Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kimesema hakijapendezwa na kitendo cha mwanasiasa kuchafua tasnia ya siasa kwa kumpa ujazito mwanafunzi wa sekondari wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Hai Laurence Kumotola Kumotola, alisema kuwa siasa ni kioo cha jamii kwani maisha ya kila siku yanategemea uwepo wa tasnia hiyo na endapo itaonekana kufanya vibaya basi huchafua hata wanasiasa wengine ambao wapo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa moyo mkunjufu.
Hayo yanajiri baada ya Diwani wa Kata ya Masama Mashariki kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Munis kupandishwa mahakamani kwa tuhuma za kumpa ujauzito mwanafunzi wa shule ya sekondari Malile iliyopo wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
“Tunaiomba serikali na vyombo vyake vyote kuchukua hatua kali kwa wale wote waliofanya vitendo hivyo na kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Hai, kimechukizwa na kitendo hicho cha Diwani huyo kuwa sehemu ya watu wanao katisha masomo wanafunzi wa shule kwa kuwapa mimba,”alisema Kumotola.
Aidha Kumotola aliwaomba viongozi wa dini kulaani vitendo hivyo vibaya na kukemea matukio ya kuwapa mimba, kuwalawiti wanafunzi na kukatisha ndoto zao za kuendelea na masomo.
Alisema katika mazingira ya kutatanisha unapotembea na mwanafunzi ambaye yupo chini ya miaka 18, hilo ni suala la ubakaji, hivyo hatuwezi kuona Chama Cha Mapinduzi kinaridhishwa na mwenendo wa kiongozi kumpa mimba mwanafunzi.
“Badala ya kiongozi kuwaongoza wanafunzi ili waweze kupata elimu yao ambayo itawasaidia kimaisha yeye anakuwa sehemu ya kushiriki kuwarubuni na kushiriki nao kingono, hiki ni kitendo ambacho hatuwezi kukivumilia,”alisema.
Mbali na hilo Kumotola aliweka bayana mikakati ya kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini Oktoba mwaka huu, ambapo alisema CCM wilayani humo imejipanga vizuri katika kushiriki vyema uchaguzi huo.
“Hivi karibuni Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC, kupitia kwa Mwenyekiti wake Jaji Semistocles Kaijage, imetangaza kuanza kwa mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura , kwa wale ambao wamehamia ama kupoteza kadi zao za kupigia kura, hivyo Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Hai, kinawasihi na kuwaomba wananchi wote kujitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao ili kuwa na uhalali wa kuwa mpiga kura mwaka 2020,”alisema Kumotola.
Aidha Katibu huyo aliwaomba wana CCM wilaya hiyo kujiandaa vyema katika kufanikisha zoezi la uchaguzi huo na kwamba ni wakati muafaka kwa wakazi wa wilaya ya Hai, kurekebisha makosa ambayo waliyafanya katika kipindi cha mwaka 2014, kwa baadhi ya vijiji na vitongoji kwa kuwachagua watu ambao sio sahihi.
0 Comments:
Post a Comment