Thursday, June 20, 2019

Mwenge wa Uhuru 2019 waanza mkoa wa Kilimanjaro


Mwenge wa Uhuru  mwaka 2019 umeanza kutimua mbio zake mkoani Kilimanjaro, ambapo unatarajia kutembelea miradi 35 yenye thamani ya shilingi bilioni 41.6 kwenye halmashauri saba za mkoa huo.

Mwenge huo wa Uhuru unatarajia kupitia miradi mbalimbali  ikiwemo ile ya kilimo, afya, elimu, maji, na barabara.

Akizungumza mara baada ya kuupokea Mwenge wa Uhuru huo, ukitokea mkoani  Manyara, Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt Anna Mghwira alisema kuwa Mwenge wa Uhuru  ukiwa mkoani humo,  utapata fursa ya kupitia jumla ya miradi 35 ya maendeleo katika halmashauri saba za mkoa huo.

Alisema Mwenge wa Uhuru, utatembelea miradi miradi 14 ambayo itafunguliwa, kuzinduliwa , miradi sita itawekewa  mawe ya msingi na miradi 12  itatembelewa na baadhi ya miradi hiyo wahusika watapatiwa mikopo.

“Miradi ya Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2019 imechangiwa na Serikali na wadau wengine wa maendeleo , Serikali Kuu imechangia shilingi bilioni 11,111,930,581, Halmashauri za wilaya na Manispaa shilingi 187,360,244, shilingi 201, 096,859 ni nguvu za Wananchi, Wahisani shilingi 30,062,401,466,”alisema Dkt Mghwira.

Akizungumzia  kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2019" “MAJI NI HAKI YA KILA MTU, TUTUNZE VYANZO VYAKE NA TUKUMBUKE KUSHIRIKI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA." Dkt Mghwira alisema kuwa mkoa wa Kilimanjaro umebahatika kuwa na vyanzo mbalimbali vya maji zikiwemo chemchemu , mito, maziwa mabwawa visima virefu na vifupi ikiwa ni pamoja na uvunaji wa maji ya mvua.

Aidha Dkt Mghwira alisema kuwa idadi ya watu wanaoishi vijijini wanaopata huduma ya maji ni asilimia 80 ambapo  kwa Manispaa ya Moshi wakazi wa maeneo hayo wanapata maji safi na salama kwa asilimia 99.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Siha Onesmo Buswelu, alisema katika halmashauri hiyo Mwenge wa Uhuru utatembelea miradi mitano yenye thamani ya shilingi  bilioni 15.2 ambapo Mwenge wa Uhuru utaweka jiwe la msingi mradi mmoja, utazindua miradi mitatu na kutembelea miradi miwili.

Akizungumza kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru  kitaifa  mwaka 2019 Mzee Mkongea Ally, aliwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru.

“Nawapongeza kwa taarifa nyenu nzuri ya Mwenge wa Uhuru katika mkoa wenu wa Kilimanjaro, natarajia kukuta miradi ya maendeleo yenye thamani ya fedha mlizonitajia hapa inaendana na thamani ya fedha hizo,”alisema Ally.

Mwenge wa Uhuru umepokelewa katika eneo la kijiji cha Ormelili wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, ukitokea mkoani Manyara, , ambapo utakimbizwa mkoani Kilimanjaro kwa siku Saba na Juni 27 mwa huu utakabidhiwa mkoa wa Tanga.

STORY & PHOTO: Kija Elias

0 Comments:

Post a Comment