicho katika Mahakama ya Hakimu  Mkazi Moshi mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi Julieth Mahole na kushuhudiwa na viongozi wa CCM mkoa na Wilaya, Wataalamu wa halmashauri pamoja na wananchi waliohudhuria tukio hilo.

Awali madiwani kabla ya kuapishwa kwao madiwani hao walikabidhiwa Hati ya kuchaguliwa kwa madiwani na Msimamizi wa Tume ya uchaguzi Moshi Vijijini ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Kastori Msigala.

“Kwa Mujibu wa kifungu cha 82(a) cha Sheria ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa sura ya 292 wamechaguliwa kuwa madiwani wa kata ya Kibosho Magharibi na Kata ya Uru Shimbwe hivyo kwa Mamlaka niliokabidhiwa napenda kuwakabidhi leo Hati ya kuchaguliwa kwao kuwa madiwani,”alisema Msigala. 

Diwani Deogratius Mushi akipokea hati kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Moshi Vijijini Kastory Msigala
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Hati ya kuchaguliwa kuwa diwani wa Kibosho Magharibi Deogratius Mushi alisema kwamba sasa anakwenda kufanya kazi kwa kutekeleza Ilani ya CCM yam waka 2015/2020.

“Nilikuwa natamani sana kuitumikia Ilani hii ya CCM kwa muda mrefu, hivyo kukabidhiwa hati hii ninakwenda sasa kumsaidia Rais Dkt Magufuli kwa ari kubwa,” alisema Mushi.

Diwani Uru Shimbwe Bertin Mkami alisema amepata chama ambacho kina ilani inayotekelezeka , kwani hapo mwanzo alikuwa anabahatisha  kufanya kazi bila kuwa na muongozo.
STORY & PHOTO BY: Kija Elias
EDITED BY: Jaizmela Desk


0 Comments:

Post a Comment